Dar es Salaam. Raia wa Visiwa vya Comoro sasa watatibiwa Tanzania kwa huduma za afya walizokuwa wakizifuata Bara la Ulaya na Mashariki ya mbali.
Hayo yamesemwa leo Jumanne, Septemba 3, 2024 na Spika wa Bunge la Comoro, Moustadroine Abdou wakati akizungumza na vyombo vya habari baada ya kutembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), jijini Dodoma.
“Huduma tulizokuwa tunazifuata Ulaya na Asia kama upandikizaji wa figo kumbe tunaweza kuzipata hapa Tanzania,” amesema Abdou.
Spika huyo wa Visiwa vya Comoro ametembelea idara za magonjwa ya moyo, huduma ya upandikizaji uloto (tiba ya sikoseli), idara ya radiolojia inayotoa huduma za vipimo mbalimbali ikiwamo MRI, kliniki maalumu ya viongozi na wodi ya Rais katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema ziara hiyo imempa fursa spika huyo kushuhudia mageuzi yaliyofanywa katika sekta ya afya.
“Pia, mradi wa Kituo cha Nuclear Medicine cha Benjamin Mkapa umefikia asilimia 50. Kituo hiki kitakuwa ni Kituo cha Umahiri wa Matibabu ya Saratani katika Afrika. Tutashirikiana na Chuo Kikuu cha Harvard cha Marekani,” amesema Dk Mollel.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dk Kessy Shija amesema BMH inahudumia takribani wananchi milioni 14 katika kanda ya kati na mikoa ya jirani.
“BMH tunatoa huduma za afya za ubingwa wa kati na ubingwa wa juu kama upandikizaji wa figo na upandikizaji uloto ambayo ni tiba ya sikoseli,” amesema Dk Shija kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Profesa Abel Makubi.
Dk Shija amesema katika ushirikiano huo wa BMH na Visiwa vya Comoro, Hospitali ya Benjamin Mkapa itafanya huduma mkoba (medical outreach) katika visiwa hivyo vilivyopo Kusini Mashariki ya Afrika.
“Ushirikiano pia utahusisha mafunzo kwa wataalamu kutoka Comoro kuja kufanya mafunzo ya vitendo hapa BMH,” amesema Dk Shija.