Mchungaji aitaka Serikali ipitie upya leseni za waganga wa kienyeji

Tabora. Mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Lutengano Mwasongela ameishauri Serikali kupitia Wizara ya Afya kufanya mapitio ya leseni wanazotoa kwa waganga wa kienyeji kwa lengo la kuhakikisha wanaopewa wanafanya yale yanayokusudiwa kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Septemba 2, 2024, Mwasongela amesema hivi karibuni mganga aliyekuwa akiishi mkoani Singida anadaiwa kuzika miili ya watu 10 kwenye makazi yake, jambo ambalo ni la hatari.

“Tumekuwa tukiona kwenye vyombo vya habari kwamba kuna watu 10 wamekutwa wamefariki na kufukiwa huko Singida, wakihusishwa na mganga wa kienyeji. Ukiangalia kwa undani, wale watu hawatajwi majina yao, kiukweli hii haikubaliki na sisi kama kanisa tunakemea kwa nguvu zote,” amesema Mwasongela.

Ameiomba Serikali ipitie upya leseni wanazotoa kwa waganga wa kienyeji, ili watoe huduma kama sheria inavyotaka.

Amesema kama mganga anaweza kufanya vitendo vya mauaji, ina maana anakwenda kinyume na sheria za matibabu.

Hata hivyo, Mwasongela amesema tabia za watu kupotea huanza kuonekana nyakati za uchaguzi.

Amewataka wananchi kama watabaini kuna mtu anasaka uongozi kwa kutaka kumwaga damu ya mtu, wamuogope na wasithubutu kumchagua.

Kwa upande wake, Naomi Lutengano amesema chanzo cha mauaji kuendelea kushika kasi hususan kwa waganga, ni watu kukosa imani juu ya Mungu na kuamini nguvu za giza.

“Watu wengi kwa siku za karibuni wamekuwa hawaamini katika Mungu, hivyo wanajikuta wametumbukia katika imani mbadala ili kufanikisha mambo yao. Ipo haja kwa watu kuamini katika Mungu aliye hai, ili kuepukana na waganga,” amesema.

Shadrack Herman, mkazi wa Manispaa ya Tabora na muumini wa kanisa la TAG, amesema changamoto ya watu kuuawa na waganga inatokana na imani potofu.

“Watu wengi wanadanganywa kwamba ili upate nguvu fulani, lazima upeleke kiungo kwa waganga na ukifuatilia kwa undani hayo mambo hayana nafasi hata kidogo. Kwa hivyo, naunga mkono kauli ya mchungaji wetu kwamba leseni za waganga wote zipitiwe upya, ili kuondoa mauaji yasiyo ya lazima kwenye jamii,” amesema.

Akizungumza katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la TAG, Manispaa ya Tabora, Meya wa Manispaa ya Tabora, Ramadhani Kapera amesema Watanzania wamebadilishwa akili na waganga wa kienyeji, huku wakitaka kujipatia utajiri bila kufanya kazi.

“Kumekuwa na changamoto ya vijana na watu wengi kutofanya kazi na badala yake wanategemea waganga kutimiza ndoto zao.

“Lazima tuseme ukweli kwamba wanaotegemea miujiza ya kufanikiwa bila kufanya kazi hawawezi kufanikiwa kamwe. Hivyo, viongozi wa dini mna kazi ya ziada ya kubadili fikra za watu kujua wajibu wao, badala ya kuamini kwamba waganga wanaweza kuwapa nguvu za kupata fedha,” amesema meya huyo.

Related Posts