Serikali kutoa maelekezo kwa halmashauri kujenga viwanja

Dodoma. Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inafikiria kuzielekeza Mamlaka bajeti zao kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa viwanja vya michezo kwa maeneo yao.

Hayo yamesemwa leo Septemba 3,2024 na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Jacqueline Kainja.

Mbunge huyo amehoji Serikali ina mpango gani wa kujenga viwanja vya michezo nchini katika ngazi ya wilaya.

Akijibu swali hilo, Mwinjuma amesema jukumu la ujenzi wa miundombinu ya michezo ni la Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya michezo zikiwemo taasisi, mashirika, watu binafsi na mamlaka za Serikali za Mitaa.

Amesema katika kuhakikisha kuwa kila wilaya inakuwa na viwanja vya michezo, karibuni Serikali itazielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga mafungu katika bajeti zao ili kutekeleza miradi ya ujenzi wa viwanja vya michezo kwa maeneo yao.

“Tayari kuna halmashauri zimeanza utekelezaji huu ambazo ni:- Halmashauri za Wilaya za Kinondoni (Uwanja wa KMC Stadium), Bukoba Mjini (Uwanja wa Kaitaba), Nyamagana (Uwanja wa Nyamagana) na Namungo (Majaliwa Stadium).

Aidha, Halmashauri ya Wang’ing’ombe inajenga kijiji cha michezo ambacho kitakapokamilika kitakuwa na viwanja vya michezo ya soka, volleyball, Netball na Basketball .Halmashauri ya Sengerema, Mkoani Geita imeandaa ‘Concept Design’  kwa ajili ya Kituo cha Michezo,” amesema Mwinjuma.

Amesema kwa sasa Serikali ipo kwenye ukarabati mkubwa wa viwanja vya Uhuru na Benjamin Mkapa hata hivyo, Serikali inaendelea na ujenzi wa Uwanja wa Arusha (Arusha Stadium) na ukarabati viwanja vingine vitano vya mazoezi kwa ajili ya mashindano ya CHAN 2025 na AFCON 2027.

Amesema ametoa rai kwa halmashauri, wilaya na mikoa ambayo haijaguswa na miradi ya AFCON 2027 kuanza kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kujenga viwanja vya kisasa vya michezo ili pia wapate vyanzo vipya vya makusanyo katika maeneo yao.

Katika swali la nyongeza, Kainja amehoji Serikali inampango gani wa kushirikiana na taasisi zenye viwanja vingi (hakuitaja), hasa kwa zile halmashauri ambazo hazina mapato ya kutosha.

Pia amehoji kama Serikali imeshafanya tathimini ya kuangalia gharama zinazohitajika katika kukarabati viwanja vyote vya wilaya.

Akijibu maswali hayo, Mwinjuma amesema bado Serikali inafanya majadiliano na taasisi husika (yenye viwanja vingi), kuangalia namna ambavyo wanaweza kufanya ukarabati na namna ambavyo fedha watakazotumia zitaweza kurejeshwa katika mfuko wa umma utakaotoa.

Amesema lengo ni kutumia mfuko wa maendeleo ya michezo ambao kwa sasa unapata mapato ya asilimia tano kutoka michezo ya kubahatisha.

“Lengo letu ni kuutunisha mfuko kwa kuongezea vyanzo vya mapato ili kuleta athari chanya katika maendeleo ya michezo nchini, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya michezo,” amesema.

Amesema watakapomaliza majadiliano watawaeleza wabunge namna ambavyo watakwenda kulitekeleza jambo hilo.

Mwinjuma amesema wajibu wa kupata gharama za kukarabati zinabaki kwa mamlaka husika lakini watakapoingia katika kuzisaidia mamlaka hizo hasa zisizo na uwezo watafanya tathimini kiasi gani kinahitajika.

Related Posts