Tasac yatoa tahadhari watumiaji wa usafiri, shughuli majini

Dar es Salaam. Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) limewataka wadau wote wa usafiri kwa njia ya maji na wanaofanya shughuli za kiuchumi baharini na kwenye maziwa, kuendelea kuchukua tahadhari, ikiwemo kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa.

Rai hiyo imetolewa wakati ambao Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kuwapo kwa uwezekano wa kutokea upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa siku tatu mfululizo kuanzia jana Jumapili, Septemba mosi hadi 3, 2024.

Kwa mujibu wa taarifa ya TMA, baadhi ya maeneo yanayotajwa kuathiriwa na upepo huo ni Ukanda wa Pwani ya Kusini mwa Bahari ya Hindi katika mikoa ya Lindi na Mtwara, baadhi ya maeneo ya kusini mwa Ziwa Tanganyika mikoa ya Rukwa na Katavi.

Pia, upepo huo unatajwa kuwa na uwezekano wa kuathiri baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini mwa Bahari ya Hindi katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikijumuisha Visiwa vya Mafia), pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba.

Taarifa hiyo imesema athari zinazoweza kujitokeza ni kuathirika na kughairishwa kwa baadhi ya shughuli za baharini na kuharibika kwa miundombinu ya bahari.

“Hivyo, Tasac inawataarifu wadau wote wa usafiri kwa njia ya maji na wanaofanya shughuli za kiuchumi baharini na kwenye maziwa, ikiwemo wavuvi na wasafirishaji kuendelea kuchukua tahadhari, ikiwemo kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa,” imeeleza taarifa ya Tasac.

Pia, imewataka wadau wote wa usafiri kwa njia ya maji kuchukua tahadhari ya hali ya juu hasa kwa wasafirishaji wa vyombo vikubwa na wadau wote wanaofanya shughuli za kiuchumi baharini na kwenye maziwa, ikiwemo wavuvi na wasafirishaji wadogo.

“Tahadhari ziendelee kuchukuliwa mpaka TMA itakapotangaza hali ya hewa kuwa shwari, ili kuzuia ajali zitakazohatarisha maisha ya wavuvi na wasafiri,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Related Posts