Serikali kugharimia matibabu ya majeruhi Hanang

Babati. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema Serikali itagharamia matibabu kwa wanafunzi majeruhi wa ajali ya magari mawili yaligongana na kusababisha vifo vya watu wanne jana.

Sendiga ameyasema hayo leo Jumapili Septemba Mosi, 2024 baada ya kuwatembelea majeruhi wa ajali hiyo ambao wamelazwa Hospitalini ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, mjini Babati.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Gajal wilayani Hanang na kusababisha vifo vya wanafunzi watatu wa Shule ya Sekondari Endasak na dereva wa basi dogo aina ya Coaster baada ya kugongana na lori.

Waliofariki dunia kwenye ajali hiyo ni Lydia Saitoti Nanyaro (17), Aisha Rahim Mollel (19) Samira Halid Manyampanda (18) na dereva Ally Ramadhan Abdala (36).

Sendiga akizungumza wakati akiwapa pole majeruhi hao hospitalini hapo, amesema Serikali itagharamia matibabu yote.

“Poleni sana watoto wetu kwa ajali hiyo na tunatoa salamu za rambirambi kwa wafiwa wote wa ajali hiyo na tupo pamoja kwenye kipindi hiki kigumu,” amesema Sendiga.

Kwa upande wake Mganda Mkuu wa Mkoa wa Manyara (RMO), Andrew Method amesema walipokea majeruhi 30.

“Majeruhi wanane wameruhusiwa jana ile ile baada ya kupatiwa matibabu na wengine wataruhusiwa kadri tunavyoendelea kuwapa huduma na afya zao zinavyoimarika,” amesema Dk Method.

Akizungumzia ajali hiyo,  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani amesema chanzo ni uzembe wa dereva wa lori aina ya Scania aliyelipita gari jingine bila kuwa na tahadhari.

Kamanda Makarani amesema wanafunzi hao walikodisha basi hilo dogo wakielekea likizo majumbani mwao baada ya shule hiyo ya Endasak kufungwa Agosti 30.

Related Posts