Arusha. Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Dar es Salaam, imewaachia huru watu watatu akiwemo aliyekuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Said Makumbusya waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji.
Katika kesi hiyo ya mauaji namba 30 ya mwaka 2023, mbali na Sajenti Said, washitakiwa wengine ni Hadija Athuman na Zamda Bilali waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya kumuua Yassir Mpakanjia (17).
Watuhumiwa hao walikuwa wakishitakiwa kwa kumuua kijana huyo wakidai kuwa alikuwa mwizi.
Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na mama wa marehemu, mmoja wa watuhumiwa, Sajenti Said alidai kuibiwa simu yake wiki mbili kabla ya tukio hilo na alifanya uchunguzi wake binafsi kuhusu wizi huo.
Mbele ya Jaji Elizabeth Mkwizu, watuhumiwa hao walikuwa wakikabiliwa na shitaka la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Mauaji hayo yalidaiwa kufanyika Oktoba 31, 2022 katika eneo la Kitomondo wilayani Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi wanane na vielelezo vitatu, huku washitakiwa wakijitolea ushahidi wenyewe.
Jaji Mkwizu ametoa hukumu hiyo Agosti 30, 2024 baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kupitia vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo.
Katika hukumu yake ambayo nakala yake ipo kwenye mtandao wa mahakama, Jaji Mkwizu amesema mahakama imewaachia huru baada ya kuwakuta hawana hatia na kukosekana kwa ushahidi unaoonyesha washitakiwa walihusika katika mauaji hayo.
Jaji Mkwizu amesema upande wa mashitaka haukutimiza wajibu wake wa kuthibitisha shitaka hilo bila kuacha shaka.
Upande wa mashitaka uliwakilishwa na mawakili, Violeth David na Saada Mohamed huku utetezi ukiwakilishwa na mawakili wanne wakiongozwa na Castro Shirima.
Shahidi wa kwanza, Monica Daudi (bibi wa marehemu), alieleza kuwa siku ya tukio Oktoba 13, 2022, saa nne asubuhi, alikuwa akitayarisha unga kwa ajili ya kuuza na alimwagiza mjukuu wake, Yasir kwenda kununua ngano.
Alisema Yasir alirudi na mtama badala ya ngano, Monica alimtuma arudi kuchukua ngano lakini hakurudi.
Monica alidai mahakamani hapo kuwa baadaye mvulana mwingine aitwaye Costa alifika akiwa na ngano na alipoulizwa alipo Yasir, alidai kuwa aliitwa na mwanamke mmoja.
Baada ya muda mrefu kupita bila kumuona Yasir, alipigiwa simu saa moja jioni na mama wa Yasir akimtaarifu kuwa Yasir ameuawa.
Monica alidai alikimbilia eneo la tukio Mtaa wa Kitomondo, mwendo wa dakika kama 10 na alipofika, alimkuta Yasir amelala chini bila shati na kulikuwa na wanaume wanne wakizungumza. Alidai alishirikiana na mama wa marehemu, Nadia Gerald kuripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi Chang’ombe.
Na polisi walienda mpaka eneo la tukio na waliuchukua mwili wa Yasir na kuupeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi na alizikwa siku iliyofuata.
Shahidi wa pili ambaye ni mama wa marehemu, alidai kuwa kati ya saa sita na saba mchana alipokea simu kutoka kwa rafiki yake aliyemtaja kwa jina la mama Leila akimtaarifu aende nyumbani kwa mama Aziza akamjulishe kuwa Yasir ameuawa.
Amedai alipofika eneo la tukio, aliona watu kadhaa wamekusanyika na mwili wa Yasir ulikuwa umelala karibu na geti, umezungukwa na fimbo na damu iliyoganda juu yake.
Miongoni mwa watu waliokuwepo ni mwenye nyumba, Yusuph Kabange, mtu mwingine ambaye hakumfahamu na Said, ambaye alikuwa na kisu na fimbo na alishuhudia Said akifungua kamba miguuni mwa Yasir.
Mama wa Yasir alidai kuwa babu Seif aliyekuwa ameongozana naye, alimuuliza Said chanzo cha tukio hilo, alimjibu kuwa ni simu yake iliyoibiwa wiki mbili zilizopita.
Alipoulizwa zaidi kuhusu kuripoti wizi huo, Said alikiri kuwa hakutoa taarifa Polisi na alifanya uchunguzi wake mwenyewe. Mama wa marehemu alidai Sajenti Said alimuagiza mama Aziza kuchota ndoo ya maji na kuumwagia mwili wa Yasir na baadaye waliondoka wakaenda kuripoti Polisi. Kabange na Said walifika kituo cha polisi na kukamatwa.
Shahidi wa nne, babu wa marehemu Hery Mpakanjia, alidai alipewa taarifa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili na watu wengine na aliutambua mwili wa Yasir, ambao ulikuwa na alama za fimbo na damu iliyoganda. Shahidi wa tano, Sajenti Simon, alidai kuwa siku ya tukio akiwa kituo cha Polisi, Nadia na mama yake waliripoti tukio hilo, na walipoenda eneo la tukio, aliona mwili wa Yasir ukiwa umelala chini.
Shahidi wa sita, Dk Paulo Makoye, alidai Oktoba 14, 2022, saa sita mchana, aliitwa kuufanyia uchunguzi mwili wa Yasir na akiwa na fomu ya Polisi namba 99, alibaini kuwa Yasir alikuwa amevimba kichwa upande wa kushoto na alama za michubuko mwili mzima.
