Dart, Udart zapewa siku 90 mabasi mwendokasi Mbezi, Mbagala yapatikane

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa amezitaka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) na Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) kuhakikisha ifikapo Desemba 2024, mabasi ya mwendokasi yanayotakiwa katika barabara ya Morogoro na ya Mbagala yawe yamepatikana.

Mchengerwa ametoa maagizo hayo leo Jumatatu Septemba 2, 2024, alipozindua mageti janja na kadi janja kwa ajili ya usafiri wa mabasi ya mwendokasi, jijini Dar es Salaam.

Katika kufanikisha hilo, Mchengerwa amesema hakuna haja ya kuwasubiri wawekezaji kutoka nje ya nchi kwa kuwa wapo Watanzania wengi wanaweza na kutaka wapewe nafasi, wakiwemo wamiliki wa mabasi ya mikoani.

“Watanzania wamesubiri kwa muda mrefu kupatikana kwa mabasi hayo na sasa inatosha, hatutaki tena kusikia changamoto hii wizarani,” amesema.

Katika kusisitiza hilo, Mchengerwa amesema:”Pia lile suala linaloitwa mchakato kila siku kuhusu utekelezaji wa suala hilo kati ya wakala wa mabasi na kampuni ya uendeshji mradi huu, nisisikie.

“Taarifa nilizonazo ni kwamba barabara ya Morogoro inahitaji mabasi 170 huku ile ya Mbagala ikihitaji mabasi 500, hivyo nataka yapatikane kabla ya Desemba mwaka huu, nina hakika tuna Watanzania wanaliweza hilo, washirikisheni wakiwemo wamiliki wa mabasi.” Kuanzia leo hadi Desemba mosi, 2024 ni sawa na siku 90.

Amesema kama mmiliki wa kampuni moja ya mabasi anamiliki magari zaidi ya 200, haoni kama watashindwa kuwa na mabasi hayo na kutaka wapewe nafasi badala ya kuwawaza wawekezaji kutoka nje ambao kwa kiasi kikubwa wanachangia kuchelewesha kupatikana kwa mabasi hayo.

Kuhusu mageti na kadi janja, amesema zinakwenda kurahisisha huduma ya usafiri huo kwa kuepuka kutumia kadi za makaratasi ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia uharibifu wa mazingira.

Hata hivyo, amesema angependa kuona kadi hizo zinaanza kutumika kuanzia leo baada ya uzinduzi na kuachana na matumizi ya tiketi za karatasi.

Awali akitoa taarifa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Athuman Kihamia amesema uzinduzi wa kadi hizo ni kuhamia mfumo wa kukusanya nauli kwa kutumia kadi janja ambao umetengenezwa na Dart.

Amezitaja faida mbali na kuondokana na matumizi ya karatasi, itasaidia kuondokana tatizo la upatikanaji chenji na zitaenda sambamba na mfumo wa uongozaji mabasi (ITS) na zitatumika katika miradi ya awamu zote sita.

Naye Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge Tamisemi, Justine Nyemoga amewapongeza Dart kwa hatua ya kuja na kadi na kueleza ni moja ya maagizo ya Bunge iliyowahi kuyatoa kutumiwa kwa kadi janja ambazo zitasaidia si tu kukabiliana na changamoto ya chenji, lakini pia kupunguza kero ya foleni katika kukata tiketi za karatasi dirishani.

“Pamoja na pongezi zetu hizo, mnapaswa  kujua kero nyingine kubwa kwa sasa ni upugufu wa mabasi ambayo tunajua waziri unaendelea kulifanyia kazi hilo, lakini wito wetu kupatikana kwa kadi janja hizi na mageti ya kisasa kuende sambamba na upatikanaji wa mabasi hayo, ili kuwaondolea wananchi kero ya usafiri huo,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkoa wa Dar es Salaam, Katibu Tawala wa Mkoa, Thobias Nguvil, amesema anaishukuru Serikali kwa namna inavyoendelea na ujenzi miundombinu ya mabasi hayo katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo na kueleza siku zijazo kero ya usafiri katika jiji hilo itakuwa historia.

Walichosema Taboa, Darcoboa

Wakati Waziri Mchengerwa akitoa kauli hiyo, wamiliki wa mabasi kupitia msemaji wao, Mustapha Mwalongo amesema ni jambo zuri na kueleza kilichokwamisha wao kutoshiriki katika mradi huo tangu awali ni kuwepo kwa masharti magumu yanayofanana na wawekezaji wa nje.

“Tuna imani na Waziri Mchengerwa, kwani akisema jambo huwa analisimamia lifanyike, na katika hili nina imani vile vigezo vikubwa vilivyowekwa ili tuombe mradi vitalegezwa kama si kuondolewa kabisa,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa wamiliki wa Daladala mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwaya Lema amesema baada ya kuelezwa mradi wa Mbagala mwekezaji amepatikana walikata tamaa kuwa wao wamewekwa pembeni, licha ya kuwahi kufanya mkutano na Dart na Udart kuomba kuendesha mradi wa njia hiyo.

“Kauli hii ya waziri inatupa moyo, labda maoni yetu tuliyoyatoa katika kikao tulichokifanya mwanzoni mwa mwaka huu na mamlaka zinazosimamia mradi huo kuwaomba watupe barabara ya Mbagala huenda yakafanyiwa kazi na tunaomba atenge siku akutane nasi tumueleze ya kwetu katika ushiriki wa kuondesha mradi huu,” amesema na kuongeza:

“Ni muda umepita sasa tangu tulivyokutana nao mpaka leo hawajatupa mrejesho zaidi ya kusikia za chinichini kuwa mwekezaji kutoka nje kashapatikana na ataanza kazi Novemba 2024.”

Hassan Mushi, mkazi wa Kibamba amesema kadi hizo zimekuja wakati muafaka, kwani ameshaacha chenji zao mara nyingi hasa wanapokuwa na wanafunzi.

Levina Mlokozi, mkazi wa Ubungo Saranga, amesema kutumika kwa kadi ni jambo zuri, huku akiomba upatikanaji wake uwe rahisi kwa wakati wote kwa kuwa kwa kufanya hivyo tija itaonekana.

Pia amesisitiza kuongezwa kwa mabasi kwa kuwa yaliyopo yanasababisha wakae kituoni muda mrefu.

Mradi huo wa mabasi yaendayo haraka ulianza kufanya kazi mwaka 2016. Barabara ya Morogoro ilitakiwa iwe na mabasi 305, lakini yaliyoletwa yalikuwa 210 na mpaka sasa mabasi mazima yanayofanya kazi hayazidi 100 baada ya mengine kuharibika.

Related Posts