Dar es Salaam. Kauli ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido (DC), Mkoa wa Arusha, Marco Ng’umbi kuwa Serikali iliwezesha ushindi wa madiwani na baadhi ya wabunge nchini katika uchaguzi uliopita, imetonesha upya kidonda cha madai ya mifumo ya sheria za uchaguzi ili viongozi wanaopatikana watokane na matakwa ya wananchi.
Aidha, kauli hiyo imeelezwa inakwenda kinyume na falsafa za 4R za Rais Samia Suluhu Hassan za Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reforms (Mabadiliko) na Rebuilding (Kujenga upya) ambazo amekuwa anazitumia katika utawala wake.
Kwa nyakati tofauti, Rais Samia amekuwa akihubiri siasa za maridhiano na kufanyika kwa uchaguzi ulio huru na wa haki, na kuwataka wasaidizi wake kuhakikisha wanaziishia falsafa hizo.
Alichokisema Ng’umbi hakiko mbali na kile alichokisema aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kuwa matokeo ya kura sio lazima yawe yale ya kwenye boksi.
Kauli za wawili hao walizozitoa kwa nyakati tofauti ziliibua mijadala mikali. Mamlaka ya uteuzi wao, Rais Samia aliwatengua. Katika hili la Ng’umbi mjadala bado unaendelea, wadau wanataka hatua zaidi zichukuliwe ikiwemo kuhoji kile alichokisema.
Wadau hao wanakwenda mbali na kuonyesha hofu katika chaguzi zijazo ukiwamo wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 wakidai kilichoelezwa na wawili hao ndio uhalisi ambao umekuwa ukijitokeza.
Jana Jumapili, Septemba 1, 2024, katika mitandao ya kijamii, kulisambaa kwa kasi kipande cha video inayomwonyesha Ng’umbi akizungumza mambo kadhaa kuhusu uchaguzi wa mwaka 2020.
Katika picha hiyo jongefu ya dakika 1.32, Ng’umbi anasikika akiwaeleza watu aliowataja mara kadhaa kuwa ni madiwani kwamba ushindi wao katika uchaguzi huo si ujanja wao, bali ni nguvu ya Serikali.
Alikwenda mbali zaidi na kueleza hata waliopita bila kupingwa ni kazi iliyofanywa na Serikali na sio ubora wa wagombea husika.
“Kama kuna mtu ambaye si mwoga ni mimi, wote hapa madiwani mwaka 2020 hayupo diwani aliyepiga kampeni hapa. Sasa yale mazingira ya mwaka 2020 si kwamba yalikuja yenyewe moja kwa moja kwa sababu ninyi mlikuwa wagombea bora sana.
“Ni mazingira ambayo yalikuwa yametengenezwa na Serikali na Serikali ndiyo iliyoifanya kazi ile ya wewe kupita bila kupingwa. Kuna watu unafahamu kilichotokea huko kwenye pori anasema mimi sijui na mimi nilihusika kwenye majimbo fulani fulani,” alisikika Ng’umbi akisema katika kipande hicho cha video.
Hata hivyo, wakati mjadala ukiendelea, taarifa iliyotolewa jioni ya Septemba 1, 2024 na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga, ilieleza Rais Samia ametengua uteuzi wa Ng’umbi. Hata hivyo haikuelezwa sababu ya uamuzi huo.
Ng’umbi alikutana na kadhia hiyo ikiwa ni takriban siku 48 kupita tangu kauli kama hiyo kutolewa na Nape, Julai 15, 2024 alipotembelea soko la Kashai mkoani Kagera na kuzungumza na wananchi, ambapo alimhakikishia ushindi Mbunge wa Bukoba Mjini, Stephen Byabato.
Nape akiwa Waziri na Byabato, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki walitembelea eneo hilo. Nape alikuwa kwenye ziara aliyoianzia mkoani Kigoma, Kagera, Geita kisha Mwanza.
Katika maneno yake, Nape alisema: “Kashai oyee! Unajua nyie sikilizeni, matokeo ya kura sio lazima yawe yale ya kwenye boksi, inategemea nani anahesabu na kutangaza… na kuna mbinu nyingi, kuna halali, kuna nusu halali na haramu na zote zinaweza kutumika, ilimradi tu ukishamaliza unamwambia Mwenyezi Mungu nisamehe.”
Saa chache baada ya kauli hiyo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla aliijibu akisema sio kauli ya chama hicho.
Katikati ya mjadala mkali uliokuwa ukiendelea, Julai 21, 2024, Rais Samia alifanya mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri. Nape na Byabato walitenguliwa.
Mwananchi limezungumza na Diwani wa Longido, Thomas Ngobei juu ya kauli hiyo akisema aliitoa kwenye kikao cha kawaida cha baraza la madiwani na madai hayo hayakuwa ya kweli.
“Kwa kifupi Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan amechukua
hatua na ingetosha kusema kwamba jambo lile halikuwa sahihi. Niseme tu
halikuwa na ukweli wowote kwani mwaka 2020 wakati tuko kwenye uchaguzi hakuwa mkuu wa wilaya hapa, katika kata yangu kulikuwa na mgombea wa Chadema ila wakati wa ujazaji wa fomu hakurejesha fomu,” amesema.
Mmoja wa viongozi wa CCM, wilayani humo ambaye hakutaka kutaja jina lake, ameeleza mwaka 2020 wagombea wote wa udiwani katika kata 18 za jimbo hilo, walipita bila kupigwa.
Alichokisema Mbowe, Rungwe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema: “Sishangai hizo kauli, alichokizungumza DC huyu na Nape ndio ukweli, ila tatizo wamesema ukweli hadharani. Wabunge na madiwani wanajua kilichotokea hadi wakawa wabunge na madiwani.”
