Yonta, Adebayor kazi imeanza Singida BS

NYOTA wawili wapya wa Singida Black Stars washambuliaji Abdoulaye Yonta Camara na Victorien Adebayor, wamepewa programu maalumu za mazoezi na kocha mkuu wa kikosi hicho, Patrick Aussems kutokana na kuchelewa kujiunga na wenzao msimu huu.

Camara na Adebayor hawakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichoanza maandalizi ya msimu (pre season), jambo ambalo limemfanya Aussems kuwapa programu maalumu za mazoezi ili Ligi Kuu Bara itakaporejea wawe fiti kwa ajili ya ushindani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Aussems alisema kwa Camara kuna maendeleo mazuri kwa sababu alipata mechi ya kirafiki na Mtibwa Sugar ya kiushindani, hivyo maendeleo yake sio mabaya sana, japo anahitaji kuzoeana na wenzake kwanza kikosini.

“Adebayor anahitaji muda zaidi kwa sababu alichelewa zaidi kujiunga na wenzake kutokana na changamoto ambazo alikuwa nazo. Sina shaka naye kwa sababu ni mchezaji mzoefu, hivyo hadi ligi itakaporejea atakuwa amekopi kwa asilimia kubwa,” alisema.

Aussems aliongeza kabla ya kujumuika na wenzao wamekuwa na programu maalumu za kutengeneza ufiti hivyo hana haraka ya kuwatumia hivi karibuni kwa sababu anahitaji wawe fiti kwa asilimia 100 kimwili, kiafya na kiakili.

Camara amejiunga na msimu huu baada ya kuachana na Milo FC ya Guinea, ambapo msimu uliopita alikuwa mfungaji bora baada ya kufunga mabao 21, huku akichezea timu kadhaa zikiwemo AS Ashanti Golden Boys na Wakriya AC.

Nyota huyo ameongeza makali katika eneo la ushambuliaji ambalo linaongozwa na washambuliaji wengine wakiwemo Mtanzania Habib Kyombo, Mkenya Elvis Rupia na nyota mpya Joseph Guede ambaye ni raia wa Ivory Coast aliyetokea Yanga.

Adebayor ambaye mara kadhaa alihusishwa kujiunga na Simba, amejiunga na kikosi hicho baada ya kuachana na AmaZulu FC ya Afrika Kusini.

Related Posts