KESI YA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA: Wapingaji watakiwa kufungua kesi ya kikatiba, wakataa

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imewataka wanaharakati wanaotaka kufungua kesi ya kupinga uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 kusimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi,) wafungue kesi ya kikatiba badala ya utaratibu wanaotaka kuutumia wa mapitio ya Mahakama.

Pendekezo hilo ni moja ya hoja za pingamizi la Serikali dhidi ya shauri la maombi ya ridhaa ya kufungua shauri la kupinga uchaguzi wa serikali za mitaa kusimamiwa na Tamisemi.

Wanaharakati hao, ambao pia wanaojitambulisha ni raia waliosajiliwa katika daftari la kudumu la wapiga kura wamefungua shauri la maombi ya ridhaa, wakiomba kuruhusiwa kufungua shauri la kupinga uchaguzi huo kusimamiwa na Tamiseni, kwa utaratibu wa mapitio ya Mahakama (Judicial review).

Waliofungua shauri hilo ni Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Bob Wangwe, mwanahabari mstaafu, Ananilea Nkya na Bubelwa Kaiza na wajibu maombi ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Shauri hilo la maombi namba 19721/21 linalosikilizwa na Jaji Wilfred  Dyansobera, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.

Wanaharakati hao wanaomba waruhusiwe kufungua shauri la kupinga  uchaguzi wa Serikali za Mitaa kusimamiwa na Tamisemi badala ya Tume Huru ya Uchaguzi.

Hata hivyo, Serikali imeweka pingamizi la awali wakiiomba Mahakama iyatupilie mbali maombi hayo huku wakibainisha hoja nne za kisheria.

Pingamizi hilo la kisheria limesikilizwa leo Jumatatu, Septemba 2, 2024 ambapo jopo la mawakili wa Serikali

likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo limefafanua sababu hizo za mapingamizi.

Katika sababu ya kwanza, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Erigh Rumisha ameieleza Mahakama waombaji hawakupaswa kufungua shauri hilo la kuomba ridhaa kufungua shauri la mapitio kwa kuwa walikuwa na njia mbadala ya kufanya.

Amefafanua ili kufungua maombi ya mapitio ya Mahakama lazima mwombaji athibitishe hakuna njia nyingine mbadala isipokuwa kwa njia ya mahakama tu, na kwamba kushindwa kulithibitisha hilo mahakama inapaswa kuyatupilia mbali.

Wakili Rumisha amebainisha kwa kuwa wanaomba Mahakama itengue kanuni zilizotungwa na waziri wakati kuna sheria inayompa mamlaka ya kutunga kanuni hata kama mahakama ikitoa amri ya kutengua kanuni hizo, wakati sheria bado ipo haitakuwa na maana.

Hivyo kabla ya kufungua shauri hilo la mapitio ya Mahakama walipaswa kwanza kufungua kesi ya kikatiba,  kupinga sheria kwa sababu katika shauri la mapitio Mahakama haiwezi kubatilisha hizo sheria.

“Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ambayo ndio wameitaja imeanza kutumika Aprili 12, 2024 lakini kuna chombo cha kikatiba kilichoanzishwa, ambacho kina mamlaka ya kipekee ya kusimamia uchaguzi huo. Na wakati sheria hiyo inatungwa, sheria hizo zilikuwepo na bado zipo,” amesema Rumisha.

Katika sababu ya pili ya pingamizi hilo, Serikali imedai kiapo kinachounga mkono maombi hayo kina kasoro kwa kuweka mambo yasiyohitajika kuwemo kama vile hoja za kisheria, maoni na hitimisho.

Wakili Sanga amehitimisha kuwa tiba pekee ya kasoro hiyo ni Mahakama kuziondoa aya hizo zenye kasoro katika kiapo hicho huku akibainisha kama aya hizo zitaondolewa basi zitakazobaki hazitakuwa na nguvu ya kuweza kuunga mkono maombi hayo, hivyo yanapaswa kutupiliwa mbali.

Katika hoja ya tatu na ya nne Wakili Sanga amesema zinakiuka Kanuni ya 5 (2) (d) ya Sheria ya Maboresho ya Sheria (Kuhusu Ajali Mbaya na Masharti Mengineyo, Tangazo la Serikali (GN) Namba 324 la mwaka 2024.

Amedai kanuni hiyo inayohusu uendeshaji wa mashauri ya namna hiyo kiapo kinapaswa kuthibitisha taarifa zilizomo kwenye maelezo ya kesi ili kuyafanya maelezo hayo kuwa sehemu ya ushahidi.

