Dodoma. Mbunge wa Ilemela (CCM), Dk Angelina Mabula amelazimika kuomba radhi bungeni na kufuta maneno yake kwamba wagonjwa wanaume, wanawake na watoto wanalazwa wote kwenye wodi moja.
Mabula amelazimika kuomba radhi baada ya ushahidi wake aliowasilisha bungeni kuthibitisha maelezo yalitolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange kwamba siyo kweli wagonjwa wanaume, wanawake na watoto wanachanganywa wodi na ilikuwa ni kulidanganya Bunge.
Waziri huyo wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitekeleza hilo leo Jumanne, Septemba 3, 2024 kabla ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuahirisha mkutano wa Bunge hadi leo Jumatano, Septemba 4, 2024.
“Asante mheshimiwa Spika (Dk Tulia Ackson) kwa kunipa fursa kusema maneno machache baada ya kupitia ushahidi wote ulioletwa. Pamoja na maelezo uliosema utambuzi ni kwamba bado pana changamoto na bado pale wamezungumzia wanapozidi bado wanaingia kule.
“Kwa hiyo kama ilileta mtafaruku kwa namna ambavyo hali halisi nilivyoiwasilisha, mheshimiwa Spika naomba kufuta hayo maneno, lakini changamoto inabaki ni ile ile ya kwamba hakuna miundombinu na naomba radhi kama limeleta mtafaruku katika kuelewa hoja halisi niliyokuwa nimeileta,” amesema Mabula baada ya kupewa nafasi na Spika.
Baada ya Mabula kuomba radhi, Spika amesema hoja hiyo sasa imefungwa. “Wabunge hoja hiyo inafungwa kwa namna hiyo kwa hiyo maneno yalizungumzwa kwa siku ile yakiashiria Serikali ama mheshimiwa naibu waziri Ofisi ya Rais Tamisemi hajazungumza jambo lenye uhalisia basi yanafutwa kwenye taarifa rasmi za Bunge kama mheshimiwa mbunge alivyozungumza.”
Spika Tulia alisema Agosti 27, 2024, wakati wa maswali na majibu, Mabula alipata fursa ya kuuliza swali la nyongeza katika swali namba tatu ambalo lilikuwa limeulizwa na Mbunge wa Korogwe Mjini (CCM), Dk Alfred Kimea.
Swali la nyongeza la Mabula lilikuwa:
“Mheshimiwa Spika Kituo cha Afya cha Sangabuye kilipandishwa hadhi mwaka 1999 kutoka zahanati na kuwa kituo cha afya, kituo hicho mpaka leo kina wodi moja ambayo inatumika na wanawake, wanaume pamoja na watoto. Je, lini Serikali itakamilisha miundombinu pale ikiwa ni pamoja na kujenga uzio.”
Spika alisema baada ya swali hilo la nyongeza, kabla hajampa naibu waziri ambaye wakati huo alikuwa mbele kwa ajili ya kujibu maswali, alimuomba Mabula kwa kumuuliza ni kwa namna gani wanawake, wanaume na watoto wote wanalala sehemu moja, ama kwenye wodi moja.
“Mheshimiwa mbunge akasema kwamba hiyo ndiyo hali halisi iliyopo.
“Nilivyompa nafasi mheshimiwa naibu waziri akasema hilo jambo katika hali ya kawaida haliruhusiwi ama kwa utaratibu uliopo haliruhusiwi, lakini atafuatilia ili aone ni nini kinachoendelea.
“Na mimi kwa kuwa lilizungumzwa kwa uzito nikamwambia naibu waziri akimaliza kujibu maswali aende akafuatilie jambo hili kisha alete taarifa,” amesema Spika.
Hata hivyo, Spika amesema kabla hajaahirisha Bunge, naibu waziri akawa amempelekea ushahidi ambao ulikuwa ni ushahidi wa maelezo, lakini pia picha ya hali halisi ya kituo hicho.
