RAIS MHE. DKT. SAMIA ACHANGIA MILIONI 50 KANISA LA MENNONITE

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akitoa hotuba kwa niaba ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Elimu Mkamba cha Kanisa la Mennonite Tanzania, Jijini Dar es salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akiteta jambo na Baba Askofu Nelson Kisare, Askofu Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Elimu Mkamba cha Kanisa la Mennonite Tanzania, Jijini Dar es salaam.

…..

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ametoa rai kwa waamini wa Kanisa la Mennonite Tanzania ya kuendelea kulinda umoja, amani, uhuru, mshikamano na ustawi wa watanzania kwa maendeleo ya Taifa la Tanzania.

Mhe. Simbachawene ametoa rai hiyo wakati alipomwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Elimu Mkamba cha Kanisa la Mennonite Tanzania, iliyofanyika katika kanisa la Mennonite Dayosisi ya Mashariki, Jijini Dar es salaam.

“Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatambua umuhimu wa elimu kwa watanzania, hivyo anachangia milioni 50 ikiwa ni jitihada za kuhakikisha kituo kinajengwa haraka ili watoto wetu waweze kupata elimu ya dunia na ya kiroho, na mimi nilitamani kuchangia milioni 2.5 lakini kwa mahubiri ya Baba Askofu Gabriel Magwega, Askofu wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Dayosisi ya Mashariki yamenigusa kutoa zaidi, sasa nitatoa sadaka milioni 5 ili kujenga kituo hiki cha kuandaa rasilimaliwatu” Mhe. Simbachawene.

Mhe. Simbachawene aliongeza kuwa rasilimawatu ikiandaliwa vizuri na kupata elimu bora, nchi itapata viongozi wenye hofu ya Mungu na watakuwa na uwezo wa kuongoza nchi kwa kuzingatia maadili mema, hivyo kuleta maendeleo ya haraka kwa taifa na wananchi kwa jumla.

Aidha, aliongeza kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan iko tayari kushirikiana na Kanisa katika kuondoa maadui watatu yaani ujinga, maradhi na umaskini. Kwa hiyo ujenzi wa Kituo hicho cha Elimu cha Mkamba ni msingi wa kupambana na maadui hao.

Awali, Baba Askofu Nelson Kisare, Askofu Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania alisema kuwa Serikali imeridhia Malengo 17 ya Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu (SDG) ambapo katika malengo hayo lengo namba 4 linahusu elimu hususani Elimu Jumuishi, kwa mantiki hiyo Kanisa la Mennonite Tanzania linaunga mkono Serikali katika jitihada za kutekeleza malengo hayo kwa kuandaa mazingira bora ya kutoa elimu kwa watanzania.

Vilevile, aliongeza kuwa Kanisa litaendelea kushirikiana na Serikali katika utoaji wa elimu bora kwa wasichana na wavulana ili kuunga mkono jitihada za kuondoa ujinga, maradhi na umaskini. Pia, kanisa litahakikisha katika shule hiyo linatoa vijana wa kitanzania waliolelewa katika misingi ya neno la Mungu, wenye kumcha Mungu na wenye hofu ya  Mungu ndani ya mioyo yao.

“Waziri, Mhe. Simbachawene tunaomba utufikishie salaam zetu za shukurani kwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupokea barua yetu, kukubali mwaliko na kukutuma wewe kuja kumuwakilisha, jambo hili ni kubwa sana na sisi tutaendelea kumuombea kwa Mungu ili aendelee kuongoza nchi hii kwa amani, furaha na upendo daima” alisema Baba Askofu Kisare.

Related Posts