Chuo cha mkwawa kuongeza majengo manne ikiwemo hosteli

Wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) wameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuanzisha mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) wenye thamani ya shilingi bilioni 14.8. Mradi huu unatarajiwa kutatua changamoto za ubakaji na wizi kwa wanafunzi wanaoishi nje ya hosteli.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi, Makamu wa Rais wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa, Remisha Gastoni Milazi, alisema kuwa mradi huu utasaidia kupunguza changamoto za ukatili, ulinzi duni, na gharama kubwa za malazi, ambazo zimekuwa zikihitaji wanafunzi kuishi mume na mke, hali inayosababisha mimba zisizotarajiwa na kushindwa kwa baadhi ya wasichana kufikia malengo yao.

 

Rais wa chuo hicho, Steaven Thomas Mgala, alisema mradi huo utaongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kwa sababu wengi wao wanaishi nje ya hosteli, hali inayosababisha baadhi yao kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao.

Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa, Prof. William Anangisye, ambaye alikuwa mgeni rasim wa hafla hiyo ya utiaji saini kati ya mkandarasi wa Chuo Kikuu Mkwawa na Mkandarasi Mzawa wa Kampuni ya Dimetoclasa Real Hope Limited alisema mradi huo utaimarisha uvumbuzi, maendeleo ya kiuchumi, na umuhimu wa soko la ajira kwa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya ufundishaji na utafiti.

 

Alisisitiza kuwa wakandarasi na mshauri mwelekezi wanapaswa kuhakikisha ujenzi unafanywa kwa uzuri na kwa kufuata sheria zote, na alitaka mradi kukamilika ndani ya miezi 15, au kabla, kwa kufanya kazi usiku na mchana.

 

Rasi wa Chuo hicho, Profesa Deusdedit Rwehumbiza, amefafanua kwamba majengo haya manne yatakuwa na hosteli ya wanafunzi, maabara za fizikia, sayansi, media, na elimu maalumu.

Amesema mradi huu utatatua changamoto kubwa ya upungufu wa hosteli, ambapo sasa wanafunzi wapatao 6,200 wanapata malazi ya hosteli elfu moja na mia moja tu.

 

Dickson Mwipopo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Dimetoclasa Real Hope Limited and Mponera Construction, alisisitiza umuhimu wa kutoa kazi kwa wazawa kwa asilimia 100 ili kuongeza uchumi wa taifa na kuunda fursa za ajira kwa vijana.

Related Posts