Dar es Salaam. Umoja wa Ulaya (EU), imeishutumu China kwa hatua ilizozichukua za kuitaka Ufilipino iondoe meli yake katika eneo linalogombaniwa na mataifa hayo.
Hatua za China dhidi ya Ufilipino, zinakuja ikiwa ni wiki kadhaa zimepita tangu meli za nchi hizo zigongane katika Bahari ya Kusini ya China na kusababisha meli ya Ufilipino kuharibika.
Kutokana na ajali hiyo, China ilisisitiza meli hizo kugongana ilikuwa na makusudi na kwamba Ufilipino ndio inahusika.
Hata hivyo, wakati China na Ufilipino zikiendelea kuvutana, Msemaji wa Mambo ya Nje wa EU, Nabila Massrali ameishutumu China kwa kuchukua hatua dhidi ya Ufilipino.
Kauli ya Massrali inajibu kilichozungumzwa awali na msemaji wa walinzi wa pwani wa China, Liu Dejun aliyeitaka Serikali ya Manila kuondoka haraka katika eneo hilo, vinginevyo China itaichukulia hatua.
Kutokana na kauli hiyo, Massrali amesema EU inalaani kitendo cha hatari cha meli za walinzi wa pwani wa China dhidi ya operesheni halali ya baharini ya Ufilipino katika eneo hilo la Sabina Shoal.
Beijing inadai kumiliki eneo lote muhimu la kiuchumi la bahari, licha ya madai ya ushindani kutoka kwa nchi nyingine na uamuzi wa mahakama ya kimataifa kueleza madai yake hayana msingi kisheria.
Ikumbukwe, hilo ni tukio la kwanza katika miongo kadhaa kwa nchi hizo mbili kugombania eneo hilo la Sabina shoal.