KOCHA wa Namungo FC, Mwinyi Zahera amepewa mtihani wa kushinda zaidi ya mechi mbili ili kuendelea kusalia ndani ya kikosi hicho, nje na hapo kibarua chake kinaweza kuota nyasi.
Zahera ambaye alianza kukinoa kikosi hicho tangu msimu uliopita akitokea Coastal Union, inaelezwa endapo dili la kocha wa Simba Queens, Juma Mgunda lingetiki basi hadi asingekuwepo katika benchi hilo.
Awali ilielezwa Mgunda angekwenda kuwa kocha mkuu, angekuwa anasaidiana na Ngawina Ngawina ambaye tayari ametangazwa kutua Namungo.
Alipotafutwa katibu wa timu hiyo, Ally Seleman, alisema Zahera hana malengo aliyopewa isipokuwa ameongezewa nguvu ya msaidizi, Ngawina.
“Kwa sasa tunaweka nguvu zetu katika kupambania matokeo ya mechi zilizopo mbele yetu. Ijulikane kocha ni Zahera ameongezewa nguvu ya Ngawina,” alisema.
Kuhusu nani anachukua nafasi ya mtendaji mkuu wa timu hiyo baada ya kuondoka Omar Kaya, alisema wanaendelea na mchakato na mambo yakiwa tayari watatangaza.