ONGEA NA ANTI BETTIE: X wangu anaelekea kusambaza picha zetu za faragha

Swali: Anti, nimekuja kuomba ushauri nimfanye nini mpenzi wangu ambaye tangu tumeachana kazi yake ni kunifuatilia kila ninachokifanya.

Kibaya zaidi amekuwa akitukana na kunikashifu kupitia mitandao ya kijamii, anazunguka sana anapotimiza azma yake hiyo, lakini ninajua kwa sababu anazungumzia vitu tulivyokuwa tukifanya pamoja.

Kukaa kwangu kimya ndiko kunakomuudhi, maana hajasikia nikipata shida wala kumuomba turudiane licha ya kuniacha na mtoto bila matunzo. Hofu yangu huko anakoelekea ataweka mtandaoni hata picha tulizopiga tukiwa kwenye uhusiano, kwani lengo lake ni kunidhalilisha na kutaka nipate tabu. Mbali na mitandaoni amekuwa akinichafua kwa ndugu, jamaa na marafiki akizungumza vitu vya uongo kunihusu na sijamjibu hata siku moja.

Naomba ushauri nifanyeje, maana simuelewi kabisa huyu mwanaume.

Jibu: Pole sana ila nianze na wewe. Ilikuwaje mpaka ukapiga picha ambazo unahisi zikiachiwa zitakuchafua?

Ina maana mapenzi hayanogi bila kupiga picha, hujasema ni mbaya au nzuri lakini kwa hofu uliyoonyesha zitakuwa hazina maadili. Kuanzia sasa hata iweje, umpende vipi mwanaume, awe mumeo sponsa na mambo mazuri kama hayo, achana na ushamba wa kupiga picha zisizo na maadili. Kwanza unajikosea heshima hata wewe mwenyewe, unajisikiaje kupiga picha za ovyo. Achana kabisa na hiyo habari.

Pia acha kufuatilia kwenye kurasa za huyo mwanaume, siyo lazima na ukiacha hautakufa. Usipoangalia hutajua kaandika nini, unasema anakufuatilia na wewe unamfuatilia ndiyo maana unajua habari zake.

Kuhusu kukuchafua kwa jamaa zako au zake, mtu akianza tu kukuambia habari za huyo bwana mwambie hutaki kuzisikia. Ukiwakatalia wawili, watatu wataambiana na habari itaishia hapo.

Ushauri wangu muhimu ni kwenda kutoa taarifa hasa katika kitengo cha makosa ya mtandao kuhusu anachokifanya huyo bwana. Lakini uwe na ushahidi wa moja kwa moja kwa hisia tu hakuna atakayekuelewa. Au elezea ana picha mlizopiga pamoja ambazo kwa mwenendo wake unahisi anaweza kuziachia ili apewe onyo mapema.
 

Ana wivu mpaka anatishia kuniachisha kazi

Nimeolewa huu mwaka wa nne, lakini sioni nikitoboa, mwenzangu kama anataka kuchanganyikiwa kwa wivu. Huwezi kuamini kuna kitu amefanya simu zangu zote zikipigwa anazisikiliza, niliweka pasiwedi ni kosa kama nimeua.

Anachiniudhi anajibu hadi ujumbe mfupi kulingana na anavyotaka, kuna watu nawaheshimu ameshawajibu vibaya vibaya hawataki hata kunisikia hamuamini mtu yoyote mpaka ndugu zangu. Pia hana adabu hata kidogo. Jambo la kushangaza hakuwa hivi, hata sielewi hizi tabia zimetoka wapi?

Amekuwa na wivu mpaka apoteze mwelekeo kazini. Kuna siku alisema ataniachisha kazi muda si mrefu na atakuwa ananifungia ndani. Hofu yangu akiniachisha kazi nitakuwa mgeni wa nani na anaweza kufanya hivyo kwa sababu hamuogopi mtu hata wazazi wake hawasikilizi. Alikuwa kijana mwelewa sana sijui nini kimetokea.

Kwanza kuwa makini sana, huyu mumeo inawezekana amepata shida ya afya ya akili. Unasema huko nyuma hakuwa hivyo ina maana hayo ni mabadiliko makubwa ya tabia, ambayo mara nyingi hayapaswi kupuuzwa.

Anatakiwa apate mtaalamu wa afya ya akili azungumze naye kumuweka sawa. Kama kuna rafiki yake unayeamini wanaelewana mtumie huyo. Kwa kuwa amebadilika akielezwa sidhani kama atasikia, hivyo mwanzoni huyu rafiki yake au wewe mmoja ajifanye ana shida hiyo hivyo amsindikize kuonana na daktari.

Madaktari wa haya matatizo wanajua jinsi ya kufanya hivyo ashirikishwe kuwa anayekuja kutibiwa si mgonjwa bali msindikizaji ndiyo mwenye shida atajua afanye nini kumuingiza kwenye matibabu na ushauri. Ila muhimu usichukulie poa kabisa hiyo hali anaweza kufanya lolote.

