Sh14 bilioni kujenga majengo manne chuo kikuu Mkwawa

Iringa. Kilio cha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Elimu Mkwawa (MUCE) cha kupanga mitaani kimeanza kufutwa, baada ya mkataba wa ujenzi wa majengo manne ikiwamo wa hosteli wenye thamani ya zaidi ya Sh14.8 bilioni kusainiwa.

Mbali na hosteli, MUCE na kampuni ya ujenzi wamesaini mkataba wa ujenzi wa majengo kwa ajili ya maabara ya fizikia, sayansi na elimu kupitia mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi.

Mwaka 2023 wakati wa mahafari chuoni hapo, miongoni mwa kilio walichowasilisha wanafunzi ni uhaba wa hosteli, jambo linalowafanya wapange mitaani.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye akizungumza leo Jumatatu Septemba 2, 2024 chuoni hapo, amesema jengo la hosteli litapunguza idadi ya wanafunzi wanaopanga mitaani.

Anangisye amesema kupitia mradi huo, majengo ya kisasa yatakayojengwa na yatapunguza uhaba uliokuwepo awali.

“Nimuombe mkandarasi afanye kazi kwa uadilifu na sisi tumepata mkandarasi mzawa, kwa hiyo majengo haya yakamilike kwa wakati na hata ikiwezeka yakamilike kabla,” amesema Profesa Anangisye.

Rasi wa MUCE, Deusdedit Rwehumbiza amesema kati ya wanafunzi zaidi ya 6,000 chuoni hapo, walio hostel ni zaidi ya 1,000 tu jambo ambalo linaongeza umuhimu wa majengo hayo.

Mkandarasi anayejenga majengo hayo, Dickson Mwipopo amesema ana uhakika wa kuanza kazi mapema na itakamilika kwa wakati, ili kuongeza imani kwa wakandarasi wa ndani.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Septemba 3, 2024, baada ya kusaini mkataba huo, Mwaipopo amesema umahiri wa makandarasi wa ndani kufanya kazi hiyo kutasaidia waendelee kupata kazi nyingi zaidi.

“Walau wakandarasi wa ndani tumeanza kuaminiwa, nitafanya kazi hii kwa weledi na niseme tu kwa wakandarasi wenzangu, tufanye kazi kwa uaminifu ili tuaminiwe, tusiache kazi kwa wakandarasi wa nje pekee, tujitokeze kuomba,” amesema Mwipopo.

Related Posts