Dar es Salaam. Wanasema samaki mkunje angali mbichi, hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya wanafunzi wa sekondari nchini kupatiwa elimu ya fedha itakayowasaidia kuanzia sasa na hata watakapokuwa watu wazima.
Hatua hiyo inatokana na changamoto iliyopo ya Watanzania wengi kukosa elimu ya fedha, hususani mikopo hivyo kujikuta wakiangukia kwenye mikopo umiza yenye riba kubwa maarufu kama kausha damu.
Kutokana na hilo, Chama cha Akiba na Mikopo cha Hazina Saccos kilichopo chini ya Wizara ya Fedha kimejitosa kutoa elimu ya fedha kuanzia shuleni, ikihusisha mikopo na akiba itakayowasaidia kama chanzo cha mtaji.
Akizungumza leo Jumatatu Septemba 2, 2024 Mtendaji Mkuu wa Hazina Saccos, Festo Mwaipaja amesema elimu hiyo itasaidia kupambana na ujinga pamoja na umaskini.
“Watu kila kona wanalia juu ya mikopo riba, wanakopa mahali ambapo hapastahili, wanafunzi wenyewe wanalia wakifika vyuoni wanaumiza vichwa namna ya kupata mitaji, tumeamua kuja kuanza nao ili kuwasaidia,” amesema Mwaipaja katika Shule ya Sekondari Kisutu wakati wa shindano la kitaifa la elimu ya fedha lililozikutanisha shule 10 za Mkoa wa Dar es Salaam.
Amesema elimu ya fedha itawasaidia wao wajiwekee akiba kupitia vyama vya akiba na mikopo, hadi pale watakapomaliza vyuo watakua na elimu na vyanzo sahihi vya mitaji.
“Hii itasaidia kupambana na changamoto ya umaskini iliyopo kwenye jamii yetu kwa sababu ya ufahamu. Tunaamini wanafunzi ni nyenzo muhimu ya kufikisha elimu kwa kuwa watakua nayo,” amesema.
Amesema wanafunzi watakapokuwa wakubwa watajua namna ya usimamizi wa fedha, namna ya upatikanaji wa mitaji ya gharama nafuu na namna ya upatikanaji wa fedha ya uwekezaji.
“Elimu hii itawasaidia kuelewa nguvu ya Saccos kwenye uchumi, mfano nchi jirani ya Kenya wenzetu Saccos zao zinamiliki matrilioni ya pesa,” amebainisha.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Klabu za Hazina Saccos Tanzania, Daniel Mwakyambiki amesema lengo la mashindano hayo ni kuwaandaa watoto kwa kuwapa elimu ya fedha kwa ujumla.
“Sasa hivi watoto tunawaona wanacheza Vicoba hadi shuleni na wana michezo yao ya pesa, hivyo tumeona tuwasaidie kuwaandaa rasmi kupitia klabu za elimu fedha shuleni,” amesema.
Amesema wameanza na shule za sekondari Tambaza, Mzimuni, Kisutu, Migombani, Kinyerezi, Minazi Mirefu, Tuliani, Kigogo, Kambangwa na Makumbusho kisha kwenda jijini Dodoma na Tanzania kwa ujumla.
Ameongeza kuwa wakiwa watu wazima watasaidia Taifa kwa kuwa wana uwezo wa kutunza akiba na wanafahamu nidhamu ya fedha.
Mmoja ya wanafunzi wa kidato cha sita, Paulo Sibora kutoka sekondari ya Tambaza amesema ni jambo zuri kwa wanafunzi kupata elimu hiyo, itakayowasaidia katika masuala ya akiba na mikopo na matumizi ya fedha kwa ujumla.
Naye Dorcas Tarimo, mwanafunzi wa kidato cha sita kutoka sekondari ya Kisutu amesema elimu hiyo inapaswa kupelekwa katika jamii, ili watu wapate uelewa wa fedha.
“Elimu ya fedha kwa mwanafunzi ina manufaa na mikopo inayotolewa na idara ya hazina inamsaidia hata akimaliza chuo, kumpa mtaji kabla ya kupata ajira,” amesema.
Aidha, elimu hiyo imetajwa kuwasaidia wanafunzi kudhibiti madeni, mikopo na riba, bima, mikakati ya kustaafu, kukuza utamaduni wa kuweka akiba, ushauri wa kifedha kusimamia vizuri kufikia malengo yao, kuepuka matumizi ya fedha yasiyo ya lazima ili kuweka akiba.