Mufti amshukuru Rais Samia, vyombo vya habari mashindano ya Quran

Dar es Salaam. Siku chache baada ya kufanyika kwa mashindano ya Quran kwa wanawake ya dunia jijini Dar es Salaam, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir ametoa shukrani zake kwa wote waliofanikisha mashindano hayo.

Mufti Zubeir pia, amemshukuru Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na mlezi wa mashindano hayo.

Sambamba na hilo, amevishukuru vyombo vya habari yakiwamo magazeti ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ya Mwananchi na The Citizen kwa kufanikisha mashindano hayo yaliyofanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania.

Mufti amebainisha hayo leo Jumanne, Septemba 3, 2024 katika Msikiti wa Mfalme Mohammed VI, uliopo Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Mufti Zubeir amesema ushiriki wa vyombo hivyo vya habari umefanikisha mashindano hayo kufanyika kwa mafanikio makubwa.

Amesema, matarajio yao kwa mwakani mashindano yatakuwa makubwa zaidi ukizingatia ya mwaka huu yameleta mwamko kwa kinamama ambao kwa namna moja au nyingine wamesahauliwa.

“Sasa hivi kuna mmomonyoko wa maadili na walengwa wakubwa ni vijana na wasichana na ukiangalia Quran inafundisha maadili, heshima, huruma na vitendo vyema pamoja na kujiepusha na vitendo visivyostahili. 

“Sasa hivi kuna dhuluma, kuuwana na mambo mengi mabaya, kitabu kitukufu kinafundisha uadilifu, sasa umuhimu wa mashindano haya kwao ni kwamba wakitoka pale wamejifunza maadili mazuri na kila mmoja ataenda kujibadilisha,” amesema. 

Mashindano hayo yaliyofanyika Agosti 31, 2024 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo mshiriki kutoka Algeria aliibuka mshindi kati ya washindani wote kutoka nchi 11, yakiwa na lengo la kuonyesha nafasi ya mwanamke katika jamii.

Katika mashindano hayo, Tanzania imebahatika kuwa nchi ya kwanza mwenyeji na katika hotuba yake, Rais Samia alisisisitiza umuhimu wa haki, amani, kuheshimiana na kustahimiliana kama nguzo za kuimarisha umoja kama taifa.

Alisema mashindano hayo yanachangia katika kuimarisha maadili ya kitaifa na kudumisha mshikamano miongoni mwa wananchi wa Tanzania bila kujali tofauti za kidini au kikabila.

Rais Samia pia, aligusia umuhimu wa kuendeleza maadili ya nchi, akibainisha familia yenye misingi imara ni msingi wa taifa lenye nguvu.

Sambamba na hilo alihimiza wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto wanalelewa katika mazingira ya heshima, amani na upendo ili kuijenga jamii yenye maadili bora.

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma ametaja nchi 11 zilizoshiriki kuwa  ni Tanzania (Bara na Zanzibar), Msumbiji, Sudan, Algeria, Jordan, Saud Arabia, Kuwait, Indonesia, Marekani, Ujerumani na Urusi.

Kufanyika kwa mashindano hayo, amesema kumelenga kuonyesha nafasi ya mwanamke katika uislamu na yamelijengea kundi hilo mazingira bora yanayohakikisha usalama, amani na haki.

Related Posts