Pili, huu ni ushauri muhimu sana, kumpuuza Mungu kwenye ndoa ni kosa kubwa linalofanywa na wanandoa wengi ni kutomshirikisha Mungu kwenye maisha yao.
Sisemi kuwa wanaofanya hivyo hawapati changamoto, hapana. Majaribu kila mwanadamu anapitia, lakini Mungu ni ngao, kuliko kuendekeza anasa. Nyumbani kwenu kukiwa na maisha ya hofu ya Mungu hizi changamoto ndogondogo zinapungua sana.

Pia mpe mumeo nafasi inawezekana ulimtelekeza ukahamishia mapenzi kwenye vikoba na marafiki akaona labda una mtu mwingine, ndiyo maana amekuwa na wivu. na kubadilika tabia kabisa. Siku hizi wanawake wapo bize sana na kutafuta maisha kiasi cha kusahau asili yao kuwa ni mama wa familia na mke wa mtu.

Tenga muda wa kuzungumza naye, mpe nafasi unaweza kujua wivu wake kupitiliza umetokana na kitu gani.

Najua kazi ni kipimo cha utu, lakini inaweza kututenga na mumeo, familia usipokuwa makini. Gawa vizuri na kwa weledi muda wa kazi na wa mumeo hii itasaidia kumtuliza kidogo. Inawezekana kabisa upo bize na kazi na awali haukuwa hivyo.
 

Sijui wanawake wakati mwingine wanataka nini

Nilikutana na huyu mpeni wangu akiwa hana amani, ana mawazo na anajiona kama asiye na bahati.

Nikajitahidi kumpa kampani na kumueleza ni kwa namna ni wa thamani. Mwanzoni sikumueleza nia yangu ya kumpenda kwa sababu hakuwa sawa, tumekuwa marafiki wa kawaida karibu miezi 10 mpaka nilipoona amekaa sawa na ananielewa nikamweleza nia yangu na kweli tukawa wapenzi.

Nikafanya taratibu za kutoa poa kwao na kumlipia mahari tukaanza kuishi kabla hatujafunga ndoa, hivyo ni kitambo kidogo tupo pamoja. Shida yake inayonichosha na kunikera ni kutaka kila kitu nifanye kama X wake.

Ukikosea kitu kidogo anaanza kusema X wake hakuwa akifanya hivyo. Mara fanya kama alivyokuwa anafanya X wake, kila unachomwambia mfano ni huyo. Kinachonichosha kabisa tukiwa faragha analalamika simkati kiu kama alivyokuwa akikatwa na X wake.

Hii imekuwa ndiyo kesi yetu kuu, analalamika kila ninavyojitahidi kuwa simkolezi kama jamaa.

Sasa nawaza nimuoe au tuishie hapa? Maana naona bado ana wenge la jamaa lisije kunisumbua huko mbele ya safari.

Pole sana. Kila ukijitutumua mwenzako anawaza shoo ya jamaa. Hiki tatizo, ina maana X wake siku atakayomtania warudiane anakuacha mchana kweupe.

Baadhi ya wanawake wamejaaliwa kuwapenda wasiokuwa na muda nao. Kabla hamjafunga ndoa hakikisha hili wenge la X linamtoka kichwani, tofauti na hapo fikiria vinginevyo. Kwanza ni utovu wa adabu mwanamke kumtaja mwanaume mwingine mbele ya mpenzi wake wa sasa iwe kwa kumsifu au kumkashifu.

Huyu hana adabu kabisa. Haijalishi unamkoleza au humkolezi suluhisho siyo kukufananisha na X wake, mnapaswa mtafute pamoja njia ya kufikishana maana amefungua ukurasa mpya wa mahusiano. Sasa kaa naye na umeelezwa kwa kituo ukiwa umetulia siyo kwa jazba ila kwa msisitizo achague anarudi kwa X wake ili wakaendelee walipoishia au anaendelea na wewe moja kwa moja na aache kukufananisha naye.

Anapaswa akujibu kwa usahihi na ajutie kosa lake, majibu yake na namna anavyokuhakikishia kutorudia yatakupa picha kama uendelee na safari au subiri kidogo, kikujibu kwa kukushangaa kuwa haoni kama anakosa kumtaja mpenzi wake wa zamani ujue hapo hakuna kitu ipo siku watarudiana maana anampenda sana. Pia akiwa mbogo kwenye majibu nalo usilipuuze inamaanisha huyo mtu bado ni muhimu kwenye maisha yake.

Sikutumi uwe na wivu, hapana. Ila fuatilia nye do zake pengine wameanza kuwasiliana wasiliana. Usikatishe safari hadi ujiridhishe kuwa imeshindikana kumtenganisha mpenzi wako na mawazo ya jamaa.

Baada ya kikao hiki naamini utaona mabadiliko kama mpenzi wako ameteuliwa usipoyaona fikiria mara mbili, usije kuoa mwili akili ipo kwa mtu mwingine.

Related Posts