“Njia si kufukuza watu kazi, ni kuweka mifumo mizuri ya uchaguzi ili kutoruhusu hayo, tunataka tume huru isimamie chaguzi zote za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu,” amesema Mbowe.
Kuhusu kauli za viongozi wa CCM na Serikali kuwa uchaguzi utakuwa huru na haki, Mbowe alisema, zimekuwa zikitolewa mara kadhaa ikiwemo awamu ya tano na uchaguzi ulipofika hazikuzaa matunda.
“Kungekuwa na dhamira za kweli kuwa uchaguzi utakuwa huru wasingekuwa wanatoa matamko, wangeweka mifumo mizuri ambayo ni sheria na si matamko,” amesema na kuongeza:
“Sisi tunajipanga, tunakwenda kwenye chaguzi tukijua tunakabiliana na hatari namna gani, lakini haya mambo ndiyo yanaleta machafuko, viongozi wanalazimishwa kushinda, kumfukuza kazi ni kumwonea, ukweli wanajua hiyo ndiyo hali halisi.”
Mwenyekiti mstaafu wa chama cha ADC, Hamad Rashid amesema kauli hiyo inakwenda kinyume na falsafa ya 4R za Rais Samia.
“Falsafa ile ilitaka tufanye siasa za kistaarabu, atakayeshinda au kushindwa apatikane, kwa hiyo amekwenda kinyume na mwongozo wa Rais aliye madarakani ndio maana akachukua hatua haraka. Kwa hiyo tunatarajia hizi kauli zidhibitiwe na ziingie katika hatua ya utekelezaji,” amesema.
Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe amesema: “Alichokisema ni sawa, tatizo yeyote anayesema ukweli wanamwondoa. Yeye amesema ukweli na Mungu amzidishie mema.”
Hata hivyo, Rungwe amesema chama chake kinajipanga kwa ajili ya uchaguzi ujao.
“Sisi tutashiriki kwenye uchaguzi, tutaangalia tukiona yamekuwa hovyo zaidi tutaacha,” amesema.
Kuhusu kauli hiyo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema kauli hiyo ataitolea ufafanuzi kwenye mikutano yake ya hadhara atakayoifanya mkoani Arusha kuanzia Septemba 4 hadi 7, 2024 katika wilaya za Longido, Karatu na Monduli.
“Kutokana na jambo hilo naomba kuweni na subira nitalitolea ufafanuzi siku zijazo katika mikutano ya hadhara nitakayofanya Arusha,” amesema.
Katika andiko lake alilolitoa kwenye mitandao ya jamii, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amesema kuna kundi la watu lililoteka falsafa ya 4R za Rais Samia.
Andiko hilo lenye kichwa kisemacho, ‘Mtekaji wa 4R akamatwa na kutenguliwa,’ alihoji, “Je, madiwani haramu wanaweza kutunga sheria halali katika halmashauri zetu?”
“DC mtenguliwa anakiri kushiriki operesheni za maporini katika wilaya kadhaa. Je, zilikuwa zipi hizo? Haziwezi kuwa za kuiba kura kwa sababu madiwani walipita bila kupingwa. Jinai haiozi; utenguzi ufuatwe na uchunguzi,” ameshauri.
“Mheshimiwa Rais asiishie kutengua waropokaji. Hata KM (Katibu mkuu) wa chama asiishie kukanusha wanaojinadi kuteka au kutishia kutumia dola kukimbia na masanduku. Kinachowawasha waropokaji hatukijui lakini kwa hakika waropokaji hawa ni maadui wa CCM kuliko wapinzani,” ameandika.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga amesema Ng’umbi ametoa kauli ya ukweli kwa kuwa mambo hayo yalitokea kweli.
“Kauli hiyo imetusikitisha sisi wapiga kura na wadau wa demokrasia, lakini inatusaidia kujua kweli kwamba uchaguzi wetu huwa hauwi wa haki.”
“Kauli hiyo si ya kwanza, kuna mmoja alishasema watashinda kwa bao la mkono na huyohuyo akasema anayehesabu kura na kutangaza matokeo ndiye anayejua mshindi, kwa hiyo kwenye demokrasia bado tuna safari ndefu,” amesema.
Dk Henga amesema pamoja na Ng’umbi kusema ukweli, bado ametenguliwa kwa kuonewa.
‘Dola imekuwa inatumika’
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisilie amesema kauli ya kiongozi huyo inaashiria ulevi wa madaraka na inajulikana Afrika nzima kwa vyama vyote tawala vimekuwa vikifanya hujuma katika chaguzi.
“Vyama ikiwemo CCM, vimekuwa vikitumia Dola kwa kiasi fulani lakini Tanzania kilichotokea katika chaguzi za mwaka 2019 na 2020 ilikuwa imezidi,” amesema.
Amesema kauli ya Ng’umbi kwamba yeye ana nguvu ni kuonesha wananchi hawana nafasi ni hali ya ulevi wa madaraka inaonesha wazi.
Machi 2020, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alinukuliwa na moja ya chombo cha habari akisema vyama tawala kama Kanu cha Kenya na Unip cha Zambia vilishindwa kutumia nafuu ya madaraka na dola, ndio maana viliondolewa.
“Unashika dola halafu unatumia dola kubaki kwenye dola, halafu akitokea mtu ambaye ana busara zaidi kukwambia usitumie dola kubaki kwenye dola ukamsikiliza, siku ukishatoka hurudi,” alisema Dk Bashiru ambaye sasa ni mbunge wa kuteuliwa.