Dar es Salaam. Ukitazama mwonekano wake unaweza kudhani ni nyumba lakini ni jokofu la mkaa (friji) maalumu kwa kuhifadhi mazao yanayoharibika mapema.
Ni friji lililotengenezwa kwa kutumia mkaa na maalumu kwa ajili ya kutunza mazao yanayoharika haraka yanapotolewa shambani ili kuwaepusha wakulima wasipate hasara baada ya mavuno.
Friji hilo hutumika katika kuhifadhi mazao ya mbogamboga na matunda ambayo hulimwa na wakulima lakini wakati mwingine hujikuta katika hasara ya kuharibikiwa na mazao yao kutokana na kukosana kwa miundombinu rafiki ya uhifadhi.
Hiyo ni kutokana na mazao hayo kukosa uwezo wa kustahamili joto au kukaa kwa muda mrefu bila kuhifadhiwa katika maeneo rafiki ili yasinyauke au kuharibika.
Kwa mujibu wa Mhandisi wa Kilimo, Usharika wa Wahitimu Wajasiriamali wa Chuo Kikuu cha Sokoine (Sugeco), Morice Kastoly mazao yanapowekwa katika friji hilo hutumia wiki moja na zaidi bila kuharibika.
“Sisi hapa tulijenga kwa ajili ya kuhifadhia viazi lishe kwa waliokuwa wakilima na wanaotumia katika shughuli zao za kila siku lakini sasa yupo mtu anatumia eneo hili kwa ajili ya shughuli zake za kilimo cha uyoga,” amesema Kastoly.
Akielezea namna lilivyojengwa, Kastoly amesema ukuta wake hugawanywa katika maeneo tofauti na kupitishwa mabomba ya maji ambayo pindi joto linapozidi yanafunguliwa ili kuloanisha mkaa.
“Mkaa ukishaloana hufyonza joto ambalo huwa ndani na kutengeneza hali ya ubaridi ambayo huwa ni rafiki kwa ajili ya mazao yanayowekwa, mazao katika friji hili yanaweza kukaa hata wiki bila kuharibika ila viazi lishe vinaweza kukaa zaidi ya muda huu,” amesema Kastoly.
Pia, amesema friji kama hilo linaweza kuwa mkombozi katika maeneo mbalimbali nchini wanayolima mazao yanayoharibika haraka kama pilipili hoho, nyanya, vitunguu.
Wakati wakisubiri wateja wakulima wanaweza kuhifadhi mazao yao katika eneo hilo jambo linalowafanya kuwa na uhakika wa kile wanachokifanya.
Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa, kuharibika kwa mazao baada ya kuvunwa ni moja ya changamoto ambayo huwakumba wakulima wadogo na kuathiri uchumi wao
Inakadiriwa kuwa asilimia 30 hadi 40 ya kiasi cha nafaka kinachozalishwa nchini kila mwaka, hupotea bila kutumiwa na walaji.
Hata hivyo, upotevu huu ni mkubwa zaidi kwa mazao yanayoharibika haraka kama ya mizizi, mbogamboga na matunda.
Kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mazao Baada Ya Kuvuna wa mwaka 2019 hadi 2029 upotevu huo wa mazao hutokana na teknolojia duni za kuyahifadhi, ufahamu mdogo wa wadau juu ya ukubwa wa tatizo na athari zake pamoja na miundombinu duni ya usafirishaji wa mazao.
Sababu nyingine ni teknolojia duni za uvunaji na ukaushaji wa mazao, masoko yasiyo ya uhakika, ukosefu wa vifungashio na huduma sahihi za vipimo na uwekezaji mdogo katika viwanda vya usindikaji wa mazao vijijini.
Pia, ukosefu wa mitaji ya kuwawezesha wakulima kumiliki teknolojia bora za kuhifadhia mazao, uwekezaji hafifu katika tafiti na ubunifu na kukithiri kwa zana hafifu za kiasili katika kuhifadhi mazao.
Mkakati huo ulitaja maeneo ambayo mazao hupotea kwa wingi kuwa ni katika uvunaji, upukuchuaji, upembuaji, ukaushaji, usafirishaji, uhifadhi, usindikaji, ufungashaji na uuzaji.
Kastoly amesema tayari wamejenga friji kama hizo katika maeneo mawili tofauti nchini ambazo hutumiwa na vikundi vya wakulima kwa ajili ya kuhifadhia mazao yao baada ya kuvunwa.
Na ili mtu ajenge friji hilo anahitaji kuwa na sehemu maalumu ya kuhifadhia maji anayoweza kuwa anayatumia kupoza hali ya hewa pindi joto linapokuwa kali.
Maji hayo huweza kuwa yamehifadhiwa katika tanki la juu au kulingana na namna ambavyo mkulima ameamua.
Akieleza namna friji hilo linavyomsaidia katika shughuli zake za kila siku, Mhitimu wa Shahada ya Uchumi na Biashara Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), Iden Revocatus amesema imekuwa sehemu ya yeye kujitengenezea kipato cha kila siku.
Revocatus kwa sasa anatumia friji hilo kwa ajili ya shughuli zake za kilimo uyoga kuanzia kupanda hadi kuhifadhi baada ya kuvuna.
Akiwa amemaliza chuo mwaka jana, amekuwa akiuza uyoga huo Sh10, 000 kwa kilo moja ambao ni mbichi na ule uliokaushwa gramu moja ikauzwa kwa Sh10,000.
“Ukiwa mbichi unakuwa mzito lakini ukikaushwa inakuwa gramu 100 ndiyo maana bei zinakuwa hivi. Lakini uwepo wa friji hili ni fursa kwangu ya kujiajiri na kuajiri wengine ili waweze kujipatia kipato,” amesema Revocatus.
Akiwa ndiyo kwanza anaanza kuvuna, kwa siku huweza kuuza hadi kilo tatu za uyoga huku malengo yake yakiwa ni kuzalisha zaidi.
“Lengo langu ni kufanya uzalishaji zaidi ili niweze kuwa na bidhaa tofauti zinazotokana na uyoga kama mafuta ya kupakaa, sabuni, mvinyo, nisijifunge, kama mtu hawezi kula basi autumie ka namna nyingine,” amesema Revocatus.
Hata hivyo, kupitia mkakati huo ulioandaliwa na Serikali, uwekezaji mbalimbali unatarajiwa kufanyika ili kusaidia kupunguza upotevu huo huku matarajio yakiwa ni kusaidia kupunguza upotevu wa mazao ya chakula baada ya kuvunwa, kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya kilimo na kuongeza kipato cha mkulima.
“Pia, kuongeza uelewa wa wadau kuhusu athari za upotevu wa mazao baada ya kuvunwa katika uchumi, lishe ya jamii na uhakika wa chakula nchini, kuhimiza ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kukabiliana na upotevu wa mazao,” inaeleza sehemu ya wa Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mazao Baada ya Kuvuna wa mwaka 2019 hadi 2029.
Pia, unahamasisha na kuongeza uwekezaji katika utafiti, ugunduzi na upatikanaji wa teknolojia sahihi zinazoendana na mazingira ya Tanzania, kuongeza uwekezaji katika viwanda vya usindikaji wa mazao na upatikanaji wa masoko ya uhakika na kuongeza upatikanaji.