Madina sasa awaita Wakenya, Waganda

Baada ya kushinda michuano mitatu mikubwa nchini Zambia na Uganda, Mtanzania Madina Iddi anawasubiri tena Wakenya na Waganda jiini Arusha ambako mashindano ya wazi ya gofu ya wanawake yatafanyika katikati ya mwezi huu.

Yakijulikana kama Tanzania Ladies Open, haya ni mashindano ya gofu ya siku tatu ambayo yatapigwa katika mashimo 54  ya viwanja vya gofu vya Arusha Gymkhana kuanzia Septemba 13 hadi 15 mwaka huu, kwa mujibu wa kalenda ya chama cha gofu ya wanawake nchini, TLGU.

“Nitafurahi kucheza nao hapa nyumbani kwani ujio wa wachezaji nyota kutoka nje ya Tanzania huinua hadhi ya mashindano na aghalabu husaidia kutuandaa kwa michezo ya kimataifa,” alisema Madina  na kuahidi kutowaangusha Watanzania katika viwanja vya  nyumbani.

Kwa mujibu wa Madina, michuano ya Tanzania Ladies Open pia itakuwa ni mtihani mzuri kwa wachezaji wa Tanzaania ambao hivi karibuni walifanya vizuri katika mashindano ya wazi ya wanawake nchini Kenya, Uganda na Zambia  kwani yatawapa nafasi ya kuthibitisha ubora wao katika  viwanja vya nyumbani kama walivyofanya ugenini.

Licha ya Madina aliyeshinda mataji matatu, wachezaji wengine kama Hawa Wanyeche,Neema Olomi, Vicky Elias na Aalaa Riyaz Somji pia waling’ara katika michuano ya hivi karibuni iliyofanyika nchini Kenya na Uganda.

“Mwezi Agosti ulikuwa mzuri kwa wacheza gofu wanawake kutoka Tanzania, hivyo hii ni fursa nyingine kwetu kuithibitishia dunia kwamba tuko vizuri kwenye mchezo wa gofu,” alisema Madina kutoka klabu ya Arusha Gymkhana.

Licha ya Madina kushinda mataji mawili katika miji ya Kampala na Entebbe, chipukizi Aalaa Somji pia aling’ara kwa kupiga hole-in-One(ace) licha ya kumaliza katika nafasi ya nne wakati Hawa Wanyeche alimaliza wa pili na Olomi wa tatu katika mashindano ya hivi karibuni ya John Walker Uganda Open.

Watanzania watakuwa wakiwasubiri Martha Babirye na Peace Kabasweka ambao walitoa upinzani mkali kwa wanawake wa Tanzania katika mashindano ya wazi ya Uganda na Mkenya Mercy Nyanchama  aliyeshinda katika michuano ya viwanja vitano vya mwambao wa Kenya.

“Tumekwisha anza mazoezi kwa kwenda ‘range’  ili kuboresha upigaji wa mipira pamoja na namna bora ya kuijaza  shimoni (putting),”  alinena Madina.

Licha ya kualika wachezaji kutoka nje ya Tanzania, mashindano ya Tanzania Ladies pia ni wazi kwa wachezaji kutoka vilabu vyote vya gofu vya Tanzania bara na visiwani.

Related Posts