Patwa, Khan waipaisha Mikumi | Mwanaspoti

MIKUMI imefanikiwa tena kuishinda Ngorongoro  katika mchezo wa pili wa majaribio kwa wachezaji nyota wa timu ya taifa ya kriketi uliopigwa jijini katika uwanja wa Anadil Burhan mwishoni mwa juma.

Timu hizi ni kombaini zinazoundwa na wacjhezaji wa timu ya taifa kwa ajili ya kuwaandaa kwa michezo ya kufuzu fainali za kombe la dunia ambapo Tanzania imepangwa kumenyana na Mali mwishoni mwa mwezi huu.

Tofauti na mchezo  uliopita ambapo Mikumi waliibuka na ushindi mkubwa  mikimbio 35, safari hii Ngorongoro walionyesha upinzani mkubwa kiasi cha kuwafanya vijana wa Mikumi kushinda kwa taabu.

Licha ya kushinda mechi yao ya pili, vijana wa Mikumi iliwabidi kufadanya kazi ya ziada kabla  ya kuchomoza na ushindi  wa mikimbio 17.

Katika mchezo huo wa mizunguko 20, Mikumi ndiyo walipata kura ya kuanza na kuamua kubeti, na azma yao iliwafikisha kwenye mikimbio 151 huku wakipoteza wiketi 6 baada ya kumaliza mizunguko yote 20.

Jitihada za Ngorongoro kuzifukuzia alama za wapinzani wao ziligota kwenye mikimbio 134 huku wakipoteza wiketi 6 baada ya kumaliza mizunguko yote 20 na hivyo kuwafanya Mikumi watoke kifua mbele kwa ushindi wa mikimbio 17.

Abhik Patwa aliyetengeneza mikimbio 47 na Zafar Khan aliyeleta mikimbio 46 ndiyo walikuwa vinara wa mikimbio kwa timu ya Mikumi.

Halid Amiri na Laksh Snehal walifanya kazi nzuri kwa timu Ngorongoro  baada kila moja wao kuishinda wiketi 2, lakini jitihada zao zilishindwa kuisadia timu yao kushinda.

Kikiwa na azma ya kuzinoa timu za taifa  za kriketi za wanaume na wanawake, Chama cha kriketi nchini, TCA pia iliandaa mechi kati ya taifa ya wanawake  na timu ya Patel B ambao waliibuka na ushindi  wa wiketi7.

Timu ya TCA Combine ndiyo iliyoanza kubeti na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 73 baada ya wapigaji wao wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 16 kati ya 20 iliyowekwa.

Ilikuwa ni ‘score’ ndogo sana kwa vijana wa Patel B kwani waliweza kuivuka kirahisi kwa kupata mikimbio 76 huku wakipoteza wiketi 3 baada ya kutumia mizunguko 12 kati ya 20 iliyopangwa na hivyo kushinda kwa wiketi 7.

Licha ya timu yao kufungwa, Perice Zakayo  aliyetengeneza mikimbio 22 na Swaumu Godfrey  aliyeleta mikimbio 13 walionyesha ustadi mkubwa wa kutengeneza mikimbio.

Related Posts