Fadlu hataki utani, ampa kazi nzito Ateba

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema licha ya mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Leonel Ateba kufunga bao moja katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Al Hilal ya Sudan, bado anapaswa kuendelea kupambana zaidi kikosini.

Nyota huyo raia wa Cameroon alifunga bao hilo ikiwa ni mchezo wa kwanza kwake akiwa na kikosi hicho tangu ajiunge msimu huu na kuifanya Simba itoke sare ya 1-1 katika mechi kali na ya kusisimua iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Fadlu alisema ni jambo zuri kwake kufunga kwani mshambuliaji yeyote hujisikia furaha anapofunga, ingawa bado ana kazi kubwa ya kufanya ili kuendana na ushindani uliopo ndani ya timu hiyo inayosaka heshima baada ya kuchemsha misimu mitatu mfululizo.

“Sio suala la mchezaji mmoja kwa sababu leo (juzi) tumeona wachezaji wengi ambao hawajapata nafasi ya kucheza tangu msimu umeanza wakicheza, kwetu kama benchi la ufundi inatupa wigo mpana wa machaguo kutokana na mpinzani wetu,” alisema Fadlu, raia wa Afrika Kusini.

Fadlu aliongeza, Al Hilal ni kipimo kizuri kwao wakati huu wanajiandaa na mchezo wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya, Simba ikianzia ugenini Septemba 13 na kurudiana Dar es Salaam Septemba 20.

“Tunahitaji mchezo zaidi ya huu kwa ajili ya kuendelea kujiimarisha, viongozi wetu wako katika hatua ya kutafuta timu nyingine tutakayocheza nayo Jumamosi hii ya Septemba 7, ambayo tunaamini pia itakuwa ni kipimo kingine kizuri kwetu.”

Ateba amejiunga na timu hiyo msimu huu baada ya kuachana na USM Alger ya Algeria aliyojiunga nayo Januari mwaka huu akitokea Dynamo Douala FC ya kwao Cameroon huku akizichezea klabu mbalimbali zikiwemo za Coton Sport na PWD Bamenda.

Nyota huyo ameichezea USM Alger jumla ya michezo 23, ya mashindano mbalimbali ambapo alifunga mabao matatu na kuchangia (asisti) saba, huku akikumbukwa zaidi mwaka 2023, alipoibuka mfungaji bora wa Ligi ya Cameroon baada ya kufunga mabao 21.

Uwepo wake unaongeza makali katika safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Mganda, Dese Mukwala ambaye pia ameanza kufungua ukurasa wa mabao na kikosi hicho baada ya kutupia kwenye ushindi wa timu hiyo wa 4-0, dhidi ya Tabora United Agosti 25.

Wakati Simba ikiwa katika maandalizi ya mchezo wa pili Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli, habari njema kwa mashabiki wa timu hiyo ni kurejea kwa kipa namba moja wa kikosi hicho, Aishi Manula.

Manula alianza katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Al Hilal ikiwa ni mechi yake ya kwanza msimu huu na kikosi hicho baada ya sintofahamu ya muda mrefu juu ya hatima yake, iliyomfanya kuhusishwa kuondoka ndani ya timu hiyo na kurejea Azam FC.

Manula ambaye amekuwa kipa namba moja wa Simba kwa muda mrefu, amekuwa na wakati mgumu ndani ya kikosi hicho hasa baada ya kuandamwa na majeraha yaliyomfanya kuwekwa benchi na Mmorocco, Ayoub Lakred na hata sasa kipa mwenzake mpya, Moussa Camara.

Katika mchezo huo alicheza kwa dakika 45 bila kuruhusu bao na alitoka Simba ikiongoza bao 1-0 na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Abel aliyewaruhusu Wasudan kusawazisha katika dakika ya 76.

Nyota mwingine ni winga, Joshua Mutale aliyerejea kikosini baada ya kuandamwa na majeraha ya nyama za paja aliyoyapata katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tabora United, uliopigwa Agosti 18 na Simba kushinda mabao 3-0.

Mwingine aliyerejea ni beki wa kati, Chamou Karaboue aliyepata majeraha Agosti 8, katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii ambao timu hiyo ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0, dhidi ya watani wao Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kurejea kwake ni faida pia kwa kocha Fadlu kwani eneo la beki wa kati linazidi kuongezeka ushindani baada ya kuwatumia Abdulrazack Mohamed Hamza na Che Malone Fondoh ambao kwa pamoja wametengeneza ukuta mgumu katika michuano mbalimbali.

Related Posts