Arusha. Mahakama ya Rufani imebariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa, aliyekuwa mlinzi wa Kampuni ya la Commercial Coal Security Company, Edger Jackson, aliyemuua mfanyabiashara wa madini, Jofrey Mbepela.
Edger alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Februari 9, 2023 kwa kumuua kwa kumpiga risasi mfanyabiashara akiwa mlinzi wa zamu ofisini kwa marehemu.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Augustine Mwarija, Rehema Kerefu na Omar Othman Makungu, walisikiliza rufaa hiyo namba 167/2023 na kutoa uamuzi huo Septemba 2, 2024, katika vikao vyake vilivyoketi Songea.
Majaji hao walifikia uamuzi huo baada ya kupitia mwenendo na kubaini upande wa mashtaka ulithibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.
Masuala mengine iliyozingatia ni kutoweka nyumbani kwake baada ya tukio na kutoroka kazini na kutokomea msituni.
Edger alishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu.
Agosti 18, 2021 katika eneo la la Dar Pori ndani ya Kijiji cha Lunyele, Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, alimuua Jofrey.
Marehemu alikuwa mfanyabiashara akiwa na ofisi yake ya biashara eneo la Dar Pori wilayani Nyasa, iliyokuwa inalindwa na walinzi wawili wa kampuni hiyo ya ulinzi inayomilikiwa na Danroof Mbinga.
Siku ya tukio, Edger akiwa ni mmoja wa walinzi wa zamu katika ofisi ya marehemu, akiwa na mlinzi mwenzake Emmanuel Ngongi.
Jofrey akiwa na mpenzi wake Neema Komba (shahidi wa 10), usiku alitoka nje kupokea simu, akarudi ndani lakini muda mfupi baadaye alitoka nje, hakurudi ndani tena, hadi alipokutwa asubuhi amefariki na mwili wake ukiwa karibu na mlango wa ofisi yake.
Ilidaiwa tukio hilo lilisababisha mkusanyiko na kutokana na Edger kutokuwepo eneo la tukio, kuliibua mashaka akihusishwa na mauaji hayo baadaye alikamatwa Kijiji cha Shawishi.
Neema katika ushahidi wake alidai akiwa amelala aliamshwa na mlio wa risasi lakini alidai hakushuku lolote baya kwa sababu alizoea ufyatuaji wa risasi uliokuwa ukifanyika eneo hilo mara kwa mara kuwatisha wezi.
Alidai baada ya marehemu kutoka kwa mara ya pili, Edger aliingia chumbani na kuomba funguo alizozitoa kwenye mfuko wa suruali ya Jofrey kwa madai kuwa ndiye aliyemtuma kuchukua na alipoamka asubuhi, alikuta mwili wake karibu na mlango wa ofisi.
Ilidaiwa mahakamani kuwa, kukamatwa kwa Edger katika Kijiji cha Shawishi kuliwezeshwa na mgambo Ditrick Ndunguru (shahidi wa tatu) ambaye alidai kupata taarifa kijijini kwao kuwa kuna mtu asiyefahamika anayedaiwa kufanya mauaji.
Alidai kuchunguza hadi kusaidia polisi kumkamata Edger aliyekuwa na pikipiki yake yenye namba za usajili MC 840 CNY.
Shahidi huyo alidai baada ya Edger kuhojiwa aliwaongoza polisi hadi alipokuwa ameificha bunduki aliyokabidhiwa na mwajiri wake ili aitumie katika majukumu yake ya uangalizi wa ofisi, aliyokuwa ameifukia ardhini.
Agosti 23, 2021 mrufani huyo alipelekwa Kituo cha Polisi cha Mbambabay na kuandika maelezo ya onyo yaliyorekodiwa na shahidi wa nane ambaye ni ASP Zabron Msusi.
Maelezo hayo ya Edger yalikubaliwa kama kielelezo cha 11 ambaye kupitia maelezo hayo alikiri kutenda kosa hilo.
