Kesi ‘waliotumwa na afande’ kuendelea leo

Dodoma. Kesi ya kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam, inayowakabili washtakiwa ‘wanaodaiwa kutumwa na afande’ leo Jumatatu, Septemba 2, 2024 inaendelea kusikilizwa.

Wakili anayewawakilisha washtakiwa, Godfrey Wasonga amesema kuwa kesi hiyo itasikilizwa mfululizo kuanzia leo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas, maarufu kama Nyundo, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.

Walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 19, 2024 na kusomewa mashtaka mawili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Zabibu Mpangule. Walikana mashtaka hayo.

Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa mfululizo kuanzia Agosti 20 hadi 23, 2024, lakini ilisimama kwa siku tano ili kupisha uamuzi mdogo wa shauri la maombi kupitia mwenendo wa kesi hiyo lililofunguliwa na wakili Leonard Mashabara kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.

Hata hivyo, Mahakama Kuu ililitupitilia mbali shauri hilo kwa kile kilichoelezwa kuwaingiza watu wasiohusika kwenye kesi ya msingi kujibu maombi ya mwenendo wa kesi hiyo.

Jaji wa Mahakama Kuu, Suleiman Hassan alisema waliongizwa kama wajibu maombi kwenye kesi hiyo ambao hawahusiki kwenye kesi ya msingi ni Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mawakili wanne wanaowawakilisha washtakiwa.

Baada ya Mahakama Kuu kulitupilia mbali shauri la marejeo ya mwenendo wa kesi hiyo washtakiwa hao waliendelea na kesi Agosti 30, 2024 ambapo mashahidi watatu walitoa ushahidi wao na kufanya mashahidi waliotoa ushahidi kufikia sita.

Related Posts