Akiwahutubia wanafunzi katika hafla iliyooneshwa kupitia televisheni katika jimbo la Siberia nchini Urusi, Putin alisema kuwa jaribio la Ukraine la kusitisha kusonga mbele kwa vikosi vya Urusi katika eneo la Donbass kwa kufanya mashambulizi katika eneo la Kursk halijapata ufanisi.
Urusi yaishambulia Ukraine usiku kucha
Putin amesema hayo saa chache baada ya Urusi kuishambulia Ukraine usiku kucha kwa makombora na droni na kuwajeruhi takriban watu watatu huko Kyivna kuharibu msikiti mmoja muda mfupi kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa shule.
Poland yasema uanachama wa NATO hauzuii nchi mwanachama kujilinda
Wakati wa mahojiano na gazeti la Financial Times la Uingereza yaliochapishwa leo, waziri wa mambo ya nje wa Poland Sikorski amesema uanachama katika jumuiya ya kujihami ya NATO hauzuii jukumu la kila nchi mwanachama la ulinzi wa anga yake.
Soma pia: Putin asema uvamizi wa Ukraine Kursk haujawa na athari
Matamshi ya Sikorski, yanakuja wiki moja baada ya kuingiliwa kwa anga yake katika kile ambacho jeshi limesema huenda ikawa ni droni baada ya Urusi kufanya mashambulizi mabaya nchini Ukraine.Licha ya juhudi za wiki moja ya utafutaji, droni hiyo inayoshukiwa haijapatikana.
Wakati wa wimbi jipya la mashambulizi ya anga ya Urusi siku ya Jumatatu, Poland ilituma ndege zake za kivita hadi kwenye mpaka wa Ukraine ili kulinda anga yake.
Ukraine yatumaini kupata ruhusu kufanya mashambulizi ya masafa marefu
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, amesema leo kwamba nchi hiyo, ina matumaini juu ya matarajio ya kupata ruhusa kutoka kwa washirika wake wa magharibi kufanya mashambulizi ya masafa marefu dhidi ya shabaha zake ndani ya Urusi.
Soma pia:Ukraine yalishambulia kwa makombora eneo la Belgorod
Baada ya mkutano wake na waziri mkuu wa Uholanzi Dick Schoof katika mji wa Zaporizhzhia kusini mashariki mwa Ukraine, Zelensky alisema kuwa ruhusa pekee haitoshi lakini kwamba washirika hao wanapaswa kusambaza silaha za mashambulizi kama hayo.
Miili ya watu 22 waliofariki katika ajali ya helikopta yapatikana
Katika hatua nyingine, maafisa wa kukabiliana na hali za dharura nchini Urusi, wamesema leo kwamba wamepata miili ya watu wote 22 waliokuwa katika helikopta iliyoanguka katika eneo la mashariki mwa Urusi.
Helikopta hiyo iliyokuwa imewabeba watalii 19 na wafanyakazi watatu ilianguka siku ya Jumamosi na maafisa wa uokoaji wakapata mabaki yake siku iliyofuata.