Watu 48 wauawa Gaza, zoezi la chanjo ya Polio laendelea – DW – 02.09.2024

Katika kipindi cha muda wa saa 24 zilizopita, mashambulizi ya Israel huko Gaza yamesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 48 kufuatia mapigano na kundi la Hamas na hivyo kufanya idadi jumla ya waliouawa huko Gaza tangu kuanza kwa mzozo huo Oktoba 7, kufikia watu 40,786. Hii ikiwa ni kulingana na wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas.

Hayo yanaripotiwa wakati Israel na Hamas walikubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa siku tatu kuanzia jana Septemba mosi, ili kupisha mchakato wa chanjo ya Polio kwa watoto 640,000 wa Gaza  wenye umri chini ya miaka 10. Hata hivyo hakuna ukiukaji wowote wa makubaliano hayo ulioripotiwa karibu na vituo vya kutolea chanjo.

Afisa wa afya akitoa chanjo ya Polio kwa mtoto wa Gaza
Afisa wa afya akitoa chanjo ya Polio kwa mtoto wa GazaPicha: Hani Alshaer/Anadolu/picture alliance

Lakini Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, limerejelea wito wake hivi leo wa kuwepo mara moja usitishaji mapigano ili kuhakikisha kampeni hiyo ya chanjo ya polio kwa watoto inafanikiwa kwa usalama. Mwenyekiti wa Kamati huru ya usimamizi na ushauri kwa mpango wa dharura wa afya (IOAC) Profesa Walid Ammar amesema:

“Umoja wa Mataifa uliomba kusitishwa kwa mapigano ili kuwezesha kampeni ya chanjo ya polio huko Gaza, na kuna aina fulani ya mwitikio mdogo. Mashirika ya WHO, UNICEF na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa yanajaribu kukabiliana na hali hii ili kuendelea na zoezi la chanjo.”

Soma pia: Israel kusitisha mapigano Gaza kwa siku 3 kupisha chanjo ya Polio

Maafisa wa Afya wamesema katika siku ya kwanza ya zoezi hilo hapo jana, zaidi ya watoto 80,000 wamepatiwa chanjo hiyo katikati mwa Gaza.

Mahakama ya wafanyakazi ya Israel yaamuru kusitishwa kwa mgomo

Mgomo huo uliitishwa na chama kikuu cha wafanyakazi na kukwamnisha shughuli Israel
Mgomo huo uliitishwa na chama kikuu cha wafanyakazi na kukwamnisha shughuli IsraelPicha: Gil Cohen-Magen/AFP

Mgomo huo uliitishwa na chama kikuu cha wafanyakazi nchini humo ili kuishinikiza serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuunga mkono makubaliano ya usitishwaji mapigano huko Gaza ambayo pia yatafanikisha kuachiliwa kwa mateka waliosalia mikononi mwa kundi la Hamas. Mahakama hiyo imesema mgomo huo uliokwamisha shughuli mbalimbali za kijamii umechochewa kisiasa.

Soma pia: Waisraeli waanzisha mgomo wakishinikiza kuachiliwa kwa mateka

Uamuzi huo wa mahakama unakuja baada ya Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich ambaye pia ni kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia anayepinga usitishaji vita huko Gaza, kuitaka mahakama hiyo kuchukua hatua ya kupiga marufuku mgomo huo akisema haukuitishwa kwa sababu za kiuchumi. Ndugu za mateka wamekuwa wakiushutumu utawala wa Netanyahu kwa kutolitilia maanani suala la kurejeshwa kwa mateka.

Kwa upande wake Rais wa Marekani Joe Biden amesema hii leo kuwa makubaliano ya kusitisha vita Gaza na kuwarejesha mateka wa Israel waliosalia yanakaribia kufikiwa lakini akasema kwamba utawala wa Netanyahu hauchukui hatua zaidi zinazohitajika ili kufanikisha mpango huo.

Vyanzo: (DPAE, AFP, Reuters, AP)

 

Related Posts