Manyama: Tutatacheza nane bora  | Mwanaspoti

BAADA ya Srelio kuifumua Ukonga Kings kwa pointi 90-50 katika mchezo wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), meneja wa timu hiyo, John Manyama ametoa kauli ya kibabe kwa wapinzani wao, akisema hakuna wa kuwazuia kucheza nane bora ya mashindano hayo.

Manyama ameliambia Mwanaspoti kuwa, ushindi huo umewanyoshea njia ya kucheza hatua hiyo ambayo ni kiu kubwa ya timu shiriki kuifikia.

Alisema licha ya timu zote kuwania kucheza nane bora, lakini wao wameweka lengo hilo kuwa kipaumbele pekee na kwamba watapambana kuhakikisha kwamba wanafanikiwa.

“Kwa kweli tulianza vibaya katika mzunguko wa kwanza na  mabadiliko yalianza kuonekana baada ya kusajili wachezaji watatu Joseph Kamamba, Spoican Ngoma (kutoka Zambia) na  Chary Kesseng (Cameroon),” alisema Manyama.

Katika mchezo huo Srelio iliongoza katika robo nne kwa pointi 28-17, 18-8, 27-12, 17-12, huku Ngoma akiongoza kwa  kufunga pointi 18 kati ya hizo alifunga maeneo ya mitupo mitatu mara tano na kutoa asisti 10 akifuatiwa na Kesseng  aliyefunga pointi 16.

Kwa upande wa Ukonga Kings myota katika utupiaji nyavuni alikuwa Stanford Robert aliyefunga pointi 16 akifuatiwa na Stanley Mtunguja pointi 15.

Related Posts