Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha amemtaka Waziri kivuli wa katiba na sheria wa chama cha ACT- Wazalendo, Maharagande Mbarala, kuthibitisha tuhuma alizotoa kuhusu mauaji ya watu wilayani Kaliua.
Pia amemtaka kuthibitisha tuhuma za kuwapo kwa ukiukwaji wa haki za binadamu katika vijiji 11 vyenye mgogoro wa ardhi unaofanywa na wenye mamlaka.
Akizungumza leo Jumapili Septemba Mosi, 2024, wakati wa hafla ya kuchangia ujenzi wa ofisi ya jimbo na Shule ya Kisili Laiser katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), alikomuwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko, Chacha amesema kuna haja ya Maharagande Mbarala kuthibitisha tuhuma hizo.
“Juzi wamekuja watu kutoka Kaliua na kuita vyombo vya habari, yule bwana wa ACT akasema Tabora, Kaliua kuna mauaji ya kutisha, jeshi la wananchi limenyanyasa na kuua watu, wanabakwa na kulawitiwa na nyumba zaidi ya 7,000 zimechomwa, jambo ambalo si la kweli,” amesema Chacha.
Amesema kauli kama hizo hazipaswi kuachwa zikaendelea kusambaa; “huyu mtu anatakiwa atuonyeshe watu waliouawa walikufa wapi? Familia zao ni zipi, walizikwa wapi Ili tuchukue hatua kwa mtu aliyefanya uhalifu huu. Watu waliobakwa na kulawitiwa walifanyiwa hivyo wapi na ni kina nani hao,”amesema.
Chacha amesema tayari amezungumza na wanasheria wa masuala ya maliasili na akasisitiza umuhimu wa kudhibiti taarifa zisizo sahihi kwa kuwa zimelitaja Jeshi la Wananchi wa Tanzania, jambo linaloweza kuleta taharuki isiyo ya lazima.
“Huko Kaliua natembelea kila siku, haya mambo yapo kweli? Nimesema huyu mtu afikishwe kwenye vyombo vya sheria atupe ukweli,” amesema, Chacha.
Akizungumza na Mwananchi Digital kuhusu suala hilo, Maharagande Mbarala amesema hajapokea wito wowote mpaka sasa wa kuhojiwa kuhusu kile alichokisema.
Bali amesisitiza kama taarifa alizotoa ni za uongo, ashitakiwe mahakamani.
“Taarifa nilizotoa ziko sahihi, maana tulimtuma mtu kukaa Kaliua kwa miezi mitatu kufanya uchunguzi na alikuja na takwimu za kutosha kuhusu madai hayo. Pia mimi na kiongozi mstaafu wa chama tulifika Kaliua na kukuta malalamiko hayo hayo,” amesema Mbarala.
Amesema ACT- Wazalendo kilishamuambia Rais Samia Suluhu Hassan kuunda kamati ya uchunguzi wa haraka na pia Bunge liunde kamati ya kuchunguza kinachoendelea Kaliua, ili majibu yapatikane kusudi haki za watu zisipotee.
Awali, taarifa ya ACT- Wazalendo kupitia kwa Mbarala ilidai kuwa vijiji 11 vikiwamo Usinge, Luganjo, Igalala namba 3, Igalala namba 4, Igalala namba 7, Igalala namba 9, Kombe, Tuombe Mungu na Limbu la Siasa vinapitia unyanyasaji wa haki za binadamu, ikiwemo wanawake kubakwa na kulawitiwa, nyumba zaidi ya 7,000 kuvunjwa na mali za wananchi ikiwemo mifugo kuporwa.