Umri ajira za Tawa zawavuruga wabunge, wataka uondolewe

Dodoma. Kigezo cha umri usiozidi miaka 25 kwenye tangazo la ajira la Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa), limeombewa jambo la dharura bungeni na wabunge ambao wameishauri Serikali waondoe kigezo cha umri.

Jambo hilo limeletwa bungeni leo Jumatatu Septemba 2, 2024 na mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ng’wasi Kamani akitumia kanuni ya 54 kulitaka Bunge lisimamishe shughuli zake kujadili jambo hilo la dharura.

“Kigezo muhimu kwa waombaji wote hawa 351 ilikuwa ni kwamba wanatakiwa wawe kuwa na umri usiozidi miaka 25. Yaani awe na umri wa miaka 25 kushuka chini.

“Na vigezo vingine, kwa mfano kwenye udereva anatakiwa awe na vyeti vyote vya Veta na lesseni, lakini awe na uzoefu wa mwaka mmoja wa udereva, kwenye hivi vingine wanatakiwa kuwa na vyeti vingine kama vile cheti, diploma au shahada,” amesema.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliruhusu kusimamisha shughuli za Bunge na kujadili hoja hiyo kwa lengo wabunge waishauri Serikali kuhusu vigezo vya ajira wanavyotumia.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema Serikali imepokea maoni ya wabunge na watafanyia kazi.

Mbunge Kamani amelieleza Bunge kuwa vijana waliomaliza shule wasihukumiwe kwa kigezo cha umri, bali wahukumiwe kwa kigezo cha uwezo.

“Hawa watu tusiwahukumu kwa vigezo kama umri, tuwahukumu kwa uwezo kama wamemaliza na wako mtaani hawana kazi, kwa nini tuwahukumu kwa umri.

“Kila mwaka wanaohitimu vyuo ni kuanzia wahitimu 100,000 hadi 300,000 na nafasi za kazi ni chache. Mwanafunzi anapomaliza chuo umri hausimami, tuongeze walau ufike miaka 30,” amesema.

Wabunge wataka ifike mika 30

Baada ya kutoa hoja yake, wabunge mbalimbali wameichangia ambapo Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara amesema kusema mwenye umri wa miaka 30 hawezi kuruka vihunzi siyo sahihi kwa kuwa hata hao wenye umri wa miaka 25 wako ambao hawawezi kuruka vihunzi.

“Kuna watu wana umri wa miaka 25 hawawezi kuruka vihunzi, lakini wenye umri mkubwa wanaweza. Watu wengine ni watu wa mazoezi. Wao wangetoa bila kuweka kigezo cha umri, watu waombe kama ni suala la mazoezi mtu ashindwe huko.

“Ilivyokaa unaweka kizuizi mtu hawezi kuomba ile kazi na hana ajira nyingine na yuko mtaani, lakini umeweka umri kumbe angeweza kushinda. Suala la umri liondolewe ili isionekane ni na ajira ya kundi fulani,” amesema Waitara.

Mbunge wa Viti Maalumu, Nusrat Hanje ameshauri Serikali iongezwe hadi umri wa miaka 30, watu wakashindwe wenyewe huko.

“Tunategemea mkitangaza ajira za Serikali basi msipuguze upana wa goli kwa kuweka kigezo cha umri, iache goli lilivyo vijana wote waende wakapambane ili kupunguza malalamiko,” amesema.

Mbunge wa Arumeru Magharibi (CCM), Noah Mollel amesema Serikali iongeza umri wa hadi miaka 30 wanapotangaza nafasi za ajira.

 “Mimi nadhani kigezi hiki bado hakiko sawa na hakitakuwa sawa kwa sababu Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na hilo Jeshi Usu, mafunzo ni tofauti hayawezi kuwa makali kuzidi Jeshi la Wananchi wa Tanzania,” amesema.

Mollel amesema suala la umri miaka 30 kwa majeshi haya ya Usu, suala la afya likajulikane kwenye kupimwa na kuangaliwa kwao. Kuweka miaka 25 ni kuzuia vijana wengi kupata ajira.

Amesema Serikali iwe inajiridhisha inapotoa ajira ni Watanzania wangapi umri umepita, pia ajira zote ziangaliwe hiki kigezo cha umri.

Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda amesema kuweka umri wa miaka 25 kutawaweka vijana wengi nje, kwa kuwa ni muda mrefu ajira hazijatoka.

“Jeshi Usu linahitaji tu ukakamavu, tusogeze hadi umri wa miaka 30 na isiishie tu kwenye mambo ya Tanapa na tufanye na kwenye ajira nyingine, vinginevyo watoto wetu waliomaliza vyuo miaka sita iliyopita wataendelea kuachwa kwenye mfumo wakati wamesoma, suala la umri liongezwe kwenye ajira zote,” amesema.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson baada ya kuliona tangazo hilo kutoka kwa mtoa hoja, aliuliza:“Hiki kigezo cha umri wa miaka 25 kilikuwa na sababu zozote?”

Waziri Simbachawene  alijibu swali hilo kwa kusema, “Tawa ni Jeshi Usu na vyombo hivi vyenye aina ya mafunzo ya kijeshi, umri ni kigezo muhimu sana katika kupima ukakamavu na uwezo wa kupokea mafunzo ya kijeshi.

“Tawa kwa uzoefu walionao na mahitaji ya nguvu kazi wanayotaka wanadhani umri wa miaka isiyozidi 25 unaweza kumuwezesha huyu mwanajeshi wanayemuandaa aende kupambana na mazingira kwenye utekelezaji wa majukumu yake.”

Hata hivyo, Spika Tulia amehoji:“Umesema hili ni Jeshi Usu kuna tofauti yeyote kati ya Jeshi Usu na Jeshi la Watanzania, liko sawa, ama hakuna tofauti ya Jeshi Usu na hilo?”

Simbachawene amejibu swali hilo kwamba Jeshi Usu na majeshi mengine yanatofautiana, isipokuwa kwa maana ya tangazo la Tawa linawahitaji wa kada za kawaida, lakini wakiwa na mafunzo ya ujeshi ndani yake kutokana na kazi wanazokwenda kuzifanya.

Spika Tulia amelieleza Bunge jambo hilo si mara ya kwanza kujitokeza bungeni kuhusu vigezo vya ajira vinavyotolewa, kwenye maeneo ya jeshi na Jeshi Usu pia yamewahi kujitokeza huko nyuma na kwa makubaliano.

“Nakumbuka tulisema kwa upande wa Jeshi kwa sababu wana vigezo vya ziada waache hivvyo, na hizi taasisi nyingine ziangalie ambazo hazihitaji hiki kigezo cha watu kupitia mafunzo hayo.

“Kwa sababu linakwenda na kurudi ni vema Serikali ipate ushauri wa Bunge leo. Ili ushauri utakaotolewa na wabunge muuchukue nyinyi upande wa Serikali, kwa sababu nilikuwa napitia hilo tangazo la Tawa,” amesema.

Related Posts