Arusha. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema ni muhimu kuwa na usawa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, huku akieleza Tanzania imeendelea kusisitiza ujumuishaji wa masuala ya jinsia na mabadiliko kupitia sera, programu na mikakati kwenye ngazi zote.
Dk Mpango amesema hayo leo Jumatatu, Septemba 2, 2024 jijini Arusha, alipofungua Jukwaa la 24 na mkutano wa 35 wa kamati ya kudumu ya fedha ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (UNFCCC).
Amesema ni muhimu kufanywa jitihada za haraka za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo athari zake zimejitokeza katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na usalama wa chakula, afya na ikolojia huku wanawake, vijana na watoto wakiathirika zaidi.
Dk Mpango amesema dunia inasubiri ripoti za tathmini na muktasari wa fedha za masuala ya hali ya hewa, ripoti ya maendeleo kuhusu Dola bilioni 100 za Marekani ili kufanikisha utekelezaji wa mkataba wa Paris kutoka kwa nchi zinazoendelea kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema Tanzania inaendelea kukuza ujumuishaji wa kijinsia na mabadiliko ya tabianchi katika sera, programu na mikakati katika ngazi zote pamoja na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu.
“Mabadiliko ya tabianchi athari zake kubwa ni kwenye mifumo ya ikolojia, usalama wa chakula na mifumo ya afya, kijamii ikiwemo usawa wa kijinsia. Mabadiliko ya tabia nchi na ukosefu wa usawa wa kijinsia ni masuala yanayohusiana,” amesema.
Dk Mpango amesema vitu muhimu vinavyoendelezwa ni pamoja na usawa wa kijinsia katika upatikanaji wa fursa za kiuchumi kwa wanawake na wanaume, kuunda mazingira ya kuruhusu wanawake kushiriki kikamilifu katika ngazi za uamuzi.
Nyingine ni usawa wa kijinsia katika upatikanaji wa elimu, matumizi ya teknolojia katika uwezeshaji wa wanawake, matumizi ya nishati safi ya kupikia katika maeneo ya mijini na vijijini.
“Kaulimbiu ya jukwaa hili inaonyesha fedha zinazozingatia usawa wa kijinsia hazitafikiwa bila mchakato wa uamuzi unaojumuisha, unaoendana na mahitaji na unaoshirikisha,” amefafanua.
Akitolea mfano hapa nchini, Dk Mpango amesema athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi zilizoathiri maeneo mbalimbali nchini ni pamoja na mafuriko, ukame, kuenea kwa majani vamizi na maporomoko ya udongo.
Amesema Desemba 2023 kutokana na mvua kubwa ilisababisha maporomoko ya tope, miti na mawe wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara na kusababisha vifo vya watu 89, majeruhi 139 na watu zaidi ya 1,500 kuathirika na tukio hilo.
Kuhusu nishati mbadala, amesema Tanzania imechukua hatua madhubuti kuongeza uzalishaji wa nishati mbadala kutoka vyanzo vinavyotumika sasa, ikiwemo umeme wa maji na kuwa imepanga kuzalisha megawati 950 kutoka nishati ya jua, upepo na mbadala mwingine.
“Tanzania imeweka lengo la kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya mijini na vijijini kutoka asilimia 86 na 67.7 mwaka 2020 hadi asilimia 100 ifikapo mwaka 2030,” amesema.
Kuhusu uchafuzi wa hewa unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa, amesema Tanzania imeipa kipaumbele ajenda ya nishati safi ya kupikia na wanashirikiana na wadau wa maendeleo.
“Lengo letu ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanapika kwa kutumia nishati safi kutoka asilimia saba ya sasa,” amesema.
Kwa upande wake, mshauri mwandamizi wa mabadiliko ya tabia nchi katika Kamisheni za Umoja wa Ulaya (EU), Apollonia Miola amesema mkutano huo unaongozwa na kaulimbiu isemayo; ‘kuongeza kasi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kupitia ufadhili unaozingatia jinsia’ na umekutanisha washiriki kutoka nchi 80 duniani.
Amesema lengo la Kamati ya Kudumu ya Fedha (SCF) ni kuangalia masuala yanayohusiana na mifumo ya kifedha na fedha za masuala ya hali ya hewa, ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), Dk Ashatu Kijaji amesema mvua za el nino ziliharibu shughuli za kijamii, kiuchumi na kusababisha vifo, huku kimbunga Hidaya kikiharibu nyumba, mbiundombinu katika baadhi ya maeneo.
“Tanzania imejizatiti kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia mipango mbalimbali, tumepitisha sera na mipango mikakati, ikiwemo Sera ya Mazingira ya Taifa ya mwaka 2021, mpango wa kitaifa wa mazingira wa muda mrefu wa mikataba ya mkakati (2022-2032),” amesema.
Dk Ashatu amesema Tanzania inashirikiana na wadau wa maendeleo katika maeneo manane, ikiwemo kukuza teknolojia za kupikia safi na nishati safi, kutekeleza mbinu za usimamizi wa taka endelevu katika miji mikubwa na kudhibiti aina za mimea vamizi katika mfumo ikolojia wa Serengeti-Ngorongoro.
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, amesema katika vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ajenda ya mabadiliko ya mabadiliko ya tabia nchi wameipa kipaumbele sambamba na masuala ya jinsia.
“Tutahakikisha masuala haya yanapewa kipaumbele na tuna uhakika kuwa hili litatuwezesha kuhakikisha kuwa rasilimali zote zitakazokusanywa zitatumika kwa uangalifu ili kufikia malengo,” amesema.