Mawakili walivyochuana kwa hoja uchaguzi serikali za mitaa

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imekamilisha usikilizwaji wa shauri la maombi ya kibali ya kufungua shauri la kupinga uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 kusimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Mahakama hiyo imehitimisha usikilizwaji wa shauri hilo baada ya mchuano mkali wa hoja za kisheria kutoka kwa mawakili wa pande zote, uliochukua siku mbili.

Wakati uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 ukipangwa kufanyika Novemba 27, 2024,  Agosti 15, 2024 Waziri wa Tamisemi alitangaza kuanza rasmi kwa mchakato wa uchaguzi huo  mpaka Novemba 27, 2024, siku ya upigaji kura.

Lakini wanaharakati watatu wanaojitambulisha ni raia wa Tanzania waliosajiliwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga, wamefungua shauri la maombi, wakiomba kibali cha Mahakama waweze kufungua shauri la kupinga uchaguzi huo kwa utaratibu wa mapitio ya Mahakama.

Shauri hilo limefunguliwa na Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe, mwanahabari mstaafu, Ananilea Nkya na Bubelwa Kaiza na wajibu maombi ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika shauri hilo la maombi namba19721/21 linalosikilizwa na Jaji Wilfred Dyansobera, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, wanaomba kibali wafungue shauri la kupinga kanuni za uchaguzi huo zilizotungwa na Waziri wa Tamisemi wakihoji uhalali na mamlaka yake.

Pia, wanaomba kibali hicho wafungue shauri la kupinga uchaguzi huo kusimamiwa, kuratibiwa na kuendeshwa na Ofisi ya Rais Tamisemi, badala ya Tume Huru ya Uchaguzi, kwa mujibu wa Sheria ya Tume huru ya Uchaguzi ya mwaka 2024.

Hata hivyo, Serikali iliibua pingamizi la awali la hoja za kisheria ikiiomba Mahakama hiyo isilisikilize shauri hilo kwa madai lina kasoro za kisheria, huku wakibainisha kasoro nne kama sababu za kulifanya shauri hilo likose sifa za kusikilizwa badala yake litupiliwe mbali.

Hata hivyo, Mahakama iliamua kusikiliza pingamizi sambamba na maombi ya msingi ya kibali, badala ya kusikiliza pingamizi pekee kwanza na kulitolea uamuzi.

Hivyo, usikilizwaji wa shauri hilo ulianza jana Jumatatu Septemba 2, ambapo mawakili wa pande zote walichuana vikali kwa hoja za kisheria.

Jopo la mawakili wa Serikali likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo lilifafanua sababu hizo za mapingamizi.

Hata hivyo, mawakili wa waombaji hao, Mpale Mpoki (kiongozi wa jopo) na Jebra Kambole walipinga hoja hizo wakidai hazina mashiko na kwamba hazikidhi masharti ya kisheria ya kuwa pingamizi la awali.

Usikilizwaji wa shauri hilo umehitimishwa leo Jumanne Septemba 3, 2024 kwa kusikiliza shauri la msingi, maombi ya kibali cha kufungua shauri rasmi kupinga kanuni zilizotungwa na Waziri na uchaguzi kusimamiwa na Tamisemi badala ya Tume Huru ya Uchaguzi.

Mchuano wa pili wa mawakili

Wakati wa usikilizwaji wa maombi leo Jumanne, Septemba 3, 2024, waombaji hao kupitia mawakili wao Mpale Mpoki na Jebra Kambole wameieleza Mahakama kuwa, wamekidhi masharti ya kisheria kustahili kupewa kibali cha kufungua kesi kupinga uchaguzi huo.

Hata hivyo, hoja hizo zimepingwa na wajibu maombi kupitia jopo la mawakili wa Serikali linaloongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo, wakidai waombaji wameshindwa kuonesha wamekidhi masharti hayo, hivyo kushuhudiwa mchuano mwingine wa hoja za kisheria.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, Wakili Kambole ametaja masharti yaliyowekwa na sheria ambayo mwombaji wa kibali cha kufungua shauri anapaswa kuyakidhi kisha akaionesha Mahakama jinsi wateja wao walivyokidhi masharti hayo.

Masharti ya shauri la maombi ya kibali kufunguliwa ndani ya miezi sita/mitatu tangu kufanyika kwa uamuzi unaokusudiwa kupinga, kuwepo kwa hoja inayobishaniwa inayohitaji kujadiliwa na kuonesha masilahi katika jambo au uamuzi uliofanywa.

