KIUNGO Mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Zabona Hamis amesema dakika 180 bila timu kupata bao ni huzuni kwao, akieleza kuwa kurejea kwa pacha wake Samson Mbangula makipa wajipange.
Prisons imeanza Ligi Kuu msimu wa 2024/25 kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana katika mechi mbili ilizocheza ugenini dhidi ya Pamba Jiji na Mashujaa na kushtua mashabiki kwa kutofunga bao hata la kuotea.
Hata hivyo, katika michezo hiyo, timu hiyo iliwakosa baadhi ya mastaa wao wazoefu, wakiwamo Nahodha Jumanne Elfadhir na washambuliaji Samson Mbangula na Jeremia Juma.
Katika msimu uliopita, Mbangula na Zabona walitengeneza muunganiko bora wakihusika kwenye zaidi ya mabao saba na kuifanya timu hiyo kuwa tishio chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Ahmad Ally aliyejiunga na JKT Tanzania.
Akizungumza na Mwanaspoti, Zabona alisema kutofunga mabao katika michezo yote miwili ni maumivu sana kwao kama straika akiahidi kuwa mchezo ujao dhidi ya Tabora United kitaeleweka.
Alisema kinachotia matumaini zaidi ni kurejea kikosini kwa straika mwenzake Mbangula ambaye walikuwa na maelewano mazuri tangu msimu uliopita hivyo nyavu za makipa zitaanza kutikiswa.
“Tunaumia sisi washambuliaji kutopata bao, lakini habari njema ni kurejea kwa baadhi ya wachezaji wenye uwezo na uzoefu na matarajio ni kwamba tutaanza kuwapa raha mashabiki”
“Bado ni mapema mechi za ugenini zina matokeo yake, lakini hatuwezi kuogopa timu yoyote na kwa sasa tunajiandaa dhidi ya Tabora United Septemba 14 kuanza kazi rasmi” alitamba staa huyo.