Dar es Salaam. Wadau wa elimu wameitaka Serikali kuanza kutenga fedha itakayotolewa kwa shule zote nchini kama ruzuku ili kufanikisha azma yake ya wanafunzi wa shule za kutwa kupata chakula cha mchana.
Wamesema hayo baada ya Serikali kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuhakikisha wanafunzi wa shule za kutwa za umma na binafsi wanapata chakula bila kujali madarasa.
Pia, imezitaka kamati za shule kuimarisha usimamizi wa chakula kinachotolewa na wazazi kwa ajili ya mpango wa chakula shuleni.
Agizo hilo lilitolewa na wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohammed Mchengerwa katika mkutano wa tathimini ya mkataba wa lishe na kutambulisha Mpango wa Taifa wa Uwekezaji katika afya ya mama na matoto nchini uliofanyika Dodoma kuanzia wiki iliyopita.
Mchengerwa amewataka wakuu hao kuendelea kusimamia kikamilifu fedha zote zinazopangwa kwa ajili ya kutekeleza afua za lishe na kusimamia ubora wa taarifa ili zinazoletwa katika ngazi za juu ziwe zinaakisi uhalisia katika jamii.
“Kwa shule za bweni zinazopata fedha kwa ajili ya chakula ni vyema kuhakikisha chakula kinachotumika mashuleni ni kile kilichoongezewa virutubishi,” amesema Mchengerwa.
Ameelekeza wazabuni wa chakula shuleni kupeleka chumvi yenye madini joto,unga na mafuta ambayo hayameongezwa virutubishi
Kwa mujibu wa Takwimu za Msingi za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hadi Desemba 2023, Tanzania ilikuwa na jumla ya shule za msingi 19,733 na 5,926 za sekondari idadi ambayo huenda imeongezeka mwaka huu.
Akizungumzia suala hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Luka Mkonongwa amesema kutoa chakula kutasaidia kuongeza ari ya kusoma kwa watoto.
“Wengi walikuwa wakishindwa kusikiliza vizuri darasani mchana, kutoa chakula ni mwanga wa kuonesha watoto wetu watakuwa wanafanya vizuri, kwa mikoa inayotoa chakula matokeo yanaonekana na hii itamuwezesha hata mwalimu kupanga ratiba ya kufundisha baada ya saa nane,” amesema Dk Mkonongwa.
Hata hivyo, Dk Mkonongwa amesema ni vyema kutowaachia wazazi wachangie peke yao chakula hicho kwa sababu inaweza kuwagawa watoto kutokana na vipato vya wazazi kutofautiana.
“Kama kitendo hicho kimeonekana kuwa na faida basi Serikali iandae bajeti kwa ajili kuhudumia chakula kwa wanafunzi kwa kutoa ruzuku. Ni suala la kujipanga vizuri kwa sababu mtoto mwenye afya nzuri ndiyo anaweza kufanya vizuri, mtoto bila chakula elimu yake inatetereka sana,” amesema Dk Mkonongwa.
Suala hilo liliungwa mkono na Mtafiti wa Elimu, Muhanyi Nkoronko ambaye amesema huenda wapo wazazi wanaoweza kushindwa kumudu utoaji wa gharama za chakula, hivyo ni vyema kuwapo na njia inayoweza kuhusisha Serikali, wazazi na wadau wa maendeleo.
“Katika ruzuku za uendeshaji wa shule zinatozotolewa inaweza kuwekwa namna kwa asilimia fulani ikatolewa kwa ajili ya chakula. Serikali itoe kiwango fulani na wazazi wajazie katika kile kinachotolewa na Serikali ili wanafunzi wote waweze kula,” amesema Nkoronko.
“Kuna ya nchi ambazo zinatoa chakula na Serikali zao zikifadhili mpango huu kwa asilimia 100 hivyo hili linawezekana. Inawezekana sana na sehemu ya fedha hizi zinaweza kutoka katika bajeti ya Tamisemi na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.”
Amesema tafiti zinaonesha utolewaji wa chakula kutamfanya mwanafunzi kuhudhuria shule bila kuwa na sababu za kutoroka.
Nkoronko amesema tafiti zaidi katika elimu zinaonyesha kuwa watoto wanapokwenda shuleni huwa na njaa, hivyo kuwapo kwa chakula kutawafanya wanafunzi kupata utulivu.
“Mwalimu atakuwa na uwezo wa kuwapa maarifa stahiki. Pia, utoaji chakula utaondoa utoro wa rejareja ambao awali mwanafunzi alitumia muda wa mapumziko kurudi nyumbani kupata chakula kabla ya kwenda tena shuleni lakini muda huu ndiyo kuna vishawishi mbalimbali anavyoweza kukutana navyo vikamzuia kufika shuleni,” amesema Nkoronko.
Amesema safari ya wao kwenda nyumbani na kurudi huondoa utulivu katika masomo, pia baadhi wanapofika nyumbani hawana uhakika wa kukuta chakula.
Nkoronko amesema wakati mwingine utekelezaji wa suala hilo unaathiriwa na namna jamii inavyoitafsiri sera ya elimu bila malipo ya ada, jambo linalowafanya kujiona si sehemu ya michango ya Serikali.
“Jamii iliona kuwa kila kitu kitagharamiwa na serikali na bahati mbaya baadhi ya viongozi walikuwa na tafsiri potofu juu ya utoaji wa elimu bila malipo jambo ambalo liliwafanya waendelee kusubiri kila kitu kufanywa,” amesema Nkoronko.
Amesema kuna haja ya kutoa elimu kwa jamii ili kuwaonyesha thamani na maana ya wao kuchangia katika utoaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni na kutoa elimu juu ya zana ya utaoji wa elimu bila malipo.
“Si chakula tu, jamii pia lazima itambue kuna vitu vingi vinapaswa kufanyika ikiwemo kuchangia gharama za upishi ili kuhakikisha kila kitu kinapikwa ipasavyo,” amesema Nkoronko.
Katika kikao hicho cha tathmini kilichofanyika jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema katika kuhakikisha mikataba ya lishe inatekelezwa kwa tija, wizara itahakikisha inakamilisha haraka Sera ya Taifa ya Chakula na Lishe na kushirikiana na sekta binafasi ili chakula cha watoto mashuleni kiongezewe virutubisho.
Alitumia nafasi hiyo kuwaomba wakuu wa mikoa na wilaya kujipanga kutoa elimu kuhusu bima ya afya kwa wote na kuhakikisha wanafanya kampeni ya mtu ni afya ili kuondoa magonjwa ya mlipuko hasa kipindupindu.
“Kwa uwekezaji ambao umefanywa na Serikali katika utoaji wa huduma za afya tukishindwa kukiondoa kipindupindu tutakuwa hatujitendei haki sisi Watanzania,” amesema Mhagama.
“Pia, twendeni tukapambane tukahakikishe ugonjwa wa homa ya nyani hauingii ndani ya nchi yetu, tukishakosea kidogo na ugonjwa ukaingia nchini madhara tutakayopata ni makubwa na kuundoa inaweza kuwa kazi ya ziada.”