Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi nchini China kuanzia Septemba 2 hadi 6, 2024 kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation-FOCAC) utakaofanyika jijini Beijing.
Wakati wa ziara hiyo, Rais Samia atakutana na mwenyeji wake Rais wa China, Xi Jinping kwa mazungumzo yanayolenga kuimarisha uhusiano mzuri na wa kihistoria kati ya Tanzania na China ulioasisiwa miaka 60 iliyopita.
Marais hao wawili pamoja na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema watashiriki na kushuhudia uwekaji saini wa Hati za Makubaliano ya Uboreshaji wa Reli ya Tazara.
Pamoja na mambo mengine, miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kupewa kipaumbele kwenye mkutano wa FOCAC ni uendelezaji wa miundombinu, kukuza uwekezaji, uendelezaji wa viwanda, kilimo cha kisasa na amani na usalama.
Pia Rais Samia anatarajia kuwa miongoni mwa wakuu wa nchi watakaohutubia ufunguzi wa mkutano wa FOCAC, akizungumza kwa niaba ya Kanda ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Agosti 31, 2024 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo alipozungumza na waandishi wa habari, ilisema Rais Samia ataenda China kusaka fedha za miradi mine.
“Tanzania inatarajia kuwasilisha miradi mbalimbali ikiwemo mipya na ile ambayo haikuweza kutelezwa kwenye mpango uliopita wa FOCAC kwa sababu mbalimbali, ili iweze kupatiwa fedha za mkopo nafuu na msaada na kutekelezwa chini ya mpango kazi wa FOCAC mwaka 2025-2027,” alisema Balozi Kombo.
Miradi minne itakayowasilishwa na Rais Samia kwenye mkutano huo ni ujenzi wa mtandao wa mawasiliano vijijini awamu ya pili, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400 awamu ya pili na ya tatu, ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi (Veta) awamu ya pili na ujenzi wa barabara za Zanzibar zenye urefu wa kilomita 277.