Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimepeleka tuhuma za Mkuu wa Mkoa wa Tabora (RC), Paul Chacha kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), kikitaka imchunguze kutokana na madai ya kuhusika na mauaji ya watu alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaliua.
Kwa mujibu wa chama hicho, Chacha alihusika na mauaji hayo mwaka 2021 katika Wilaya ya Kaliua wakati wa mpango wa uhamishaji wa wananchi kutoka kwenye vijiji 11 vilivyokuwa na migogoro ya ardhi.
Sambamba na hatua hiyo, ACT-Wazalendo pia imepeleka tuhuma za kiongozi huyo kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na kuzisihi mamlaka za uteuzi ziangalie uhalali wa Chacha kuendelea kushika wadhifa alionao sasa.
Hata hivyo, Chacha amekanusha tuhuma hizo, akisema wanaomtuhumu wanatafuta umaarufu wa kisiasa na kwamba aliyetuhumu anapaswa kuweka wazi walipo waliouawa.
“Muhimu atusaidie (aliyetuhumu) ili tupambane na hao wadhalimu, kama kuna mauaji huo ni uharamia kwanini hasa tunyamazie, kama kuna taarifa hiyo na watu wanajulikana tuwachukulie hatua tujue familia gani? watu wameuawa na wamezikwa wapi? Na kina nani hao ili aliyefanya hayo achukuliwe hatua,” amesema Chacha.
Kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria, Chacha akizungumza na Mwananchi amesema mtuhumu anapaswa kuweka bayana taarifa za mauaji hayo ili muhusika achukuliwe hatua.
“Jambo hili si dogo kuongea kwenye vyombo vya habari na tukakaa kimya nikasema huu ni udhalimu basi huyu mtu atusaidie inawezekanaje watu wanauawa na kubakwa ni wapi. Sina taarifa hiyo Serikali haiwezi kuona jambo kubwa kama hilo alafu ikanyamaza,” amesema.
Tuhuma dhidi ya Chacha, zimetolewa jijini Dar es Salaam leo Jumanne Septemba 3, 2024 na Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria wa ACT-Wazalendo, Maharagande Mbarala katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Katika mkutano wake huo, amesema ni vema Bunge la Tanzania likaunda kamati kwenda kuchunguza matukio hayo.
“Tayari tumeshapeleka malalamiko, mashtaka na madai mbele ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ili waweze kuchukua hatua zao kwa mujibu wa taratibu na sheria za taasisi hizo, ndani ya taarifa hiyo tumeambatanisha na orodha ya watu wote waliouliwa katika kadhia hii.
“Tumepeleka ushahidi wa ubakaji uliofanywa na migambo pamoja na orodha ya watu walioondolewa katika eneo hilo na mali zilizoporwa na kuchukuliwa na operesheni hiyo,” amesema Mbarala
Mbarala ambaye ni Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu wa ACT-Wazalendo, amesema haiwezekani kiongozi huyo aliyehusika na matukio hayo baadaye anaenda katika nyumba za ibada kujitangaza kwa usafi.
“Unafanya matendo ya kiovu halafu baadaye unaenda kuwatisha watu kwamba wewe ni msafi na unakwenda katika nyumba takatifu za ibada unazungumza maneno ambayo hayakubaliki,” amesema Mbarala.
“Malalamiko yetu hatujapeleka THBUB tu,tumenakilisha kwa Waziri wa Katiba na Sheria na Bunge la Tanzania kuona hatua gani za haraka zinachukuliwa kwa sababu matatizo yanawagusa moja kwa moja wananchi,” amesema.