NYOTA wa kimataifa wa Tanzania na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta mwezi huu anatajiwa kuanza kucheza mechi za michuano ya Ligi ya UEFA Europa League akiwa na klabu ya PAOK ya Ugiriki, huku akitarajiwa kuja kukutana uso kwa uso Man United, Novemba 7 mwaka huu.
Katika droo ya michuano hiyo inayoendeshwa kwa mtindo wa ligi tofauti na ilivyokuwa zamani kuchezwa makundi, iliyofanyika jijini Monaco, Ufaransa, PAOK ya Samatta ikipangwa chungu namba mbili na Lyon, Fenerbahce, Real Sociedad, Braga, AZ Alkmar, Olympiacias, M.Tel Aviv na Ferencvaros.
Baada ya upangwaji wa ratiba ni kwamba PAOK itaanza mechi ya kwanza dhidi ya Galatasaray iliyokuwa chungu namba tatu siku ya Septemba 25 kisha kuvaana na FCSB Oktoba 3 na wiki moja baadae itaumana na Viktoria Plzen.
Pia timu hiyo itakuja kukutana na Man United Novemba 7 kisha RFS Novemba 28 na Desemba 12 itacheza na Ferencvarosi na kabla ya kuumana na Slavia Prague Jan 23 na wiki moja baadae itamaliza mechi hizo dhidi ya Real Sociedad.
Hata hivyo, Samatta amekuwa hana nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza kiasi iliezwa alikuwa akiwindwa na klabu kadhaa za Cyprus kabla ya dirisha la usajili barani Ulaya kufungwa wikiendi iliyopita naye akisalia kikosini hapo.
Mara ya mwisho Samatta kuonekana uwanjani ilikuwa Julai 31 mwaka huu katika mechi ya Ligi dhidi ya Borac Banja Luka akikaa benchi, huku timu yake imecheza mechi nane za mashindano mbalimbali lakini Mtanzania huyo hakuwepo hata benchi.
Hata hivyo, amekutana na ugumu eneo la ushambuliaji mbele ya Mmorocco Tank Tissoudali aliyesajiliwa msimu huu akitokea Gent ya Ubelgiji aliyefunga mabao 43.