Tarime. Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara inakabiliwa na uhaba wa vituo vya kutolea huduma ya dawa kinga kwa ajili ya ugonjwa wa Ukimwi (PREP na PEP), hali inayoelezwa kuwa ni moja ya changamoto katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya ugonjwa huo.
Akizungumza leo Jumatatu Septemba 2, 2024 mjini Tarime kwenye kikao baina wataalamu wa afya, madiwani, wadau na watendaji katika halmashauri hiyo, Ofisa Miradi kutoka Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Anold Masawe amesema halmashauri hiyo ina vituo vinne vinavyotoa huduma hiyo.
Amesema kwa mujibu wa miongoni na sera za Wizara ya Afya, dawa hizo zinapaswa kutolewa kuanzia ngazi ya kituo cha afya na kwamba licha ya halmashauri hiyo kuwa na vituo vya afya 11 na hospitali moja, ni vituo vinne pekee ndivyo vinavyotoa huduma hiyo, huku changamoto ikielezwa kuwa ni kutokuwa na watumishi wenye mafunzo juu ya namna ya utoaji wa dawa hizo.
Amesema kutokana na hali hiyo, ni vema halmashauri hiyo kupitia wataalamu na baraza la madiwani ikaanza kutoa kipaumbele kwa kutenga bajeti itakayowezesha vituo hivyo vya afya kuanza kutoa huduma hizo, ili iwe rahisi kupatikana pale zinapohitajika.
“Huduma hizi ni moja ya huduma zinazohitajika sana na vijana, hivyo kupatikana kwake kwa urahisi kutawezesha vijana hawa na walengwa wengine kuzipata kwa urahisi pale inapotakiwa na kuzitumia kwa wakati ili kuepuka maambukizi ambayo yangeweza kuzuilika,” amesema Masawe.
Amesema mazingira rafiki ya utoaji huduma za afya ni moja ya kivutio kwa vijana wengi zaidi kujitokeza kupata huduma hasa za afya ya uzazi na VVU katika vituo vya kutolea huduma za afya hivyo ni wajibu wa wahusika kuhakikisha wanatenga bajeti ya kutosha ili vijana wengi zaidi wapate huduma hizo.
Masawe amesema kupitia mradi wa Youth Care unaotekelezwa na shirika lake kwa vijana wenye umri kati ya miaka 10- 24 katika kata tisa wilayani Tarime wamebaini ukosefu wa huduma za dawa kinga ni moja ya changamoto inayowakabili viijana katika eneo hilo.
Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto katika halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Beatrice Luomba amesema halmashauri hiyo imekuwa ikitenga bajeti kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa ujumla kulingana na upatikanaji wa fedha.
Amesema kutokana na umuhimu na unyeti wa masuala ya afya kwa ujumla ushirikiano kati ya wadau na serikali, ni muhimu ili kufikia malengo ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma kinga kwa ukaribu na mazingira rafiki.
“Jamii, wadau na Serikali tunatakiwa kuungana kutoa elimu kwa vijana, ili wawe na uelewa wa kutosha juu ya mila zilizopitwa na wakati na namna ambavyo zinachangia kuathiri afya na ustawi wa vijana,” amesema
Baadhi ya vijana wamesema mazingira yasiyokuwa rafiki kwao ni moja ya sababu zinazopelekea vijana wengi wasiwe na utaratibu wa kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma kupata huduma hasa za afya ya uzazi na Ukimwi.
Linah Omary amesema kuwa kundi la vijana bado linakutana na changamoto mbalimbali, hivyo Serikali haina budi kushirikiana na wadaui ili kuweka mazingira rafiki, ili wapate huduma wakiwa peke yao.
Diwani wa Nyamwaga, Mwita Magige amesema kundi la vijana ni muhimu na kwamba amebani upo umuhimu wa wao madiwani kutoa kipaumbele na kuweka mikakati sahihi ya kuwasaidia.