WAZIRI wa Madini Mh. Anthony Mavunde amesema Tanzania inakaribisha wawekezaji wote wa madini mkakati na kuweka msisitizo kwamba uongezaji thamani wa madin hayo mkakati lazima ufanyike Tanzania.
Mavunde ameyasema hayo leo Bali,Indonesia wakati wa majadiliano juu ya manufaa ya Madini Mkakati katika kukuza uchumi wa nchi wazalishaji ikiwa ni sehemu ya mkutano wa jukwaa la INDONESIA AFRIKA.
Waziri Mavunde ameonesha dhamira njema na mazingira mazuri yaliyowekwa na serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia S. Hassan kuvutia uwekezaji nchini na hivyo kuwakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika uchimbaji wa madini mkakati ambayo yana mahitaji makubwa duniani na Tanzania imebarikiwa nayo.
Waziri Mavunde alisisitiza kuwa kwasasa ni sharti la lazima kwamba madini mkakati hayo yaongezwe thamani nchini ili kuvutia viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo betri ya magari ya umeme.