Kambole amesema kanuni wanazokusudia kuzipinga zilizotungwa na Waziri wa Tamisemi na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali kupitia Tangazo la Serikali (GN) 571, 572, 573, 574, Julai 12, 2024 , hivyo maombi hayo yako ndani ya muda huo wa miezi.

Kuhusu hoja inavyotakiwa kujadiliwa, Kambole amedai Mahakama kwa kuangalia nyaraka za waombaji kama maelezo ya shauri,  kiapo na hati ya maombi yafaragha, zitaifanya Mahakama itoe amri zinazoombwa.

Amedai waombaji wanadai Waziri kutunga sheria za kusimamia uchaguzi huo si halali kwa kuwa hilo ni jukumu la Tume Uhuru ya Uchaguzi, lakini wajibu maombi wanadai kuna sheria zinampa mamlaka Waziri na hazijafutwa.

“Mheshimiwa Jaji kama ni halali (Waziri kutunga sheria kusimamia uchaguzi huo) hiyo ni hoja ya kesi ya kujadiliwa. Kwa hiyo basi ni muhimu Mahakama hii ikawafungulia mlango waombaji ili haya mabishano yakajibiwe vizuri na Mahakama,” amesema Wakili Kambole.

Katika sharti la tatu la kuwa na maslahi, Kambole amedai aya ya 2, 3, 4 na ya 14 ya kiapo zinaonesha waombaji wana masilahi kwa sababu wameeleza ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pia ni wapigakura kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Amedai pia, wameambatanisha nakala za vitambulisho vya upigaji kura kama nyaraka za kuthibitisha masilahi yao katika uchaguzi huo, ambavyo ni miongoni mwa vitu ambavyo kanuni hizo kwa mujibu wa GN 574 (3) (a) inavitambua.

Pamoja na ufafanuzi huo wa hoja za kuishawishi Mahakama iwape kibali hicho, ndipo likaibuka ombi la kusimamisha mchakato wa uchaguzi huo unaoendelea.

Kwa upande wake, Wakili Mpoki ameiomba Mahakama wakati inatoa uamuzi wake, ilikubali maombi hayo na itumie mamlaka yake kusimamisha utekelezaji wa kanuni hizo zinazopingwa, ambazo utekelezaji wake unapoendelea, mpaka hapo shauri lenyewe litakalofunguliwa litakaposikilizwa na kuamuriwa.

Amedai uchaguzi ni mchakato na kwamba kama ukiruhusiwa kuendelea litasababisha ukosekanaji wa haki kwa waombaji.

Amedai si mara ya kwanza kwa Mahakama kutoa zuio kwenye maombi ya kibali, huku akiirejesha Mahakama kwenye uamuzi wa kesi kadhaa zilizoamuriwa na Mahakama hiyo kwenye mazingira yanayofanana na shauri hilo.

“Endapo amri hii (zuio) haitatolewa waombaji watapata hasara ambayo haitaweza kufidiwa,” amesema Wakili Mpoki na kusisitiza si hao waombaji watatu tu, bali nyuma yao kuna kundi kubwa ambalo pia litaathirika.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Erigh Rumisha amesema wanapinga maombi haya kwa sababu waombaji hawana kesi na kwamba huo ndio msingi wa pingamizi lao la awali.

Amedai waombaji wanapaswa kuonesha hawana namna nyingine isipokuwa kufungua shauri hilo.

“Tunasema hivi kwa sababu wao wanasema Waziri hana mamlaka ya kusimamia, kuratibu na kuendesha uchaguzi wa Serikali za mitaa na kwamba haya mamlaka imepewa Tume Huru ya Uchaguzi hasa kifungu cha 10 cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi,” amesema Rumisha na kuongeza:

“Lakini wameshindwa kutambua kwa mujibu wa kifungu hicho ili Tume Huru ya Uchaguzi iweze kufanya kazi na kusimamia hayo yote lazima kuwepo na sheria nyingine.”

Amesema bila kuwepo hiyo sheria nyingine, Tume Huru ya Uchaguzi haiwezi kufanya kazi, lakini akasema bado sheria zipo zinazompa mamlaka Waziri kutunga kanuni kuendesha uchaguzi huo.

“Kama sheria zipo zinazompa Waziri mamlaka ya kutunga kanuni, kosa gani Waziri amelifanya? Sasa wameleta kesi gani,” amehoji Rumisha na kusisitiza wameshindwa kuleta kesi yenye mashiko.

