Hatua muhimu Shilingi ikiporomoka dhidi ya Dola

Dar es Salaam. Shilingi ya Tanzania imeshuka thamani dhidi ya Dola ya Marekani kwa asilimia 11.4 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita, hali inayowastua waagizaji wa bidhaa, sanjari na hofu ya ongezeko la gharama za utekelezaji wa baadhi ya miradi mikubwa.

Kushuka kwa Shilingi dhidi ya Dola kulitokana na kuadimika kwa sarafu hiyo ya Marekani baada ya Benki Kuu ya taifa hilo namba moja kiuchumi duniani (Federal Reserve) kuongeza viwango vya riba kufikia kiwango cha juu cha miaka 23 cha asilimia 5.25 hadi 5.5, Julai 2023.

Uamuzi huo ulipunguza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa Dola ambayo aghalabu hutumika katika miamala ya kimataifa.

Kabla ya changamoto hiyo viwango vya Benki kuu ya Tanzania (BoT),  vilikuwa Dola moja ilibadilishwa kwa wastani wa Sh2,365.38, lakini kufikia jana Septemba 03, 2024, kiwango hicho kilipanda hadi Sh2,635.92.

Baadhi ya benki za kibiashara zinatoa viwango vya hadi Sh2,738 kwa Dola, huku katika soko la magendo kiwango kikiwa kikubwa zaidi hadi kufikia zaidi ya Sh3,000 kwa Dola moja.

Akizungumza na gazeti dada la The Citizen, mchambuzi wa masoko ya fedha, Bernard Mumwi alibainisha kuwa mwenendo huu unaonyesha kuwa huenda bei ya Dola moja kwa Shilingi ikazidi kuongezeka zaidi hadi mwishoni mwa mwaka huu.

“Gharama ya juu ya Dola nchini Tanzania inatokana na kudorora kwa Shilingi yetu, ndiyo sababu tumeshuhudia taasisi kama BoT imeanzisha sera za kubana uchumi na kudhibiti bei. Juhudi nyingine ni pamoja na kufungua hatifungani za hazina zenye riba kubwa ili kuhamasisha akiba na kupunguza fedha kutoka kwenye uchumi,” alisema.

Mumwi alisisitiza umuhimu wa kufuatilia viashiria vya kiuchumi vya Marekani ambavyo vinaweza kusababisha kubana zaidi uchumi. “Kama Marekani inabana uchumi wake, tunapaswa kuendelea na juhudi zetu za kuongeza thamani ya shilingi yetu.”

Hata hivyo, hivi sasa kuna uvumi katika masoko ya Marekani unaoelezea kuwa huenda Kamati ya Soko Huru (FOMC) ikapunguza viwango vya riba katika mkutano wake wa Septemba 18, 2024.

Vyombo vya habari vya Marekani, likiwamo Jarida la Forbes, vinaonyesha ushahidi wa nguvu unaounga mkono mtazamo huu, kulingana na muhtasari wa FOMC na kauli za hadharani.

Kulingana na tovuti ya Forbes, Mwenyekiti wa Benki Kuu ya Marekani, Jerome Powell aliashiria kwa nguvu kwamba upunguzaji unakuja wakati wa hotuba yake katika Mkutano wa Uchumi wa Jackson Hole.

“Muda umefika kwa sera kurekebishwa. Mwelekeo wa safari uko wazi lakini muda na kiwango cha kupunguza viwango vya riba itategemea data zitakazopatikana, tathimini ya  mambo na vihatarishi,” Powell alinukuliwa na Forbes.

Iwapo Benki Kuu ya Marekani itapunguza viwango vya riba, itaongeza upatikanaji wa Dola duniani, jambo linaloweza kushusha bei yake na kunufaisha uchumi wa mataifa tofauti ikiwemo Tanzania.

Hata hivyo, ukubwa wa athari za hatua hiyo tarajiwa bado ni za kusubiri, lakini Serikali ya Tanzania huenda itahitaji kuendelea na juhudi zake za kudhibiti athari za kudorora kwa Dola dhidi ya Shilingi.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya fedha, Christopher Makombe alihusisha kupanda kwa bei ya Dola nchini Tanzania na sababu za kuongezeka kwa mahitaji yake ulimwenguni.

“Kumekuwa na mahitaji makubwa ya Dola nchini, hasa kutokana na miradi mingi kulipwa kwa pesa hiyo. Ukuaji wa biashara na uchumi pia unachangia mahitaji haya na kusababisha kushinda kwa ugavi,” alisema.

Makombe alipendekeza kuwa kuongeza ukwasi wa Dola, hasa kwa kukuza mauzo ya nje ni muhimu kwa kushughulikia uhaba wake ambao una athiri moja kwa moja thamani ya Shilingi.

“Ili kudhibiti uhaba huu, tunahitaji kutafuta njia za kuongeza ukwasi wa Dola, ikiwa ni pamoja na kuboresha mauzo yetu ya nje ili usambazaji wa Dola nchini ukidhi mahitaji yetu,” alisema.

Msimamo wa Sera ya Fedha ya Tanzania

Kwa upande wa ndani, Benki Kuu ya Tanzania ilirekebisha Kiwango cha Riba cha Benki Kuu (CBR) hadi asilimia  sita kutoka asilimia 5.5 iliyokuwapo Aprili 2024, ili kudhibiti shinikizo la mfumuko wa bei linalotokana na maendeleo ya kiuchumi ya kimataifa.

Uamuzi huu ulidumishwa kwa robo inayoisha Septemba 2024, kutokana na kuwapo kwa usimamizi mzuri wa matarajio ya kiuchumi katika robo iliyopita.

Hatua nyingine muhimu ilielezwa katika hotuba ya bajeti ya Juni 13, 2024, ambapo Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alitoa agizo la kudhibiti matumizi makubwa ya Dola ya Marekani ndani ya nchi.

Aliagiza miamala yote ifanyike na kutangazwa kwa Shilingi ya Tanzania kuendana na mfumo wa kisheria wa nchi na kukuza utulivu wa kifedha, ikiwa ni hatua ya kupunguza utegemezi wa Dola na kuimarisha mahitaji ya Shilingi.

Kadhalika, Oktoba 2023, BoT pia ilianzisha kanuni mpya za kubadilisha fedha za kigeni (Bureau de Change), ambazo zinafuta kanuni za mwaka 2019, ili kurahisisha na kudhibiti shughuli za kubadilisha fedha.

Kanuni hizi zilijumuisha utambulisho wa aina tatu za leseni za Bureau de Change: A, B, na C na sehemu muhimu ya sheria hizi mpya iliruhusu hoteli zenye nyota tatu na zaidi kuanzisha maduka ya kubadilisha fedha bila mahitaji ya mtaji wa chini.

Hadi sasa, hoteli takribani 30 kote nchini zimepewa leseni ya kutoa huduma za kubadilisha fedha ndani ya maeneo yao.

Related Posts