Zimamoto wataja chanzo moto ulioteketeza bweni

Mbeya. Siku chache baada ya bweni la wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nsenga, jijini Mbeya kuteketea kwa moto, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limesema chanzo ni betri ya sola iliyokuwa ikiwaka na kusababisha ushike kwenye bweni lililoteketea.

Agosti 26, 2024 wanafunzi wa kike 107 walinusurika kifo baada ya bweni lao kuteketea kwa moto.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Septemba 2, 2024, Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoani Mbeya, Malumbo Ngata amesema uchunguzi umebaini chanzo cha moto huo ni hitilafu katika betri ya sola iliyokuwa ikitumika kwa ajili ya nishati ya mwanga kuungua.

Amesema kutokana na tukio hilo, ameshauri wananchi na taasisi zote zinazotumia nishati yoyote ya umeme kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kubaini tatizo na kulitolea taarifa kwa mamlaka.

Mrakibu huyo amesema kutokana na hali ya hewa Mbeya kuwa na upepo mwingi kipindi hiki cha kiangazi, wananchi wanatakiwa kuwa makini na usafishaji wa mashamba kwa njia ya moto.

“Wananchi waepukane na uchomaji moto bila kuchukua tahadhari kutokana na kiangazi hiki na upepo uliopo. Kipindi hiki majanga huwa ni mengi, Zimamoto tumejipanga kukabiliana na matukio ya aina hii na wakuu wote wa vituo wilaya wana maelekezo,” amesema kamanda huyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Nsenga, Noel Mwanshusa amesema wanafunzi wanane waliopatwa na mshtuko wakati wa tukio hilo wanaendelea vizuri na wamesharejea darasani kuendelea na mitihani.

Kuhusu ujenzi wa bweni na uzio, amesema kwa sasa hawezi kulifafanua kutokana na jambo hilo kuwa katika ngazi za juu kwa uchunguzi na hatua zaidi.

Related Posts