Amedai kifungu cha 10 (1) (C) cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi kinasema Tume hiyo itasimamia na kuendesha uchaguzi kwa kuzingatia sheria nyingine itakayotungwa na kwamba wakati Bunge linatunga sheria hiyo lilikuwa linajua sheria hizo bado zipo.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kelvin Kisayo amedai  kanuni ziliizotungwa na Waziri wa Tamisemi kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, kwa mujibu wa Kanuni ya 13 GN namba 574 na 13 GN 573 na 572, imeanisha vigezo muhimu.

Wakili Kisayo amevitaja vigezo hivyo ni  kuwa raia wa Tanzania, umri kuanzia miaka18, mkazi wa mtaa husika na kuandikishwa katka orodha ya wapiga kura.

Amedai kanuni ya 14 inasema atakayekosa mojawapo ya sifa hizo sasa swali ni kwamba wameandikishwa kwenye orodha ya wapigakura?

Amedai kwa uandikishaji wa orodha ya wapigakura bado haujafanyika basi waombaji hawajawa na vigezo vya kuwa na masilahi katika uchaguzi huo mpaka watakapoandikishwa.

Wakili amedai kitambulisho cha mpigakura si kigezo kwa kuwa kanuni ya 14 inamtaka mtu kuwa na kitambulisho cha kujiandikisha katika orodha ya wapigakura na kwamba kadi hiyo ya mpigakura haitambuliki katika uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Amedai angalau waombaji wangekuwa na barua za utambuliaho kutoka kwa viongozi wa maeneo wanayoishi ili kuwatambulisha kama wakazi wa maeneo hayo, lakini hawajawasilisha hata utambuliaho wa makazi yao.

“Hivyo, mheshimiwa Jaji hawajaonesha masilahi mapana,” amesisitiza Wakili Kisayo.

Wakili wa Serikali Ayoub Sanga amepinga maombi hayo ya kusimamisha mchakato wa uchaguzi huo kwanza akidai hayo ni maombi ya mawakili na si ya waombaji kwa kuwa hawajayaweka kwenye kiapo chao.

Wakili Sanga amedai hakuna taarifa kuunga mkono namna gani hiyo amri isipotolewa watapata madhara yasiyoweza kurekebishika.

Akirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani amesema maombi ya mawakili si ushahidi hivyo hayapaswi kuzingatiwa.

Amesema pia hawajaonesha ni madhara gani ambayo watayapata yasiyoweza kurekebishika akisema uchaguzi umepangwa kufanyika Novemba na mahakana ina muda maalumu wa kusikiliza shauri hilo.

“Mheshimiwa Jaji ni madhara gani yasiyorekebishika ikiwa Mahakama hii haitatoa amri hiyo (kusimamisha mchakato wa uchaguzi) ikiwa alichokifanya sasa hivi mjibu maombi wa kwanza (Waziri) ni uelimishaji na uratibu wa shughuli za awali,” amehoji Wakili Sanga.

“Kwa hiyo ikiwa Mahakama hii itatoa amri hiyo basi atakayepata hasara ni mujibu maombi wa kwanza (Waziri) kwani shughuli hizo zitasimama na wao hawatapata hasara yoyote.”

Amedai uchaguzi ujao unatarajiwa kupata wapigakura wasiopungua milioni 34, sasa na kwamba hawa wote, wanaendelea kupata huduma ya uelimishaji na uratibu ambayo waombaji hao wanataka isimamishwe.

Hata hivyo, ameiomba Mahakama kama itaamua kutumia mamlaka yake hayo basi inapaswa kuangalia maslahi ya pande zote.

Wakijibu hoja hizo za mawakili wa Serikali, mawakili wa waombaji wamesisitiza hoja zao wakidai waombaji wakidhi masharti ya kupewa kibali hicho.

Kuhusu ombi la zuio, Wakili Mpoki ameieleza Mahakama halitoki kwa mawakili kama Wakili wa Serikali Sanga alivyodai bali kwa waombaji akiielekeza Mahakama katika aya ya sita ya hati ya maelezo ya kesi.

Amedai lipo tatizo la taasisi mbili (Tume Huru ya Uchaguzi na Ofisi ya Rais Tamisemi) kupewa jukumu moja la kusimamia uchaguzi hio kwa sheria mbili tofauti na kwamba Mahakama hiyo ndicho chombo pekee cha kutatua tatizo hilo kwa kuwapa kibali waombaji kufungua kesi hiyo.

Jaji Dyansobera baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha shauri hilo hadi Septemba 9, 2024 saa 6: 00 mchana kwa ajili ya uamuzi.

Related Posts