Wazazi wanaofanya watoto wao vitega uchumi kikaangoni

Mbeya. Halmashauri ya Jiji la Mbeya imesema itachukua hatua kali kwa mzazi au mlezi yeyote atakayeharibu ndoto za mtoto wake katika elimu kwa kumtumia kama chanzo cha mapato kwa njia ya kumuozesha au kumfanyisha kazi kinyume na sheria.

Kauli hiyo imetolewa ikiwa zimebaki siku chache kwa wanafunzi wa darasa la saba kuhitimu elimu ya msingi nchini. Watafanya mitihani yao ya Taifa, Septamba 12, mwaka huu.

Akizungumza leo Jumapili Agosti 31, 2024 kwenye mahafali ya shule saba za msingi jijini humo yaliyoandaliwa na kampuni ya Mc Luvanda Branding & Entertainment, kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Davis Mbembela amesema wazazi na walezi watakaokatisha ndoto za mtoto watachukuliwa hatua.

Amesema kuna tabia ya baadhi ya wazazi wanaosubiri mtoto hasa wa kike, ahitimu elimu ya msingi amuozeshe au kumtumikisha kwa shughuli mbalimbali kinyume na sheria, hivyo yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali.

“Serikali inatumia nguvu na gharama kubwa kuboresha miundombinu ya elimu, tunaboresha madarasa, madawati na kuajiri walimu, hatutasita kuchukua hatua kwa mzazi au mlezi atakayekatiza ndoto za mtoto kielimu,” amesema Mbembela na kuongeza;

“Leo tunasherekea miaka saba ya watoto kuhitimu elimu ya msingi, kila mmoja ana ndoto zake, hivyo haitakuwa busara kuona mzazi au mlezi anaharibu maisha ya mwanafunzi. Tukisikia ameozeshwa au kutumikishwa, Serikali itachukua hatua.”

Pamoja na hayo, amewataka wanafunzi hao kujiandaa vyema kiakili kufanya mitihani huo, ili wafaulu na kufikia malengo yao kielimu.

Pia amewataka wazazi na walezi kuhakikisha nao wanatimiza wajibu wao kugharamia mahitaji yote na Jiji la Mbeya linatarajia kuona ongezeko la ufaulu katika mitihani hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa shule hizo, Steven Mbowe wa shule ya msingi Airport, amesema wamejiandaa vema na watahakikisha wanazingatia waliyofundishwa na walimu wao, ili wafaulu.

“Tumekuwa na ushirikiano katika mambo mbalimbali kati ya wanafunzi na walimu, tumezingatia walichotufundisha na matarajio yetu ni kufaulu na kutimiza ndoto zetu kielimu” amesema Mbowe.

Kwa upande wake, mwandaaji wa sherehe hiyo, Edwine Luvanda ‘Mc Luvanda’, amesema lengo ni kuwakutanisha wanafunzi wa shule zote za jiji hilo kubadilishana mawazo na kupanua uelewa.

Amesema ikiwa ni mara ya pili kufanyika kwa sherehe hiyo kwa kushirikisha shule saba, mwakani wanatarajia kukutanisha shule zote za Jiji hilo, ili kupanua wigo kwa walimu, wanafunzi, wazazi na walezi kusherekea tukio hilo.

“Tunapowakutanisha wanafunzi na walimu wa shule zote wanabadilishana mawazo, sawa na wanafunzi ambao baadaye watakutana katika ngazi ya sekondari na kutengeneza umoja kwa faida yao” amesema Luvanda.

Mwalimu Jane Ntale, amesema sherehe ya kukutanisha wanafunzi wa shule zote na walimu wake inasaidia kuongeza uhusiano na kupanua mawazo katika majukumu yao ya kila siku.

“Tunashukuru waandaaji Luvanda brand and Etertainment kwa kutuweka karibu, tunahitaji kubadilishana mawazo na kutengeneza uhusiano baina yetu na wanafunzi” amesema Jesca.

Mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao, Matrida Nechemia amesema wazazi au walezi wanaosubiri kuozesha au kutumikisha watoto wanaomaliza elimu ya msingi, ni kuwanyima haki kielimu na kwamba Serikali ichukue hatua.

“Naungana na Serikali katika hili, tunatumia gharama kubwa kuwasomesha watoto, inakuaje badala ya mtoto kuhitimu asiendelee hata na kozi ya ufundi kwa maisha yake? Aende kuoa, kuolewa na kutumikishwa?”  amehoji Matrida.

Related Posts