Shahidi wa sita, Kamilius Lupembe ambaye alikuwa mlinzi wa zamu ya usiku katika ofisi nyingine, alidai alisikia mlio wa risasi eneo la tukio na alipokwenda kuulizia Edger alimjibu kuwa alimuua mwizi.
Alidai alipokwenda eneo la tukio aliuona mwili wa marehemu na kukuta hakuna mlinzi hata mmoja kati ya wawili hao.
Katika utetezi wake, Edger hakukana kumpiga risasi marehemu lakini alidai ufyatuaji wa risasi ulitokea wakati wa mapambano kati yake na Jofrey.
Alidai siku hiyo Jofrey alimuomba bunduki ili akafungue mlango kuchukua mtungi wa gesi lakini muda mfupi baadaye alimuona akiwa na mtu mwingine, kwa kuwa alikuwa amemnyooshea bunduki, ugomvi ulitokea.
Alidai kuwa aliona kidole cha marehemu kikiwa kwenye kifyatulia risasi na ghafla akafyatua risasi iliyompata (Edger) shavuni na kuanguka chini na kuona picha za watu wanne waliokuwa wamefunika nyuso zao.
Alidai kuwaambia watu hao wachukue bunduki kwa marehemu lakini alipoenda na kuhangaika kuichukua, aligeuza bunduki kuelekea kwa marehemu na kwa bahati mbaya alifyatua risasi iliyompata na kumuua marehemu.
Alidai baada ya tukio hilo, aliingiwa na wasiwasi, hivyo kukimbilia Kijiji cha Kingunita kwa kutumia pikipiki yake na kukiri baada ya kukamatwa, aliongoza polisi hadi alipokuwa ameificha bunduki.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Mahakama ilimhukumu adhabu hiyo baada ya kubaini upande wa mashtaka umethibibisha kesi pasipo shaka na ilitegemea maelezo na tabia ya Edgar kukimbia baada ya tukio.
Katika Mahakama ya Rufani, Edger aliwasilishwa na Wakili Eliseus Ndunguru huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Hellen Chuma.
Baadhi ya hoja zake ni Mahakama kumtia hatiani wakati upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi, Mahakama ilikosea kisheria ilipoandika ushahidi kinyume na maagizo ya Kanuni za Mwenendo wa Jinai.
Nyingine ni Mahakama ilikosea kisheria ilipokubali kielelezo cha 11 (maelezo yake ya onyo), ambacho kilirekodiwa kinyume na matakwa ya kifungu cha 57 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) pamoja na mrufani kunyimwa haki ya kuwakilishwa ipasavyo na wakili.
Kuhusu hoja ya kukiukwa kwa kifungu cha 57 cha CPA, Jaji Mwarija amesema madai ya maelezo ya onyo kudaiwa kurekodiwa nje ya muda tangu mrufani alipowekwa kizuizini, haikutajwa muda ambao maelezo hayo yalichukuliwa.
Jaji Mwarija amesema wamezingatia ipasavyo mawasilisho ya upande wa Edger na kuwa wamegundua maelezo hayo ya onyo yalichukuliwa kinyume na sheria hivyo kufuta maelezo hayo kwenye kumbukumbu ya Mahakama.
Kuhusu kesi kutothibitishwa bila kuacha shaka, Jaji Mwarija amesema uamuzi wao katika msingi huo ni kuangalia iwapo mauaji hayo yalikuwa ya bahati mbaya au la.
Alieleza hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa kulikuwa na vita kati ya mrufani na marehemu ila baada ya tukio hilo alikimbilia kijiji kingine na kuficha bunduki iliyotumika katika mauaji hayo.
“Mwenendo huo wa mrufani kutoweka baada ya tukio na kutoroka kazini hauendani na kutokuwa na hatia kuhusiana na mauaji ya marehemu. Kwa maoni yetu kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa bila shaka yoyote na kutupilia mbali rufaa yake,” amesema Jaji Mwarija.