Kipengele cha kuthibitisha mtoa rushwa, mpokeaji chang’olewa kwenye sheria

Dodoma. Changamoto za Serikali kushindwa kesi za uchaguzi, michezo ikiwamo ya kubahatisha na burudani, imepatiwa ufumbuzi baada ya kuondolewa kipengele cha kuthibitisha mtoa rushwa na mpokeaji.

Mbali na changamoto hiyo kupatiwa ufumbuzi,  mapendekezo  mapya ni kwamba, rushwa ya ngono sasa ni kosa kwa mtu anayeahidi au kutoa kwa mwenye mamlaka ili kupata upendeleo wa ajira, cheo na haki.

Hivyo, wanawake au wasichana wanaotumia ushawishi wa ngono kupata ajira, cheo au upendeleo mwingine pia watakuwa wametenda kosa la rushwa.

Mapendekezo hayo yamo kwenye Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wa mwaka 2024, uliowasilishwa leo bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.

Simbachawene amesema kuna changamoto ya kuchunguza tuhuma za rushwa katika maeneo ya uchaguzi, michezo ikiwamo ya kubahatisha na burudani kwa kutumia kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, kinachohusu hongo.

Amesema kifungu hicho kinahitaji kuthibitisha uwepo wa uhusiano kati ya mtoaji na mpokeaji wa rushwa, lakini haupo kwenye maeneo hayo, hivyo kusababisha Serikali kushindwa kesi hizo mahakamani.

Pia, katika mapendekezo mengine, Ibara ya 10 inapendekeza kufuta kifungu cha 25 kilichopo na kukiandika upya.

Amesema kifungu kinachopendekezwa kinasema: “Ni kosa kwa mtu mwenye mamlaka kuomba rushwa ya ngono au upendeleo mwingine kama sharti la kutoa au kupata ajira, cheo, haki au upendeleo wowote.”

Aidha, Simbachawene amesema kifungu hicho kinaeleza kuwa mtu atakayetiwa hatiani kwa makosa hayo atapewa adhabu ya faini isiyopungua Sh2 milioni na isiyozidi Sh10 milioni au kifungo kisichopungua miaka mitano.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Joseph Mhagama amesema muswada huo unakusudia kurekebisha sheria hiyo ili kutatua baadhi ya changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake.

Amesema pia, unalenga kuimarisha malengo makuu ya sheria hiyo ambayo ni kuzuia, kuchunguza na kupambana na rushwa na makosa yanayohusiana na hayo pamoja na kuhakikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

“Mapendekezo ya mabadiliko ya sheria katika kifungu cha 25 hasa ongezeko la kifungu kipya cha 25(1)(b), kimeleta hisia hasi kwa wadau waliofika mbele ya kamati, asasi za kiraia na wanaharakati mbalimbali kwenye vyombo vya habari na mitando ya kijamii.

“Wadau wengi wamelalamikia kifungu hicho kwa mtazamo kuwa, kinawanyima waathirika wa rushwa ya ngono haki zao stahiki na kinawapa kinga wahusika wa vitendo hivyo,” amesema Dk Mhagama.

Amesema kamati ilibaini kuwa chimbuko la mapendekezo ya kumhusisha mtu atakayeshawishi rushwa ya ngono kwa mwenye mamlaka,  na yeye awe ametenda kosa linatokana na mikataba ya kimataifa na kikanda.

Dk Mhagama amesema Zanzibar kupitia Baraza la Wawakilishi imeweka wazi kwenye Sheria ya Kupambana na Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2023, kifungu cha 52, kwamba ni kosa kushawishi kutoa rushwa ya ngono.

Pia, kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, sura ya 329, kinaainisha kuwa ni kosa kwa mtu yeyote atakayetoa au kuahidi kutoa rushwa ili kupata upendeleo wowote.

Kuhusu marekebisho mengine, Dk Mhagama amesema Ibara ya 14 kwenye kifungu cha 38A(1) inalenga kumpa mamlaka mkurugenzi mkuu wa taasisi, baada ya kupata idhini ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kumuelekeza ofisa uchunguzi mwandamizi au mkuu wa taasisi kuzuia fedha za mtuhumiwa zinazohusika na uchunguzi zilizopo kwenye akaunti ya benki au miamala ya kifedha; na kuchukua nyaraka kutoka benki au taasisi ya fedha kwa siku 21, huku idhini ya  Mahakama ikifuatiliwa.

Awali, kamati iliishauri Serikali kutafuta kwanza idhini ya Mahakama kabla ya kuzuia fedha au nyaraka kutoka benki au taasisi ya fedha.

Baada ya kujadili ugumu wa uchunguzi na uwezekano wa fedha kuhamishwa au nyaraka kuharibiwa, kamati ilishauri idadi ya siku kupunguzwa kutoka 21 hadi 14 na idhini ya Mahakama itafuatiliwa ili kuendelea kuzuia au kuachilia akaunti ya mtuhumiwa.

Related Posts