WIKI chache tangu aiachane na aliyekuwa kocha mkuu, David Ouma, klabu ya Coastal Union ya Tanga inadaiwa imemshusha kimyakimya kocha mpya kutoka Burundi, Domonique Niyonzima ambaye kwa sasa anaendelea kusimamia mazoezi yanayoendelea kambini eneo la Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Licha ya kwamba mabosi wa Coastal bado haijatangaza rasmi juu ya kocha huyo ambaye ni Mshauri wa Ufundi wa FIFA kwa nchi za Magharibi, lakini Niyonzima ana wiki kama moja sasa anahudhuria mazoezi ya timu hiyo kama kawaida.
Chanzo cha kuaminika kutoka Coastal iliyong’olewa hivi karibuni katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikitolewa na AS Bravos ya Angola kilisema kuwa, kocha anasimamia mazoezi akisaidiana na makocha wengine aliowakuta, walioachiwa timu baada ya Mkenya Ouma kupigwa chini.
“Taarifa kamili sina kujua kama ameishasaini mkataba au la, ninachokiona ni yeye kuwepo mazoezini na tayari ameiona timu, anashauri kinachotakiwa kushauriwa,” kilisema chanzo hicho.
Mwanaspoti liliamua kumtafuta katibu wa timu hiyo, Omary Ayubu ili kupata ufafanuzi juu ya taarifa hiyo ya Niyonzima kutua kwa Wagosi naye alijibu kwa kifupi; “Tunazungumza na makocha mbalimbali, hatujafikia nao mwafaka, akiwemo na huyo Niyonzima.”
Licha ya kutotaka kuwataja majina kwa sasa, lakini Mwanaspoti linafahamu kuwa, mbali na Niyonzima, pia Coastal inahusishwa na kutaka kumchukua Kocha Mmarekani Melis Medo, aliyepo Mtibwa Sugar kwa sasa iliyoshuka Ligi Kuu Bara kwenda Ligi ya Champioship.
Mara baada ya kuachana na Ouma aliyeinusuru timu ikiwa mkiani na kuifanya imalize nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu bara iliyopita na kukata tiketi ya CAF, huku pia ikifika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho na kupoteza mbele ya Azam FC, timu hiyo ipo chini ya Joseph Lazaro na Ngawina Ngawina.
Lazaro ni nyota wa zamani wa timu hiyo aliyewahi kutamba pia Yanga, aliyerejeshwa kikosini hapo huku Ngawina akichukuliwa kutoka Singida Fountain Gate aliyoinusuru isishuke daraja.