China imeongeza mahusiano yake na mataifa ya Afrika katika kipindi cha muongo mmoja uliiopita, ikiyamwagia mabilioni ya fedha kupitia mikopo ambayo imeyasaidia mataifa hayo kujenga miundo mbinu.
Lakini pia baadhi ya wakati nchi hiyo imeonesha kuibuwa utata kutokana kuzibebesha madeni makubwa nchi nyingi za bara hilo.
China imepeleka mamia kwa maelfu ya wananchi wake kufanya kazi barani Afrika katika sekta za ujenzi wa miradi yake mikubwa huku ikijipatia rasilimali nyingi za barani huko zikiwemo shaba,dhahabu,chuma na madini mingine yasiyopatikana kirahisi duniani.
Tayari serikali ya mjini Beijing imeshasema kwamba mkutano wa kilele wa wiki hii kati ya China na Afrika utakuwa ni mkutano mkubwa kabisa wa kidiplomasia kuwahi kufanywa tangu janga la Uviko-19,ambapo viongozi kutoka Afrika Kusini,Nigeria,Kenya na mataifa mengine wamethibitisha kushiriki.
Nchi za Afrika zinatarajia kutafuta fursa ya kuleta maendeleo kutoka China,amesema hivyo mchambuzi wa masuala ya sera katika shirika moja la ushauri wa masuala ya maendeleo,Ovigwe Eguegu.
Soma pia:China au Marekani: Nani anachelewesha msamaha wa madeni kwa mataifa maskini?
Shirika la habari cha China limesema,nchi hiyo ambayo inashikilia nafasi ya pili duniani kwa kuwa na uchumi mkubwa, ni mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa bara la Afrika,ambapo biashara kati ya pande hizo mbili ilifikia dola bilioni 167.8 katika nusu ya mwanzo ya mwaka wa kiuchumi.
Mwaka jana mikopo iliyotolewa na China kwa mataifa ya Afrika ilikuwa ndio mikubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitano,kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya data ya China kuhusu mikopo kwa Afrika.Nchi zilizopokea mikopo mikubwa zaidi ni Angola,Ethiopia,Misri,Nigeria na Kenya.
Wachambuzi: Beijing inajikongoja kiuchumi
Lakini wachambuzi wanasema kujikokota kwa hali ya ukuaji kiuchumi nchini China kumeifanya serikali ya Beijing hivi sasa kuendelea kujizuia kutoa mikopo mikubwa.
Pia imejizuia kusamehe madeni yake hata katika wakati ambapo baadhi ya mataifa ya Afrika yanahangaika kulipa madeni yao,na baadhi zikilazimika kupunguza bajeti zao za matumizi katika huduma muhimu za umma.
Tang Xiaoyang kutoka chuo kikuu cha Tsinghua mjini Beijing,ameliambia shirika la habari la AFP kwamba tangu mkutano uliofanyika miaka sita iliyopita kati ya China na Afrika,ulimwengu umeshuhudia mabadiliko makubwa ikiwemo janga la Corona,mivutano ya kisiasa ya kikanda pamoja na hivi sasa changamoto za kiuchumi.
Soma pia:Mikopo inayohusishwa na maliasili za Afrika yakosolewa
Amesema kutokana na yote hayo,mtindo wa zamani wa kutowa mikopo mikubwa kwaajili ya miradi ya miundo mbinu na ukuzaji wa kasi wa kiviwanda,ni suala ambalo hapana shaka haliwezekani tena.
Bara la Afrika ni muhimu kwa mradi wa China wa ujenzi wa miundo mbinu ya reli na barabara ambao ni nguzo muhimu ya mpango wa rais Xi Jinping wa kutanuwa ushawishi wa nchi yake Kimataifa.
Afrika yabebeshwa mzigo wa madeni
Wakosoaji wanailaumu serikali ya Beijing kwa kuyabebesha mizigo mizito ya madeni mataifa hayo na kufadhili miradi ambayo inaharibu mazingira.
Miongoni mwa miradi yenye utata ni ule wa ujenzi wa reli wa Kenya uliogharimu dola bilioni 5,uliofadhiliwa kwa mkopo kutoka benki ya Exim ya China.
Reli hiyo inauunganisha mji mkuu Nairobi na ule wa bandari wa Mombasa.Hata hivyo awamu ya pili ya mradi huo iliyokusudiwa kuendelea kwa ujenzi wa reli hiyo kuelekea nchini Uganda haikufanikiwa huku nchi zote mbili Kenya na Uganda zikihangaika kulipa madeni.Kenya inadaiwa zaidi ya bilioni 8 na China.
Soma pia:Utafiti: China yaongeza utoaji wake mikopo kwa Afrika
Katika kanda ya Afrika ya Kati,nchi za Magharibi na makampuni ya China zinapambana kuwania madini adimu yanayopatikana kwenye eneo hilo.
Kuongezeka kwa mivutano wa siasa za kimaeneo kati ya Marekani na China ambazo zinavutana kuhusu takribana kila kitu kuanzia suala la hadhi ya kisiwa cha Taiwan hadi biashara pia zinapambana kuwania ushawishi barani Afrika.
Mchambuzi wa masuala ya sera,Eguegu anasemamataifa ya Afrika huenda yakalazimika kuchaguwa yanasimama upande gani. Mtaalamu huyo anasema hivi sasa mataifa ya Afrika hayana ubavu wa kuipinga China.