Familia yagomea Polisi kufukua mwili bila kibali

Moshi. Polisi wameshindwa kufukua mwili unaodaiwa kuzikwa kimakosa katika kitongoji cha Dungi, Kijiji cha Kibosho Kindi, Wilaya ya Moshi, baada ya ndugu kudai hawana taarifa hiyo na kutaka waonyeshwe kibali cha kuwaruhusu kufanya hivyo.

Mwili huo unaodaiwa kuwa wa Richard Shoo, aliyefariki dunia Juni 19, 2024 ulitakiwa kufukuliwa kwa ajili ya uchunguzi na vipimo vya vinasaba (DNA), baada ya familia moja kuibuka na kudai mwili huo uliozikwa  si wa marehemu Shoo bali  wa kijana wao.

Baada ya sintofahamu hiyo, inadaiwa Mahakama iliamuru mwili huo ukafukuliwe, ili kufanyika kwa vipimo na taratibu nyingine za kisheria zifuate.

Hata hivyo, Polisi jana Jumapili Septemba Mosi, 2024 wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Moshi wakiambatana na madaktari wawili, walifika kwa ajili ya kufukua mwili huo, lakini ilishindikana baada ya familia kudai kutoshirikishwa na kutaka kuonyeshwa kibali cha kufukua mwili huo na polisi hawakuwa nacho.

Polisi walilazimika kuomba kutumiwa kibali hicho kwa simu ambacho walieleza walikiacha ofisini, lakini familia hiyo ilikataa na kudai wanahitaji kukiona, hali iliyosababisha kuahirishwa shughuli hiyo.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema kazi ya kufukua mwili huo lilishindikana baada ya upande mmoja kutoridhia na baadhi ya wanafamilia kudai kutoshirikishwa suala hilo.

“Wale ndugu walidai hawakushirikishwa, wamedai si ndugu wote walishirikishwa, kuna baadhi hawakuhusishwa hivyo hawakuridhika na uamuzi huo.”

“Maazimio ni kwamba waende mahakamani na Mahakama itatoa uamuzi ni nini kifanyike, hivyo kwa mazingira hayo imeishia hapo warudi mahakamani Mahakama waamue,”amesema Kamanda Maigwa.

Baba mdogo wa marehemu, Jubilati Shoo amesema  wamezuia kufukuliwa kwa mwili huo kwa sababu hawakuwa na taarifa na Polisi hawa kwenda na kibali.

“Walivyokuja tulitaka kuwaruhusu, nikaona kwamba sio halali, kimsingi watupe kibali tusaini ili tuwaruhusu wauchukue, lakini tukaona hapana hawajaja nacho tukawaambia basi tuanzie taratibu hizi Polisi ndio tuweze kuja kufukua mwili wa marehemu wetu”

“Wanalalamika kuwa mwili huu sio wa Shoo ni wa upande mwingine ambao sijui ukoo wao, sababu ya kuzuia ni kukosa kibali na kuja siku ambayo sio na kutuvamia tukiwa hatuna taarifa, hivyo tumekubaliana tukutane Polisi  ili tupate muafaka wa pande zote mbili kwa sababu sisi hatujakataa mwili usichukuliwe ila tulihitaji kuona kibali na walikuja kwa muda ambao siyo muafaka,”amesema.

Ameongeza kuwa “Kwa niaba ya wananchi waliokuwa pale wakaomba kibali, wakasema kwamba haitawezekana labda mkajiandae tena na sisi kiserikali tufike pale tushuhudie pande zote mbili tupate haki yetu.”

Akielezea mazingira ya kifo cha kijana huyo, amesema alifariki akiwa kwenye shughuli zake mjini Moshi na walipopata taarifa walifuatilia polisi na kufanya taratibu zote walizoelekezwa ndipo kukabidhiwa mwili.

“Tukafuatilia tukaambiwa tupeleke picha, vyeti vya ubatizo na taratibu zote za uongozi wa kijiji tukapeleka, wakatupa vibali na sehemu za kulipia nyingi na ndani ya siku saba tukafanikiwa kuchukua mwili wa marehemu.”

“Tumemaliza ndani ya wiki tatu, nne, tunaitwa Polisi tunaambiwa jamani ule mwili sio wa kwenu, tukawaambia si tulipata vibali toka kwenu, mpaka Mawenzi (Hospitali ya Mawenzi) mpaka Polisi tukachukua mwili wetu tukaja kuzika, leo wanasema mwili sio wa kwetu,”amesema.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Dungi, Kijiji cha Kibosho Kindi, Obedi Lema amesema alipigiwa simu na polisi  Septemba mosi  akijulishwa kutakuwa na shughuli ya kufukua mwili kwenye kitongoji chake.

Amesema pamoja na polisi kufika kwa ajili ya kufukua mwili huo, shughuli hiyo ilishindikana baada ya wahusika kudai hawana taarifa na polisi hawakuwa na kibali.

“Walihitaji kuonyeshwa kibali cha Mahakama ili wao wajiridhishe ni kweli walikuwa wanafukua kihalali ila hakikuwepo hivyo ikawa ndio sababu ya kwanza, lakini jambo lingine  hawa wana mila na desturi zao za kufukua makaburi, wana mambo yao hawawezi kuacha kaburi wazi, kwa hiyo walihitaji muda wa kujiandaa ili wasiache kaburi lao wazi,”amesema Lema.

Related Posts