BAADA ya kurejea nchini, beki Lameck Lawi amesema hatma ya yeye kuitumikia Coastal Union ipo chini ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Lawi ambaye anatajwa kusaini mkataba ndani ya Simba, ameshindwa kuitumikia timu hiyo na badala yake alitimkia Ubelgiji kwa ajili ya kujiunga na Klabu ya K.A.A Gent lakini mambo yameenda tofauti, hivyo amerudi Tanzania.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lawi alisema amerejea nchini na anaendelea kufanya mazoezi na Coastal Union huku akisubiri kuanza kucheza mechi za ligi.
“Nipo nchini, kwa sasa siwezi kuzungumza chochote kuhusiana na mambo yaliyotokea Ubelgiji, kikubwa ninachoweza kusema naendelea kujifua na Coastal Union, kuhusiana na kucheza sijajua hatma yangu hadi sasa,” alisema na kuongeza;
“Tangu nimerudi nipo pamoja na Coastal Union lakini mambo bado hayajakaa vizuri kwenye suala la Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ambapo ndio kesi ipo huko, hivyo mambo yakienda sawa nitacheza.”
Lawi akizungumzia namna mchakato wake wa usajili ulivyoenda alisema anapitia wakati mgumu sasa kutokana na kukosa nafasi ya kucheza kuendeleza alipoishia msimu uliopita na hatimaye kufikia malengo.
“Siwezi nikawa sawa wakati sichezi na ligi inaendelea, hakuna mchezaji ambaye anapenda kukaa nje ya uwanja wakati anaona ana ,uwezo wa kucheza lakini naamini muda utafika nitacheza,” alisema.
Wakati Lawi akifunguka hayo, chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Coastal Union kimeliambia Mwanaspoti kuwa beki huyo atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaocheza mechi ijayo.
“Lawi ni mchezaji wa Coastal Union, ni kweli kamati ilitupa nafasi ya sisi na Simba kumalizana na hilo limefanyika, huyu ni mchezaji wetu na mchezo ujao mtamuona akiitumikia timu yake aliyoipa mafanikio msimu uliopita,” kimesema chanzo hicho.
Wakati Coastal Union wakisema hivyo, Simba wameendelea kusisitiza kwamba walimsajili nyota huyo hivyo ni mchezaji wao.