Muswada kifungu cha rushwa ya ngono kutua bungeni kesho, wanaharakati waukataa

Dodoma. Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wa Mwaka 2024 unawasilishwa kesho Jumatatu Septemba 2, 2024 bungeni.

Muswada huo unalenga kurekebisha kifungu cha 25 cha sheria hiyo kinachozungumzia rushwa ya ngono, kwa kuweka kipengele kinachoeleza kwamba lazima kuwepo mtoaji na mpokeaji, ili kitendo hicho kiitwe rushwa.

Hata hivyo, mtandao wa kupinga rushwa ya ngono umewataka wabunge kutoupitisha muswada huo, ukidai unalenga kuwanyamazisha waathirika na kuimarisha nguvu za wenye mamlaka wanaofanya vitendo hivyo.

Mtandao huo umesisitiza kuwa kifungu cha 10(b), kilichoongezwa kwenye mabadiliko hayo kinahalalisha matumizi mabaya ya mamlaka kwa kuwaadhibu waathirika wa rushwa ya ngono kama mbinu ya kuwatishia.

Kifungu hicho kinaeleza kuwa mtu yeyote ambaye amemsababishia mwenye mamlaka kufanya kosa kwa kumuahidi, kumshawishi, au kutoa rushwa ya ngono ili apendelewe, apewe cheo, ajira, au kupandishwa cheo, anakuwa hatiani kwa kosa la rushwa ya ngono.

Rebecca Gyumi, akizungumza hivi karibuni kwa niaba ya mtandao huo, alisema iwapo wabunge watapitisha mabadiliko hayo, watachangia kuiangamiza jamii ambayo imeathiriwa na rushwa ya ngono.

Rebecca aliongeza kuwa rushwa ya ngono imeendelea kuota mizizi na sasa inaathiri hata vijana wa kiume ambao wanaombwa rushwa ya ngono na wanawake wenye mamlaka na wakati mwingine na wanaume wenzao.

Alisisitiza kuwa mabadiliko hayo yanayoelekea kumshtaki pia anayetoa rushwa hiyo yana lengo la kuwanyamazisha waathirika, akisema mara nyingi wanaoomba rushwa hiyo ni watu wenye mamlaka.

Mwanaharakati mwingine, Dk Ananilea Nkya alisema kama wabunge wataruhusu muswada huo kupita, watakuwa wamejichimbia shimo hasa kuelekea kwenye chaguzi zinazotarajiwa kufanyika mwaka huu na mwakani.

Alionya kuwa wabunge wakipitisha mabadiliko hayo wataturudisha nyuma mapambano na itakuwa ni sawa na kuwalinda wanaotenda vitendo hivyo.

Dk Ananilea alitoa ushuhuda wake wa jinsi alivyoathirika na rushwa ya ngono baada ya kunyimwa fursa ya kwenda nje ya nchi kwa kushindwa kukubali matakwa ya bosi wake.

Alisema vitendo kama hivyo vinakatisha tamaa na kuwaangamiza wengi na alisisitiza umuhimu wa kuwawajibisha wale wanaotenda rushwa ya ngono, bila kuwa na namna yoyote ya kuwalinda.

Ushuhuda mwingine ulitolewa na Asha Omary aliyedai aliombwa rushwa ya ngono na daktari aliyekuwa akimtibu bibi yake.

Alidai daktari huyo alimpa sharti la kushiriki naye ngono, ili apate dawa kwa ajili ya bibi yake, hali iliyomweka katika wakati mgumu wa kuamua kati ya kuokoa maisha ya bibi yake au kulinda utu wake.

Katika vikao vinavyoendelea, tayari Bunge limeshapitisha miswada mingine minne ya sheria ambayo inasubiri kutiwa saini na Rais Samia Suluhu Hassan, ili iwe sheria kamili.

Miswada hiyo ni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Shule ya Sheria Tanzania wa Mwaka 2024, Muswada wa Sheria ya Viwanja vya Ndege Tanzania wa Mwaka 2024, Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii wa Mwaka 2024, na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria zinazohusu Ulinzi wa Watoto wa Mwaka 2024.

Katika muswada wa Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii, mabadiliko yameruhusu mwanachama wa mfuko kulipwa mafao bila kujali kama mwajiri amekamilisha kuwasilisha michango yote.

Pia, mabadiliko haya yameruhusu mwanachama kutumia sehemu ya mafao yake kama dhamana kwa mkopo wa nyumba, na mfanyakazi aliyeajiriwa na waajiri zaidi ya mmoja kuchangiwa na waajiri wote kwa ridhaa yake.

Kwa muswada wa kuanzisha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), TAA itakuwa na mamlaka juu ya viwanja vyote vya ndege, vikubwa na vidogo, na kuondoa utata wa kampuni binafsi kuendesha viwanja hivyo.

Pia, muswada wa Sheria za Ulinzi wa Watoto unatoa adhabu ya fidia kwa waathirika, kuanzisha mabaraza na mahakama za watoto, na kutoa mamlaka kwa Mahakama kufuta amri ya kuasili mtoto baada ya kupokea maombi kutoka kwa mzazi, mlezi, au ndugu.

Muswada hiyo inasubiri kutiwa saini na Rais Samia ili iwe sheria kamili.

Related Posts