Shahidi wa nane, Inspekta Tumaini Swilla, alidai Desemba 7, 2022, kati ya saa saba na nane mchana, katika Kituo cha Polisi Chang’ombe, alipewa kazi na mkuu wake, ASP Ernest Mzava, kuandika maelezo ya ushahidi kutoka kwa Mfaume Hamis kuhusu kifo cha Yasir. Alithibitisha taarifa hiyo na kueleza kuwa maelezo hayo ya shahidi huyo yalihusisha watu waliotajwa kushiriki katika tukio hilo, wakiwemo Mwanajeshi, Said, Mama Aziza, Bilal na shangazi wa Aziza.
Sajenti Said akijitetea mahakamani, alidai siku ya tukio jioni alitoka kazini na alipofika nyumbani kwake alikuta geti liko wazi na kuona watu watatu waliokuwa wakifahamiana naye, wakimuhoji kijana wa kiume ambaye alikuwa amepiga magoti.
Alidai watu hao walikuwa wakimuhoji kijana huyo aliyedaiwa kuingia ndani ya ukuta wa nyumba yake ambapo yeye alienda ndani kubadilisha nguo na kuungana na nao nje na kuendelea kumuhoji kuhusu kuingia humo ndani.
Alidai awali kijana huyo alikana kuiba chochote ila baada ya kutishiwa alikiri kuingia kwenye makazi ya watu mara nyingi na kutaja baadhi ya vitu alivyokuwa ameiba.
Alidai wakati mazungumzo yanaendelea umati wa watu ulikusanyika nje, wakisema kwa sauti kubwa kwamba walimtambua kijana huyo kama mwizi na licha ya kushauri wampeleke Polisi, ushauri huo ulipuuzwa na umati ambao ulimshambulia kijana huyo.
Alidai baada ya kushindwa kudhibiti vurugu hizo, aliambatana na Kabange kwenda Polisi kuripoti na mmoja wa maofisa wa polisi alieleza taarifa hizo zinafanana na zilizotolewa na mwanamke aliyeenda kituoni hapo.
Kufuatia hilo, Said na Kabange waliwekwa chini ya ulinzi na baadaye Kabange aliachiwa na Said alibaki kituoni hapo.
Hata hivyo, Said alisisitiza kutohusika na kifo cha Yasir ambaye alidaiwa kuingia nyumbani kwake wakati yeye hayupo na kuomba kufutiwa mashitaka.
Naye Hadija alidai siku ya tukio aliarifiwa na wakwe zake kuhusu fujo zilizotokea nyuma ya choo chake, alipokuwa anajaribu kutazama alikutana na kijana aliyekuwa akiitiwa mwizi.
Alidai wakati huo geti la nyumba yake lilikuwa wazi, hivyo umati wa watu wote uliingia ndani na kuanza kumshambulia mshitakiwa kwa fimbo licha ya Saidi kujaribu kuwazuia, lakini hakufaulu.
Alidai umati uliendelea kumpiga kijana huyo hadi akaachwa hoi chini na kuomba mahakama imuondolee hatia kwani hahusiki.
Zamda alidai saa tano usiku siku ya tukio alisikia fujo kutoka nyuma ya nyumba na alipoenda kuangalia, alimuona kijana huyo, hivyo kulazimika kumwita mkwe wake baada ya kumuona kama mwizi kulingana na kuingia kwake kwa siri.
Alidai baada ya kujaribu kumuhoji kijana huyo ambaye alishindwa kutoa majibu yanayoeleweka, watu wengine waliendelea kumuhoji na wakiwa hapo kundi la watu liliingia ndani ya eneo hilo na kuanza kumpiga kijana huyo aliyedaiwa kuwa mwizi na kukana kuhusika na kifo hicho.
Jaji Mkwizu, alianza kwa kueleza kuwa ni kanuni iliyoimarishwa na sheria kuwa upande wa mashitaka una wajibu wa kuthibitisha mashitaka ya jinai bila kuacha shaka yoyote kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 3 (2) cha Sheria ya Ushahidi.
Kuhusu iwapo washitakiwa hao waliofikishwa mahakamani walihusika na mauaji ya Yasri, alisema maelezo ya mashitaka yanategemea kwa kiasi kikubwa ushahidi wa moja kwa moja uliotolewa mahakamani na maelezo ya Mfaume (kielelezo cha tatu) na ushahidi wa kimazingira.
Jaji Mkwizu alisema hakuna mashaka kwamba washitakiwa walipatikana kwenye eneo la tukio kwa wakati, lakini uwepo wao unamaanisha wao ndiyo wauaji? Alihoji.
Huku akinukuu mashauri yaliyotolewa uamuzi na Mahakama ya Rufani, Jaji Mkwizu amesema mara kwa mara, hutokea mkanganyiko kati ya kuwepo kwenye eneo la uhalifu na kushiriki katika kutenda kosa, na kuwa imesisitizwa kuwepo eneo la tukio hakufanyi mtu kuwa muhusika wa kosa.
“Ushahidi zaidi ulihitajika kuwaunganisha na mauaji haya. Upande wa utetezi umewasilisha maelezo na kutoa mwanga kuhusu mazingira ya marehemu kuingia nyumbani kwao, ila upande wa mashitaka hadi sasa haujaweza kutoa ushahidi madhubuti unaowahusisha washitakiwa na tukio linalodaiwa.”
Jaji Mkwizu amesema kutokana na kukosekana kwa ushahidi unaoonyesha kuhusika kwa washitakiwa katika mauaji hayo, hivyo upande wa mashitaka haujatimiza wajibu wake wa kuthibitisha kosa hilo.
“Wanaachiwa huru kwa kosa la mauaji chini ya masharti ya kifungu cha 235 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai,” alihitimisha Jaji.