Wafanyakazi hao wanapinga hatua za serikali kushindwa kuumaliza mzozo huo na kufanikisha kuwarejesha nyumbani mateka waliosalia mikononi mwa kundi la Hamas.
Mgomo huo unaoongozwa na muungano wa mashirika ya wafanyakazi ya Israel, Histadrut umekwamisha shughuli za kibiashara na kijamii. Idadi kubwa ya miji na jamii kadhaa zilijiunga na maandamano hayo, huku baadhi wakikataa kufanya hivyo kwa kuwa wanaunga mkono serikali ya mrengo wa kulia ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Katika miji mingi, shule, benki na ofisi za serikali zimefungwa huku usafiri wa umma pia ukiathirika pakubwa. Lakini shughuli katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion ulio karibu na Tel Aviv ziliendelea kama kawaida tofauti na ilivyoelezwa hapo awali.
Siku ya Jumapili, Muungano huo wa mashirika ya wafanyakazi Histadrut ulisema unalenga kukwamisha shughuli zote nchini humo kwa kuitisha mgomo wa kitaifa wa siku moja. Lengo kuu ikiwa ni kuongeza shinikizo kwa Netanyahu kukubali makubaliano ya usitishwaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka waliosalia Gaza.
Kiongozi wa muungano huo wa Histadrut Arnoni Ben-David amesema hawawezi kukaa na kushuhudia mateka wakiendelea kuuawa katika mahandaki ya Gaza, jambo ambalo amesema halikubaliki.
Soma pia: Mkuu wa sera za nje wa EU Joseph Borrell ashtushwa na mauaji ya mateka 6 wa Israel
Mbali na mgomo huo, baadhi ya raia waliandamana pia mjini Tel-Aviv wakiwa na malalamiko kama hayo. Adva Adar , ni binamu wa mateka Tamir Adar ambaye tayari alifariki:
“Kwa kweli tunatarajia serikali yetu itafikia mpango huo na kuhakikisha kuwa mateka wote wanarejea hivi karibuni.”
Jamaa na mawakili wa mateka wameushutumu utawala wa Netanyahu kwa kutochukua hatua zaidi za kuwarejesha mateka wakiwa hai, na wametaka kusitishwa kwa mapigano mara moja ili kuwaokoa mateka waliosalia.
Biden akutana na wapatanishi katika mzozo wa Gaza
Rais wa Marekani Joe Biden na Makamu wake na mgombea urais kupitia chama cha Democratic Kamala Harris wamekutana hivi leo na timu ya wapatanishi wa Marekani katika mzozo wa Gaza ambao wanajaribu kuhimiza kufikiwa kwa makubaliano ya usitishwaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka.
Mkutano huo unafuatia mauaji ya siku ya Jumamosi ya mateka sita huko Gaza akiwemo raia mmoja wa Marekani aliyefahamika kwa jina la Hersh Goldberg-Polin. Kwa miezi kadhaa sasa, Marekani, Misri na Qatar, wamekuwa wakijaribu kufikiwa kwa mkataba wa kusitishwa vita huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka wa Israel pamoja na wafungwa wa Kipalestina.
Wakati wa shambulio lao la Oktoba 7 mwaka jana, wanamgambo wa Hamas waliwachukua mateka 251. Makumi kadhaa waliachiliwa huru kufuatia makuliano ya mwezi Novemba na sasa wamesalia mateka karibu 97 huko Gaza ambao 33 kati yao wameelezwa na jeshi la Israel kwamba tayari wamekwishafariki.
Vyanzo: (DPAE, AFP)