Huku akitaja baadhi ya aya na maelezo yake, Wakili Sanga amedai hata hivyo kiapo hicho kina mambo mengine ambayo hayamo katika maelezo ya kesi yaliyowasilishwa mahakamani.

Hivyo amedai taarifa hizo kuwepo kwenye kiapo bila kuwepo kwenye maelezo yaliyowasilishwa mahakamani, hivyo zinapaswa kuondolewa kwenye kiapo hicho na kama zikiondolewa basi kiapo kitakachobaki hakitakuwa na nguvu ya kuunga mkono maombi hayo kuendelea kuwepo mahakamani, hivyo maombi hayo yanapaswa yaondolewe.

Akihitimisha hoja hizo kiongozi wa jopo, Wakili Mulwambo amedai, “tunatambua kuna baadhi ya mashauri mengine kama ya kikatiba gharama huwa hazitolewi lakini Mahakama inaweza kutoa gharama kulingana na mazingira. Hivyo kwa mazingira haya ya mapungufu haya na kwa ubobezi wa mawakili hawa Mahakama inaweza ikatoa gharama”, amesema Wakili Mulwambo

Hata hivyo, mawakili wa waombaji hao wamezipinga hoja za pingamizi lililoibuliwa na wajibu maombi hao wakidai hazina mashiko kwa kuwa hazijakidhi matakwa ya kisheria ya kuwa hoja za pingamizi.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa waombaji hao, Mpale Mpoki amedai pingamizi linahusu ukiukwaji wa sheria na walipaswa waonyeshe kuwa ni kifungu gani kilichovunjwa.

Akijibu hoja ya kwanza Wakili Mpoki amedai kwa mujibu wa sheria walizozitumia waombaji kufungua maombi hayo, hakuna fursa au njia nyingine inayobainishwa ambayo wangeweza kuitumia zaidi ya kufungua maombi hayo, “hata wajibu maombi  hawajaitaja.”

Amedai katika maombi hayo hakuna mahali ambako waombaji wanaeleza kuna haki wanataka kuitekeleza bali kuiomba Mahakama itoe amri za kutengua kanuni za uchaguzi huo zilizotungwa na waziri.

Kuhusu hoja ya kasoro za kiapo, Wakili Mpoki amedai hakuna mahali ambako sheria inasema maoni hayakubaliki katika kiapo, huku akifafanua kiapo hicho hakina mambo yasiyohusika, kwa kuwa yote yaliyomo yanahusiana na shauri hilo.

“Mambo mengi yaliyomo ni ukweli kabisa, mfano kwamba sheria imetungwa (ya Tume Huru ya Uchaguzi).  Kwa hiyo kusema hilo hitimisho si sawa maana kweli sheria ilitungwa,” amesema Mpoki.

Kwa upande wake Wakili Jebra Kambole amedai ingawa mawakili wa Serikali wameorodhesha aya mbalimbali za kiapo hicho, lakini wakati wakitoa ufafanuzi hawakuweza kubainisha shida ya aya hizo.

“Kwa kutokueleza shida iliyoko katika hizi aya sisi tunaamini kwamba ziko sawa. Tunaomba Mahakama itambue kuwa aya 1-7, 8, 9, 11, 13, 14, 18, 19 na 20 hazina shida yoyote”, amedai Kambole.

Kuhusu aya ambazo mawakili wa wajibu maombi wamedai kuwa zina mambo yasiyohitaji kuwemo Wakili Kambole amedai kuwa mambo yote yaliyomo humo huku akiyataja kwa kila aya ni taarifa za kweli.

Baadhi ya taarifa hizo ni maelezo kuwa waziri wa Tamisemi ndiye anahusika na uchaguzi huo, kwamba ni mwanachama wa chama tawala na hivyo yuko katika mgogoro wa kimasilahi, na kwamba ndio maana  Bunge limetunga Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi.

“Kwa hiyo ni hoja yetu kwamba hizo aya hazina shida na kiapo hiki kilichowasilishwa mahakamani kipo sahihi kabisa, kimeandaliwa kulinga na mazingira ya kesi yenyewe kama ilivyo,” amesema Wakili Kambole.

Pia amesisitiza hakuna taarifa ambazo wanasema ni mpya zilizoko kwenye kiapo ambazo hazipo kwenye maelezo na kwamba Kanuni ya 5 (2) haina hilo takwa kuwa  taarifa zilizoko kwenye maelezo ndio hizohizo tu zinazopaswa ziwepo kwenye kiapo.

Amedai maelezo ya kesi hayana huo ushahidi na ushahidi uko kwenye kiapo ambacho ndio kinapaswa kufafanua yale yaliyoko kwenye maelezo.

Shauri hilo litaendelea kusikilizwa kesho

Related Posts