“Kwa kuwa nililetewa mimi kwa maandishi, nilimpa taarifa mbunge Mabula kwamba haya ndiyo maelezo ya Serikali, kwa maana kuwa kwanza hicho Kituo cha Afya hakina wodi kabisa, lakini Serikali kwa kutambua hilo wale watumishi wamejiongeza wamewekwa vyumba vitatu kwa ajili ya watoto chumba kimoja, wanaume chumba kingine na wanawake chumba kingine.
“Na wakawa wamepiga picha vile vibao kuashiria kwamba hilo eneo kuna sehemu tatu za kulaza wagonjwa, lakini ile taarifa ilionyesha wodi hakuna isipokuwa vile vyumba ambavyo vingetumika kwa shughuli nyingine hapo, sasa vinatumika kwa ajili hiyo wakati wanasubiri ujenzi wa wodi.
“Baada ya kutoa maelezo hayo Mabula alisimama kuomba mwongozo kwamba yale maelezo yaliyotolewa kama ushahidi wa kile kinachoendelea pale kwenye kituo cha afya hakuna uhalisia kwa sababu yeye amefanya ziara kwenye hilo eneo hivi karibuni na amekuta hao wanawake, watoto na wanaume wanalala sehemu moja,” amesema Spika.
Spika amesema kwa sababu alikuwa amepelekewa ushahidi na upande wa Serikali alimhoji mbunge kama naibu waziri ama Serikali inasema uongo bungeni.
“Mheshimiwa Mabula akasema kile alichokisema ndio hali halisi. Sasa kwa sababu kanuni yetu ya 70 ukisoma kwa ujumla wake inamtaka yule anayetoa tuhuma ndiye athibitishe nikamtaka Mabula alete ushahidi na alileta ushahidi unaothibitisha jambo lake,” amesema Spika.
Spika amesema ushahidi aliopelekewa na Mabula umetoka maeneo matatu, kwenye ofisi ya mbunge, ushahidi mwingine ni muhtasari cha kamati ya siasa ya Kata ya Sangabuye, ambayo inaonesha wakati wakijadili jambo hilo ambalo ni changamoto kwenye kata yao.
“Maelezo yaliyochukuliwa kwenye huo muhtasari yanaashiria mjadala ulisema wodi ya wanaume hakuna kwa hivyo, kwa kuwa wodi ya wanaume hakuna wakati mwingine wanapelekwa kwenye chumba cha wanawake.”
Maneno yanavyosema: “Kituo cha Afya cha Sangabuye hakina wodi ya wanaume, wagonjwa wanapozidi wanahamishiwa kwenye chumba cha wanawake, kwani chumba kilichopo cha wanaume ni chumba kimoja tu chenye vitanda viwili.”
Spika amesema ukisoma hayo maneno hayapingani na majibu aliyokuwa ameyatoa naibu waziri kwa ushahidi kwamba chumba kipo cha wagonjwa wanaume, maana wanasema wakizidi, wasipozidi maana yake wana chumba chao.
“Wanapopelekwa kwenye chumba cha wanawake ile siyo wodi ni chumba ambacho kimetengwa kwa ajili ya kuwahudumia wanapokuwa na hizo changamoto na kwamba siyo kwamba wanachanganywa ikiwa wanawake hawapo na chumba kiko wazi wanaume wanapozidi ndio wanapelekwa kule. Siyo kwamba wanalazwa wote kwa pamoja.
“Ushahidi mwingine ulioletwa na kiambatanisho cha maadhimisho ya kuzaliwa CCM miaka 47 ambayo inaonyesha wodi katika Kituo cha Afya cha Sangabuye hakipo kabisa,” amesema.
Spika amesema katika kuchambua ushahidi wote, alichokisema mbunge kile kituo cha afya kina changamoto za miundombinu, kilichoongezeka hapo wagonjwa wanalala wote sehemu moja. Hoja ya mbunge kwamba wote wanalala pamoja siyo kweli.