Zanzibar rasmi utalii wa mikutano, mataifa 12 kushiriki kongamano la maadili

Unguja. Wakati Zanzibar ikitafuta nyanja mbalimbali za kuhamasisha na kutangaza utalii wake, linatarajiwa kufanyika kongamano kubwa la kimataifa linalohusiana na utalii wa maadili na mikutano.

Katika kongamano hilo la kwanza liitwalo (Light upon Light) mataifa zaidi ya 12 yanatarajia kushiriki ambapo litawaleta pamoja masheikh maarufu akiwemo Mufti maarufu duniani, Ismail Menki.

Akizungumza wakati wa kuzindua shamrashamra za kueleka katika kongamano hilo litakalofanyika Oktoba 12 na 13, 2024 Kisiwani Zanzibar jana Jumamosi, Agosti 31, 2024 Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga alisema Serikali inatafuta nyanja mbalimbali za kuhamasisha na kutangaza utalii.

Alisema wanatafuta mwenendo wa wazi kutafuta mbinu mbalimbali za kukuza utalii badala ya kutegemea wa aina moja.

“Tungeweza kujifungia kwa kutumia mkakati mmoja lakini kwa namna sekta hiyo inatumia wigo mpana ukisema unajifungia katika utalii wa aina fulani peke yake unaweza ukakosa fursa kubwa sana,” alisema 

Alisema licha ya utalii huo kufungamanishwa na kidini lakini ni wenye tija na unajumuisha masuala ya maadili na familia, huku akitaja nchi za Uturuki, Saudia, Oman na nyingine ambazo zimeanza utalii wa aina hiyo na kuleta matokeo chanya, hivyo Zanzibar ina kila sababu kuanzisha utalii huo kinachotakiwa ni kuelimisha na kuhamasisha wengi. 

Alisema watu wanaoshiriki katika utalii wa namna hiyo wana fedha nyingi hivyo Zanzibar ina fursa ya kufanya jambo hilo kwani mwamko umekuwa mkubwa,“tukiwekeza miundombinu ya kufanya utalii wa namna hii wigo utapanuka.”

Awali, Mwenyekiti wa Light upon Light, Nadir Mahfoudh alisema kongamano hilo litakuwa na kazi ya kuwaleta watu pamoja na masheikh wakubwa duniani na kuitangaza Zanzibar kimataifa.

“Baada ya kuelewa dhamira ya Serikali yetu ya kuendeleza utalii na maadili ndipo tumekuja kuratibu kongamano hili la kimataifa,” alisema.

Alisema katika jambo hilo yatafanyika matukio mawili, ambapo litafanyika kongamano la wazi kwa watu wote katika uwanja wa Amaan Complex Agosti 12 na 13 kutakuwa na chakula cha usiku.

Zaidi ya nchi 12 ikiwemo Falme za Kiarabu, Afrika Kusini, Kenya, Uingereza, Oman, Finland na Marekani zimeshathibitisha ushiriki wake. 

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Mufti Zanzibar, Khalid Ali Mfaume amesema ujio wa Sheikh Menk ni heshima na atafungua milango katika utalii na uchumi wa Zanzibar.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria utumishi na utawala Bora, Haroun Ali Suleiman aliwataka watu kujitokeza kwa wingi katika kongamano hilo. “Hili ni jambo muhimu kwa nchi yetu kuna tabia ya watu kutothamini vya kwao lakini huu ndio muda wa kuona vya kwetu na kuvitangaza.”

Related Posts